Malkia Maxima wa Uholanzi (kushoto), akilakiwa
na Mke wa Rais Jakaya Kikwete, Mama Salma, baada ya kuwasili kwa Malkia
huyo jijini Dar es Salaam jana.
Maxima aliwasili jana saa 7:43 mchana kwa ndege katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), jijini Dar es Salaam na kulakiwa na mwenyeji wake, Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete.
Baada ya kuwasili uwanjani hapo, Malkia Maxima, alipokea shada la maua kutoka kwa kijana wa kiume na kisha kutembezwa na mwenyeji wake kwenye zulia jekundu ambalo pembeni mwake limechorwa bendera ya taifa ya Tanzania na kukagua vikundi viwili vya ngoma vilivyoandaliwa rasmi kwa ajili ya kumpokea.
Vikundi hivyo ni pamoja na bendi ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Mgulani na kile cha matarumbeta cha Mount Meru Voice kutoka jijini Arusha.
Baada ya kutoka uwanjani hapo, malkia huyo akiwa na Mama Salma walikwenda moja kwa moja katika Hoteli ya Hyatt Regency kabla ya kwenda Ikulu kwa mazungumzo zaidi.
Ziara ya Malkia Maxima inaanza rasmi leo wakati atakapokwenda kuzindua Karakana Jumuishi ya Kitaifa ya Fedha, itakayofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu nchini (BoT).
Karakana hiyo inalenga kujadili masuala ya kiuchumi ikiwa ni pamoja na kuangalia namna ya kuwasaidia wakulima wadogo wakiwamo wanawake na vijana.
Kabla ya kurejea nchini mwake kesho jioni, Maxima anatarajia kumalizia ziara yake ya siku tatu mjini Dodoma katika Kijiji cha Vigawe, ambako atakagua mashamba ya wakulima wadogo wadogo na kupata fursa ya kuzungumza nao.
Mbali na cheo hicho, Maxima pia ni mwakilishi wa Umoja wa Mataifa (UN) katika mashirika ya kimataifa ya umoja huo ikiwa ni pamoja na lile la Chakula (Fao), Mpango wa Chakula (WFP) na Mfuko wa Maendeleo ya Kilimo na Chakula (Ifad), na kwamba ziara hiyo ililenga zaidi mashirika hayo.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment