Na.Mhariri wa MOblog
Ingawaje Tanzania inaitwa nchi masikini
pamoja na kwamba wahisani na wadau wa maendeleo wanasema ni nchi
inayoendelea lakini kwa ujumla na kwa yeyote anayeijua nchi yetu kwa
maana ya hali ya maisha ya wananchi wake, ni jambo la hatari kwa kikundi
kidogo cha watu waliokalia ofisi za umma na kujipangia utaratibu fulani
wa kujinufaisha.
Kikundi hiki kidogo tena kilichochaguliwa na
wananchi kama wawakilishi wao (wabunge) na ndio watunga sheria
kujinufaisha kwa jasho la walipa kodi kwa kisingizio cha sheria ambazo
wametunga wao wenyewe kwa kujipendelea.
Ni aibu zaidi kusikia kwamba wabunge wengi
na hata baadhi ya mawaziri kukejeli juhudi binafsi za baadhi ya wabunge
wa Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania wenye kuogopa kodi za
wananchi na kutaka mabilioni hayo kuelekezwa katika miradi ya maendeleo
ya wananchi kwa maslahi mapana ya taifa.
Tumeamua kusema hayo bila kuficha kwamba ni
muhimu kwa Serikali pamoja na Bunge kufikiri upya mtindo huu wa kifisadi
wa kulipana posho ya kukaa (Sitting Allowance) wakati wana mishahara
mikubwa kuzidi wafanyakazi wenye kufanya kazi usiku na mchana kama vile
madaktari wanaosubiri kulipwa posho ya (overtime) ya shilingi elfu kumi
ambayo hukaa hadi miezi mitatu mpaka sita haijalipwa.
Tunasema na kusisitiza kuwa ujira wa vikao
ambavyo ni kazi halali za ubunge ni mshahara na si posho! Posho ni wizi
wa fedha za umma mchana kweupe kwa sababu kazi ya Mbunge ni uwakilishi
na pale anapokaa kwenye vikao vya bunge na kamati mbalimbali anatimiza
wajibu wake kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi iweje alipwe Posho?
Mwaka juzi kwenda mwaka jana 2011/2012
Serikali ililiomba Bunge kupitisha sh bilioni 987 kwa ajili ya psoho
mbalimbali za watumishi wa Serikali wakiwamo wabunge. Hii ni hatari kwa
mustakabali wa taifa changa kama Tanzania.
Huu ni kweli kwamba mabilioni ya shilingi
zikiwa ni kodi za wananchi kila mwaka wa fedha yanatengwa kwa ajili ya
posho tu, na hata mwaka jana Benki ya Dunia na wahisani wa maendeleo
walihoji uwepo wa posho za kukaa kwa watumishi wa serikali na wabunge
lakini bado tatizo hili la kuzoea posho linaitafuna nchi yetu bila
huruma.
Serikali kupitia wizara ya fedha mwaka
2011/2012 iliahidi kwamba posho ambazo hazina tija zitaondolewa kauli
iliyoonekana kama mwanzo wa mageuzi ya kweli, lakini leo asubuhi
niliposikia kipindi cha tuongee magazeti juu ya Wabunge kutafuna posho
ovyo wote wa chama tawala na upinzani ni ishara kwamba serikali ilitaka
kauli ile ieleweke kinyume nyume.
Gazeti la kila wiki la Raia Mwema limeongoza
leo na habari za wabunge kutafuna posho hovyo hovyo na Mbunge kijana
Joshua Nasari amekiri kwamba alichukua posho ya kwenda safari Malaysia
lakini ikatokea dharula ya Harambee jimboni kwake akaona ni busara
kujumuika na wananchi wake bravo kwake.
Bila kutafuna maneno Tanzania ni nchi
maskini, kwani kipato cha mwaka cha mwananchi wa kawaida ni Sh 770,463
hivi, wastani wa kama Sh 2,140 kwa siku, kwa mantiki hiyo Mtanzania wa
kawaida kuishi katika maisha ya leo kwa kipato hiko ni kwa kudra za
mwenyezi mungu kama si rushwa dogo dogo zinazomwezesha kumaliza mwaka.
Lakini wakati wananchi walio wengi wakiishi
katika umaskini wa kutupa, wapo watu waliaomua kusaka nafasi za uongozi
katika nchi hii si kwa nia ya kusaidiana na wananchi kutokomeza umaskini
ulioelemea taifa hili, ila kujitenga nao kwa kutengeneza utaratibu
mbaya na kandamizi wa kujilipa mafao manono kama hizi zinazoitwa posho
za vikao za wabunge.
Kwa maelezo yoyote yale, posho hizi si
halali hasa zinapolipwa na taifa maskini kama Tanzania ambalo haliwezi
hata kujitegemea kwa kuwa na bajeti yake walau kwa mwaka mmoja tu bila
kutembeza bakuli kwa wafadhili ili kufanikisha miradi mbalimbali ya
maendeleo.
Kwa mtanzania yeyote makini atakubaliana
nasi kwamba walioweka utaratibu huu ama walipotea njia kwa ama
walitanguliza mbele maslahi binafsi lakini wananchi wameamka na wanajua
kinachoendelea na wanawasubiri 2015 kwenye uchaguzi watawaita wabunge wa
posho na vitambi vya posho kama si mchemsho na kiti moto na bia kaeni
chonjo uchaguzi unakuja!
Na kuna taarifa za kutisha kwamba siku hizi
hata kazi ambazo ni wajibu wa watumishi wa umma kuzifanya watu hawafanyi
mpaka kuwepo na posho (Bahasha) yaani ofisa wa serikali kukaa kwenye
kikao cha kazi ambayo ni wajibu wake, anadai mshiko tumekwisha!
Kwa utaratibu huu watanzania itatuchukua
muda mrefu mpaka kuja kupata maendeleo ya kweli na hakuna jambo lolote
linalokwamisha uwezo wa serikali kutimiza wajibu wake zaidi ya maposho
yasiyo kuwa na kichwa wala miguu ndugu zangu tukafanye kazi tuliotumwa
na wananchi tuache rongo rongo za posho zisizo kuwa na tija kwa maslahi
ya vizazi vya sasa na vijavyo.
Naomba kuwasilisha !
Damas Makangale
Mhariri Mkuu
0 comments:
Post a Comment