Home » » SITTA:KUNAMPANGO KUVURUGA BUNGE

SITTA:KUNAMPANGO KUVURUGA BUNGE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

MWENYEKITI wa Bunge Maalum la Katiba, Samwel Sitta amefichua siri za kuwepo kwa mipango ya siri, inayodaiwa kufanywa na wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kuvuruga mchakato wa kuundwa kwa Katiba mpya.
Sitta ambaye anachukuliwa kama mwanasiasa imara na mkongwe na mwenye uwezo wa kuwaunganisha Watanzania bila kujali itikadi zao za kisiasa, amesema kwamba hali inayoendelea ndani ya Bunge hilo ni hatari kwa demokrasia ya Tanzania.
Alisema hayo mjini hapa jana, muda mfupi baada ya kuahirishwa kwa kikao cha Bunge hilo Maalum la Katiba.
Alikiahirisha baada ya Ukawa chini ya Msemaji wake, Tundu Lissu, kupinga mabadiliko ya kanuni yaliyopangwa kuwasilishwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge, Pandu Ameir Kificho.
“Sasa nadiriki kusema ipo nia ovu, ya wazi kabisa ya kutaka kuzuia dhamira ya dhati ya Rais wetu (Jakaya Kikwete) ya kuwaachia Watanzania urithi wa Katiba mpya. “
Aibu hii iliyotokea leo (jana) inadhihirisha wazi kuwepo kwa kikundi hiki cha wanasiasa wachache ambao wamedhamiria kuvuruga mchakato huu. Tuhuma za leo (jana) ambazo Lissu amezielekeza kwangu ni za uongo, uzushi na hazikunitendea haki,” alisema Sitta.
Alisema ni jambo la kushangaza kuona kuwa wakati Kanuni zinamruhusu hata mjumbe wa kawaida kuwasilisha mabadiliko ya kanuni, lakini Kundi la Ukawa linazuia hata Mwenyekiti wa Bunge hilo, kuwasilisha mapendekezo ya kanuni, ambayo hata hivyo huwasilishwa kwenye Bunge zima na Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge ili kutolewa uamuzi.
“Kanuni ya 58 na ile ya 59 inasema wazi, Mwenyekiti na Kamati ya Uongozi wana jukumu la kuendesha Bunge, sasa inakuwaje kanuni hizo zimpe Mwenyekiti uwezo wa kuendesha Bunge bila kumpa mamlaka ya kusimamia katika kuona kunakuwa na kanuni nzuri? Alihoji.
Alisema kilichowasilishwa na Lissu bungeni jana ni waraka wa mawasiliano baina ya Kamati ya Uongozi na Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge na siyo kweli kwamba waraka huo ungewasilishwa bungeni, bali baada ya kufanyia kazi mapendekezo hayo ya Kanuni, Kamati ya Kanuni ingeandaa waraka ambao ndio ungewasilishwa na kufanyiwa uamuzi na Bunge zima.
Alisema si hoja ya msingi kwamba mabadiliko ya kanuni hayawezi kubadilishwa ndani ya wiki tatu tangu kupitishwa, kwani kanuni zinaendana na haja ya wakati husika.
Alitoa mfano wa Kanuni ya 87 ambayo ilizua utata, kutokana na kutokuwa na kipengele kuruhusu kiongozi wa kitaifa au rasmi kuingia bungeni, ambapo marekebisho ya sasa yanataka kuweka kipengele cha kuruhusu.
“Ni dhahiri kwamba Ukawa inatumika vibaya na hata ukiangalia kirefu chake kinasema Umoja wa Katiba ya Wananchi. Jina tu linaonesha kiburi fulani, yaani wachache hawa ndiyo wanapigania Katiba ya wananchi sasa wengine wote ndani ya Bunge wanataka Katiba ya nani?” Alihoji.
Chanzo:Habari leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa