Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari.PICHA|MAKTABA
Dodoma.Sakata la wabunge waliochukua posho kwa
ajili ya safari za mafunzo nje ya nchi na kuacha kusafiri, limeingia
hatua mpya baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda kuwataka wazirudishe.
Katika orodha ya wabunge wanaotajwa katika sakata
hilo, wamo baadhi ya wabunge wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema), Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha NCCR-Mageuzi.
Sakata hilo liliibuliwa bungeni wiki iliyopita
mjini Dodoma na Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy (CCM) wakati
akichangia taarifa ya Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa
(Laac).
Keissy alisema baadhi ya wabunge wanapaswa
kuchunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kwa
kuchukua posho za safari za nje ya nchi lakini hawakwenda safari hizo.
Mbunge huyo alifafanua kuwa mbali na kutokwenda
kabisa safari hizo, lakini wapo ambao walikwenda na hawakukaa siku zote
zilizopangwa.
“Tunawajua na wapo humu ndani,” alisema huku
baadhi ya wabunge wakipaza sauti wakitaka awataje, lakini yeye akasema
siyo jukumu lake kuwataja kwani Ofisi ya Bunge inawajibika kufanya
hivyo.
Mbunge huyo alienda mbali na kudai mbunge mmoja
alikatisha safari ya kwenda Marekani na kuamua kwenda Dubai kwa safari
binafsi ambayo haikuwepo katika ratiba ya ziara hiyo ya mafunzo.
Habari za uhakika zilizopatikana jana zilisema
wabunge wanane walichukua posho ya safari ya kati ya Sh5 milioni na Sh6
na Spika amewaandikia barua akiwataka warudishe fedha hizo.
Majina ya wabunge hao tunayo, lakini kwa sababu za
maadili ya uandishi wa habari, gazeti hili halitaweza kuwataja kwa kuwa
hawakupatikana ili kujibu tuhuma hizo kama maadili yanavyoelekeza.
Akizungumza na gazeti hili ofisini kwake bungeni
mjini Dodoma jana, Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel, alisema kuwa Spika
ameshaliona jambo hilo na kulichukulia hatua za kiutawala.
“Spika amewaandikia barua akiwataka kurejesha
fedha zote za safari ambazo hawakwenda. Ni lazima wazirudishe hakuna
namna,” alisema Joel ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Shughuli za
Bunge.
Alipoulizwa kuhusiana na majina yao na kiasi
walichochukua, Joel alisema hilo ni jambo la kiutawala na kwamba Spika
ndiyehuarifiwa na kamati kuhusiana na wabunge ambao hawakusafiri
“Spika ndiye anayearifiwa na wenyeviti wa kamati husika juu ya
wabunge waliosafiri na wasiosafiri kwa sababu wao ndiyo wanapanga safari
na sisi tunawapa posho,” alisema.
Akizungumzia malalamiko ya wabunge juu ya baadhi
ya wabunge wasiofika bungeni kusaini ili wapate posho ya kikao, Joel
alisema tatizo hilo limepungua kwa kiasi kikubwa.
“Lilikuwepo lakini limepungua kwa kiasi kikubwa
baada ya kugundua wakifika kwenye malipo majina yao waliosainiwa
yamekatwa,” alisema Joel.
Alipoulizwa kuhusiana na tatizo hilo la kupokea
posho za safari za nje ya nchi bila kwenda, Mnadhimu wa Kambi ya Rasmi
ya Upinzani bungeni, Tundu Lissu alisema kuwa bado hajapata taarifa
hizo.
“Lakini muhimu hapa ni Bunge kuandaa utaratibu wa
kurejesha mrejesho wa jinsi walivyozitumia na hapo ndipo watagundulika
wabunge wanaosafiri kweli na muda waliokaa mahali husika,” alisema
Lissu.
Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari
(Chadema) ambaye anatajwa kuwemo kwenye orodha ya wabunge waliopokea
posho bila kusafiri, alikiri na tayari alishamuandikia barua Katibu wa
Bunge akimueleza kwamba hakusafiri na kuomba utaratibu wa kurejesha
fedha hizo.
Nasari alisema yeye alikuwa Jimboni kwake kwa
shughuli za wananchi wake, hivyo hakuweza kusafiri na suala hilo
alilifikisha mapema kwa Katibu ili ampe maelekezo namna ya kurejesha
fedha hizo
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment