MENEJA Msaidizi wa Uwanja wa Jamhuri Dodoma , Saidi Kalela,
amezishawishi timu za Ligi Kuu Tanzania Bara na Ligi Daraja la Kwanza
ambazo viwanja vyake vimefungiwa na havifai kutumika kwa mashindano,
viombe kutumia huo.
Viwanja vilivyofungiwa ni Ali Hassan Mwinyi Tabora, Mkwakwani Tanga,
Kaitaba Bukoba, Jamhuri Morogoro, Sokoine Mbeya, Majimaji Songea na
Sheikh Amri Abeid Arusha.
Kalela alijipigia upatu huo, baada ya kuhojiwa na Tanzania Daima
wanafanya jitihada gani ili uwanja huo usikumbwe na panga la Bodi ya
Ligi nchini (TPL-Board), lililovipitia viwanja saba kutokana na
kutokuwa na hali nzuri.
Akijibu, Kalela alijinasibu kuwa anazishawishi timu za Ligi Kuu na
Daraja la Kwanza ambazo viwanja vyake vimefungiwa, ziombe kuutumia
Uwanja wa Jamhuri Dodoma kwa sababu una hali nzuri, sambamba na hamasa
ya wadau kushuhudia mapambano ya soka.
“Mbali ya uzuri wa Uwanja wa Jamhuri, hapa ni katikati ya nchi, pana
mapato ya kutosha, miundombinu inayostahili, unafuu wa maisha na
uwezekano wa kusafiri kokote na kwenda popote katika pembe ya
Tanzania,” alisema Kalela.
Kalela aliongeza kuwa ushirikiano wao mzuri na Katibu wa Chama cha
Mapinduzi (CCM), Mkoa, Albert Mgumba, wanaomiliki uwanja huo, ndio
unaofanya usiwe katika hali mbaya.
“Tumetoa mwanya kwa wadau wetu, kama ninyi waandishi, mashabiki wa
michezo yote, marefa, wachezaji, viongozi wa vyama na serikali,
wananchi, wageni wanaotutembelea kimichezo na wabunge wakiwa bungeni,
kutukosoa na kutuelekeza palipo pabaya ili turekebishe na kupaboresha,”
alisema na kuongeza: “Kimsingi tunakubali changamoto, tukiambiwa pale
panasababisha dimbwi la maji, vyoo au milango ina shida, uchafu na
mahali popote panapohitaji matengenezo, tunakubali kupafanyia kazi kwa
ushirikiano, bila kumrushia huyu koleo la mchanga kuwa ndiye
anayehusika.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment