Home »
» Pinda azitwisha mzigo halmashauri
Pinda azitwisha mzigo halmashauri
|
|
WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, amejivua lawama akisema kuwa
halmashauri ndizo zinasababisha kuchelewesha marudio ya chaguzi za
madiwani na viongozi wa serikali za mitaa na vijiji.
Alisema kuwa ofisi yake kama msimamizi wa Wizara ya Tamisemi
inapopokea taarifa yoyote kuhusu marudio ya uchaguzi na kuifanyia kazi
kwa muda usiozidi hata siku mbili.
Pinda alitoa kauli hiyo jana bungeni mjini Dodoma wakati akijibu
swali la Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe
(CHADEMA) katika kipindi cha maswali ya papo kwa hapo.
Katika swali lake, Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, alimtaka Waziri
Mkuu atoe kauli ni kwanini ofisi yake inashindwa kutatua mgogoro wa
muda mrefu katika Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela jijini Mwanza.
Pia alitaka aeleze ni kwanini ofisi yake imekuwa ikichelewesha
marudio ya chaguzi za madiwani na viongozi wa serikali za mitaa, jambo
ambalo linasababisha wananchi katika kata nyingi nchini kukosa
wawakilishi.
Pinda alikiri kuufahamu mgogoro huo wa Ilemela akisema kuwa matatizo
makubwa ni madiwani wa CHADEMA kufukuzwa na Meya, Henry Matata, na
kwamba taarifa hizo zinafanyiwa kazi.
Alisema kuwa pamoja na taarifa hizo kuendelea kufanyiwa kazi lakini
pia madiwani hao walileta malalamiko kwa njia ya rufaa na kwamba kwa
sasa ofisi yake imeagiza kupatiwa taarifa mbalimbali na kuzipitia na
kisha kutoa maamuzi.
Akifafanua kuhusu kucheleweshwa kwa chaguzi za marudio za madiwani
alisema kuwa ofisi yake haikai na taarifa kwani baada ya kuzipokea
huzipeleka Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
“Kwa kuwa serikali imeweza kuliona jambo hilo kuwa linasababisha
kuwepo kwa mrundikano, itawasiliana na Tamisemi ili kuhakikisha
inafanya utaratibu kwa ajili ya kuangalia uwezekano wa kuondoa huo
mrundikano wa kuwepo kwa chaguzi za madiwani na serikali za mitaa na
vijiji.
Ajibu swali la Mbunge wa Mkanyageni, Mohamed Habib Mnyaa (CUF),
aliyetaka kujua kama Tanzania ina nia ya kuuendelea na ushirikiano wa
Jumuiya ya Afrika Mashariki, Pinda alisema kuna jitihada kubwa
kuhakikisha wanafanya kila linalowezekana ili umoja huo uendelee.
Katika hatua nyingine, Pinda alisema ni ruksa kwa wafanyabiashara wa mazao kuuza mazo yao nje ya nchi.
Pinda alitoa ufafanuzi huo wakati akijibu swali la Mbunge wa
Peramiho, Jenister Muhagama (CCM) aliyetaka kujua kwanini serikali
inekuwa na tabia ya kuwakopa wakulima mazao yao lakini inachelewa
kuwalipa, jambo ambalo linawachelewesha kuendelea na shughuli zao.
Alisema kuwa ni kweli serikali ilikuwa na deni kwa wakulima lakini
hadi sasa imeishatenga sh bilioni 25 kwa ajili ya kuwalipa.
Pinda alisema kuwa kwa sasa serikali imewaruhusu wafanyabiashara kuuza chakula nje ya nchi ilimradi wasiwapunje wakulima.
chanzo;Tanzania Daima
|
|
0 comments:
Post a Comment