WATU wenye ulemavu wametakiwa kujiamini kwa kujitokeza na kugombea
nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya Chama cha Watu Wenye Ulemavu
Tanzania (CHAWATA) na nje ya chama badala ya kuwalalamikia viongozi
waliopo madarakani.
Katibu wa Chawata Mkoa wa Dodoma na Kaimu Mwenyekiti wa Chawata
taifa, John Mlabu, alitoa wito huo jana alipokuwa akifungua mkutano wa
uchaguzi wa viongozi wa chama hicho Wilaya ya Dodoma Mjini.
Mlabu alisema watu wenye ulemavu pamoja na kuwa na chama kikubwa,
lakini hawapo tayari kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali na badala
yake wamekuwa mabingwa wa kuwalalamikia viongozi waliopo madarakani
kuwa hawatetei masilahi ya watu wa jamii hiyo.
Kiongozi huyo alisema watu wenye ulemavu wanapaswa watambue wanao
wajibu wa kuwania nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama na nje,
ili kupata wepesi wa kutetea masilahi ya watu wenye ulemavu.
Katibu wa Chawata Wilaya ya Dodoma Mjini, Mchungaji Kalebi Mhawi,
alisema chama hicho kimefanya mambo mengi kwa jamii ikiwa ni pamoja na
kuwezesha kutoa matibabu kwa wale wenye uhitaji.
“Chawata wilaya tumeweza kujitahidi kuwatafuta wafadhili kwa ajili ya
kuwapatia matibabu watu ambao walikuwa ni wagonjwa na wakati mwingine
wagonjwa hao walihitaji fedha nyingi kwa ajili ya matibabu hususan ya
upasuaji,” alisema.
Chanzo;Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment