Home » » BUNGE LA KATIBA LAVUNJIKA

BUNGE LA KATIBA LAVUNJIKA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

TAARIFA ya kuwepo kwa marekebisho mapya ya Kanuni za Bunge Maalumu la Katiba, zimesababisha vurugu, kurushiana matamshi yasiyo ya staha na kuzomeana bungeni, huku Mwenyekiti wa Bunge Maalum, Samuel Sitta, akituhumiwa kushiriki kuchakachua Kanuni hizo.
Hali hiyo ilijitokeza jana jioni, baada ya Sitta kuruhusu mwongozo kutoka kwa Mjumbe wa Bunge hilo, Tundu Lissu, ambaye alidai kuwa na waraka wenye mapendekezo ya marekebisho hayo.
Akiomba mwongozo, Lissu alisema unahusu kukiukwa kwa kanuni kunakofanywa na kiti, ambacho kimekuwa kikiyumba.
Lissu alisema wakati Kanuni za Bunge Maalum zilipopitishwa kwa azimio la Bunge, waliacha kiporo cha kanuni mbili pekee za 37 na 38, ambazo zinahusu namna Bunge litakavyofanya uamuzi kwa kupiga kura za wazi au za siri.
Alisema ameshangazwa kuona jedwali la mapendekezo ya marekebisho ya Kanuni za 32, 33, 35, 37, 38, 58, 63 na 64. Lissu alisema utaratibu uliotumika kufanya marekebisho hayo, umekiuka kanuni kwa kuwa mabadiliko hayo, yameletwa na Katibu wa Kamati ya Uongozi.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 87 (2), marekebisho hayo yalipaswa kuletwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge.
“Mwenyekiti, hii Kamati ya Uongozi haina mamlaka ya mambo ya Kanuni…hii takataka, huu ubatili usiingie katika Bunge hili, hatuwezi kuruhusu uchafu wa aina hii,” alisema Lissu huku akipigiwa makofi na wajumbe wengine wakizomea.
Bulembo Mjumbe Abdallah Bulembo alisema wajumbe wote ni watu wazima na vikao vya kuzomeana, havisaidii Watanzania.
“Huu ni utaratibu gani wa vikao wa kihuni? Kama ni vya Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi), na hawataki waondoke… kuzomeana si kanuni,” alisema.
Waziri wa Sheria na Katiba wa Zanzibar, Abubakar Khamis Bakary, alisema Bunge linapaswa kuendeshwa na kanuni na Kanuni ya 87.2, imeweka utaratibu wa kubadili kanuni.
“Hili Bunge tunaliheshimu, hivyo ni muhimu tufuate kanuni…haiwezekani tupitishe kanuni juzi, leo tubadilishe kinyemela,” alisema Abubakar.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jaji Fredrick Werema alisema Kanuni ya 87 (1) inaruhusu Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge, kuleta marekebisho na ndiye aliyekuwa akisubiriwa kufanya hivyo.
Mjumbe Ismail Jussa Ladhu alisema jedwali hilo la marekebisho, limesainiwa na Katibu wa Kamati ya Uongozi na si Mwenyekiti na kuhoji iweje Kanuni hazijafanya kazi, zionekane zina upungufu? “Tulivutana sana, tukapata maridhiano…kumbe ni unafiki, Mwenyekiti aliyepita, leo ndio Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni…hatutakubali,” alisema Jussa.
Kutokana na hali hiyo na vurugu zilizokuwa zikiendelea, Sitta aliahirisha Bunge mpaka leo saa 10 jioni na kuelekeza malalamiko hayo, yapelekwe katika Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge.
Awali, wakizungumza na waandishi wa habari kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa jana, katika kikao kilichojumuisha viongozi wakuu wa Ukawa, Freeman Mbowe, Profesa Ibrahim Lipumba na James Mbatia, Msemaji wa Ukawa na Tundu Lissu, alisema Ukawa haukukubaliana na hautakubaliana na mabadiliko, yanayotaka kuingizwa kwenye Kanuni za Bunge hilo.
Chanzo:Habari leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa