Home » » Kisasa watangaza mgogoro wa viwanja

Kisasa watangaza mgogoro wa viwanja

WAKAZI wa eneo la Kisasa ‘C’ Center katika Halmashauri ya Dodoma wametangaza mgogoro wa viwanja kati ya Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) na kamati ya kijiji ya kushughulikia upimwaji viwanja.
Wakazi hao wamemuomba Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka kuushughulikia haraka ili kuepusha madhara yanayoweza kutokea.
Wakizungumza na Tanzania Daima kwa nyakati tofauti katika mkutano waliouitisha kupinga maeneo yao kupewa watu wengine, walisema wanaweka azimio la kuhakikisha hakuna mtu atakayeingia katika eneo hilo kujenga kama wenyeji hawajapatiwa viwanja.
“Eneo hili tangu mababu na mababu tulikuwa tunalima na tunaishi hapa, lakini miaka ya hivi karibuni CDA walikuja na kutueleza wanataka kupima viwanja, ili mji uweze kujengeka katika mpangilio.
“Sisi hatukukataa. Tulitaka kulipwa na kupewa viwanja kwa ajili ya kujenga na kwa kuwa tuna watoto na wajukuu na maeneo haya ni yetu kwa miaka mingi, tulikubaliana kila mtoto ambaye amejenga banda apewe kiwanja jambo ambalo mpaka sasa halijafanyika,” alisema mmoja wa wakazi hao.
Walisema waliteua kamati ya kufuatilia upimaji wa viwanja, lakini cha kushangaza hawajapewa viwanja badala yake wamepewa wageni.
Balozi wa mtaa huo, Wiston Kyeju, alisema kitendo cha wakazi wa maeneo ambayo yalipimwa viwanja kukosa na kupatiwa watu wengine kinaweza kusababisha uvunjifu wa amani.
Grest Wiston aliituhumu kamati ya kijiji ya kusimamia viwanja kwa madai wamefanya kinyume na matarajio ya wananchi ambao waliamini watawasaidia kuwatetea kupata viwanja.
Chanzo;Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa