RAIS Jakaya Kikwete amesema Tanzania haina mpango wa kujitoa
kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), itaendelea kuwepo licha ya
kutengwa na baadhi ya nchi wanachama.
EAC inahusisha nchi tano washirika za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi
na Tanzania ambapo kwa siku za karibuni wakuu wa nchi za Rwanda, Uganda
na Kenya wanaonekana kuanzisha umoja wao ndani ya jumuiya hiyo.
Alisema anaamini kinachoifanya Tanzania ichukiwe na nchi nyingine
wanachama wa EAC ni msimamo wa viongozi wake kuhusu ardhi, ajira,
uhamiaji na uharakishwaji wa shirikisho.
Akilihutubia Bunge mjini Dodoma jana, Rais Kikwete alisema hataki
mambo yaliyotokea mwaka 1977 yajirudie huku akisisitiza kwamba Tanzania
itaendelea kuwepo kwenye jumuiya hiyo.
Alisema Tanzania inatimiza ipasavyo wajibu wake kwa jumuiya na
kushiriki kwa ukamilifu katika ujenzi wake na utengamano ndani ya EAC
huku akisisitiza kwamba sababu ya wakuu wa nchi hizo tatu kufanya mambo
yasiyohusu jumuiya haieleweki.
“Tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa jumuiya haidhoofiki wala
kufa. Na iwapo itadhoofika au kufa kamwe hatutaki Tanzania inyooshewe
kidole kuwa chanzo wala kichocheo chake.
“Tanzania haijafanya lolote baya dhidi ya jumuiya hiyo au kwa nchi
mwanachama kama kuna ushahidi uletwe… tusingekuwa na sababu ya
kuchangia dola milioni 12 za Marekani kila mwaka, hii ni fedha nyingi,”
alisema.
Aliongeza kuwa viongozi wenzake hao walifanya mikutano mitatu, yaani
Juni 24 hadi 25 mwaka huu, mjini Entebbe-Uganda, mkutano mwingine
walifanya mjini Mombasa-Kenya Agosti 28 na Oktoba 28 walikutana tena
mjini Kigali, Rwanda.
“Wanafanya mikutano hiyo bila kutualika… wanazungumzia masuala ya
jumuiya, nimeambiwa eti huo ni ushirikiano kwa walio tayari, wanasema
tumekuwa kikwazo tunawachelewesha wenzetu kwenye maendeleo.
“Maneno haya yamekuwa yakijirudia lakini hayana ukweli wowote, sababu
zao hazina mashiko,” alisema Rais Kikwete huku akisisitiza kwamba
Tanzania ni mwanachama mtiifu, mwaminifu na mvumilivu kwa jumuiya.
Msimamo wa EAC unaelekeza kwamba nchi mbili wanachama au zaidi
hazikatazwi kuwa na makubaliano ya ushirikiano katika kufanya mambo
mbalimbali.
Alisema kitu cha kushangaza ni pale nchi hizo tatu zinapofanya mambo
yaliyoamuliwa ndani ya EAC, ambayo lazima nchi washirika wakubaliane.
Rais Kikwete aliyataja mambo manane yaliyoamuliwa na wakuu wa nchi za
Uganda, Kenya na Rwanda kuwa ni kujenga reli ya kisasa kutoka Mombasa
hadi Kampala, Kigali na Bujumbura, kuongeza uzalishaji na usambazaji
wa umeme.
Jambo jingine ni ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Kenya hadi Uganda
na Sudan ya Kusini, kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta nchini Uganda,
kuanzisha himaya moja ya ushuru wa forodha wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki na kutekeleza vipengele vyote.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, wakuu wa nchi hizo pia wamekubaliana
kuharakisha Shirikisho la EAC na kwamba itaundwa kamati ya kuandaa
rasimu ya Katiba ya Shirikisho, kuharakisha uanzishwaji wa viza ya
pamoja ya Utalii ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na kutumia vitambulisho
vya taifa kama hati ya kusafiria katika nchi zao.
Alisema mambo hayo yanachanganya yale ya jumuiya na yasiyokuwa, huku
akiyataja mambo manne ya EAC yaliyopo kwenye mipango ya viongozi wa
nchi hizo ‘zinazoisaliti’ jumuiya.
“Hata hivyo bado jukumu la kuzalisha na kusambaza umeme huo
limeachiwa nchi wanachama kuamua…lakini, hivi ndugu zetu hawa wanaona
muhali kuishirikisha Tanzania katika mpango ambao kimsingi umebuniwa na
Jumuiya ya Afrika Mashariki ambayo sote ni wanachama?
“Nimeambiwa kuwa Jumuiya imeshazungumzia bomba la mafuta kutoka
Eldoreti hadi Uganda, Rwanda na Burundi kuwa nalo lifike Tanzania
kupitia upande wa kaskazini magharibi mwa Tanzania.
“Inaelekea mpango huo sasa haupo maana hatujausikia kutajwa katika
ujenzi wa bomba hilo ambalo wenzetu wanalizungumzia,” alisema.
Kuhusu ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Mombasa–Kampala – Kigali –
Bujumbura alisema halina tatizo kwa kuwa si mradi wa EAC, upo chini ya
mamlaka ya nchi wanachama.
Hata hivyo, alisema ni vema kutambua kuwa ujenzi wa miundombinu ya
reli, barabara, usafiri wa anga na majini kuunganisha nchi za EAC ni
miongoni mwa mambo ya kipaumbele cha juu yanayoshughulikiwa na jumuiya
hiyo.
Alisema jumuiya hutengeneza mikakati ya pamoja na ndiyo maana kuna
‘East African Railway Masterplan, inayohusisha East African Road
Network na Lake Victoria Development Programme kwa Ziwa Victoria.
“Lazima nikiri kuwa inashangaza na tunayo kila sababu ya kuuliza kwa
nini wenzetu wameamua kufanya hivi… kimetokea nini tangu tukutane wakuu
wa nchi zote za Jumuiya Arusha Aprili 28 na vikao vyao vilivyoanza
Juni 24 walipoamua kujenga na kuimarisha utengamano wa Afrika Mashariki
kwa kubaguana. Haijawahi kuwa hivi kabla,” alisema.
Alisema uchumi imara ndiyo kichocheo cha nchi kujiunga na kuendelea kuwa mwanachama wa jumuiya yetu.
Rais aliongeza kuwa kabla ya kuanza tena kwa EAC asilimia 78.4 ya
Watanzania waliohojiwa na kamati iliyoongozwa na Profesa Samwel Wangwe
waliunga mkono kuwepo kwa shirikisho huku asilimia 25.4 kati yao
wakitaka uharakishwaji wake.
Wapinzani wamsifu
Kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe (CHADEMA),
alisema amefurahishwa na hatua ya Rais Kikwete kwa kuweka msimamo wa
kutojiondoa katika jumuiya hiyo.
Mbowe alisema msimamo huo ndio wa siku nyingi kwa kambi ya upinzani
kwani kujiondoka katika jumuiya hiyo si jambo la kizalendo.
Hata hivyo, aliitaka serikali kuachana na tabia ya kutotekeleza mambo yake kwa haraka ili kumaliza migogoro mapema.
Mbunge wa Kasulu Mjini, Mosses Machali (NCCR-Mageuzi), alisema kuwa
alichoelezea Rais Kikwete ni sahihi lakini kunatakiwa kuwa na
utekelezaji wa kimaamuzi.
Machali aliongeza kuwa kuna kila sababu ya Tanzania kuona umuhimu wa
kufanya mazungumzo ya kiushawishi kwa ajili ya nchi ambazo zinaonekana
kujitenga ili kuondoa tofauti.
Naye Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa, alisema kwa mara
ya kwanza anaungana na Rais Kikwete kwa kuona umuhimu wa kupambana na
majangili ambao wanaonekana kutokomeza rasilimali ya wanyamapori.
Alisema yeye kama mbunge amekuwa akipiga kelele zaidi juu ya ujangili
ambao unaendelea kuonekana na kusababisha kuwamaliza tembo huku
wahusika wakiwa hawachukuliwi hatua za kisheria.
Kuhusu suala la jumuiya, Msigwa alisema Kikwete anatofautiana na
mawaziri wake ambao walikuwa wakitoa kauli kana kwamba inaweza kuvunjika
muda wowote.
Mbunge wa Viti Maalumu, Naomi Kaihula (CHADEMA), alisema hotuba ya
Rais imekuja wakati mzuri, ambapo kulikuwa na mkanganyiko mkubwa kwa
wananchi na wabunge kwa ujumla.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Amina Makilagi (CCM), alisema hotuba
hiyo ni nzuri na imekonga moyo wake na Watanzania kwa ujumla, kwani
imeweka wazi mambo muhimu ambayo yalikuwa yakipotoshwa.
Chanzo;Tanzania Daima
|
0 comments:
Post a Comment