Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ni moja ya makundi ambayo
yamekuwa na sauti kubwa katika Bunge la Katiba linaloendelea mjini
Dodoma.
Umoja huu unaundwa na wajumbe kutoka vyama vya
upinzani na baadhi ya wawakilishi wa makundi yaliyoteuliwa na Rais
Jakaya Kikwete na baadhi ya wabunge wa CCM.
Julius Mtatilo ni katibu wa muda wa kundi hilo.
Katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Mtatiro anaeleza mambo kadhaa
yanayohusu umoja huo kama ifuatavyo;
Swali: Katika siku za karibuni Ukawa ni moja ya
makundi ambayo yamekuwa yakitajwa sana kwenye Mchakato wa Katiba Mpya.
Je, nini maana yake na ulianza lini?
Jibu: Ukawa ni kifupi cha Umoja wa Kutetea Hoja za
Wananchi zilizopo kwenye Rasimu ya Katiba ambayo imewasilishwa bungeni
na Jaji Joseph Warioba.
Swali: Umoja huu umeanzishwa lini na kwanini ulianzishwa?
Jibu: Ukawa ulianzishwa mara tu baada ya kufika
bungeni na kuona wenzetu CCM wana misimamo yao kuhusu Rasimu ya Katiba
na wamekuwa wakikutana na kutoa maoni tofauti na Rasimu ya Katiba.
Tulipobaini hilo, tukaona ni busara kuanzisha Ukawa ili kutetea maoni ya
wananchi katika rasimu.
Swali: Je, umoja huu una jumla ya wanachama wangapi?
Jibu: Umoja huu ulianzishwa ukiwa na wanachama 203
na hadi sasa tuna jumla ya wanachama 286, kati yao kuna wabunge wanne
wa CCM na tunatarajia wanachama kuongezeka zaidi.
Swali: Je, umoja huu unaongozwa na kina nani, baada ya kupata wazo na kuanzishwa?
Jibu: Ukawa ulichagua viongozi wa muda. Mwenyekiti
ni James Mbatia na mimi ni katibu. Pia kuna wenyeviti wenza kama
Profesa Ibrahim Lipumba na Freeman Mbowe na yupo Tundu Lissu na wengine
wengi.
Swali: Je, mna mpango wa kufanya uchaguzi ili kuwa na viongozi wa kudumu hadi mwisho wa Bunge hili maalumu?
Jibu: Ndiyo hivi sasa tunajiandaa kwa uchaguzi ambao tunahitaji
ukusanye makundi yote yenye uwakilishi hapa bungeni ili kuwa na sauti ya
pamoja.
Swali: Katika siku za karibuni Ukawa mmekuwa
mkitajwa kuwa sehemu ya makundi ambayo yanaweza kuleta vurugu bungeni
nini maoni yako?
Jibu: Hapana, sisi malengo yetu makubwa ni kutetea
hoja za wananchi, kanuni za bunge na taratibu bila kujali misimamo ya
vyama vyetu. Sasa unavyofanya hivyo kila mtu anatafsiri yake, lakini
wanaojua ukweli wameona mchango wetu katika katiba hii.
Swali: Ni jambo gani kubwa ambalo mnadhani Ukawa mmefanya tangu kuanza kwa Bunge maalumu la katiba?
Jibu: Tumefanya mengi lakini, kubwa lilikuwa ni
kushinikiza Jaji Warioba kupewa muda wa kutosha katika kuwasilisha
Rasimu ya Katiba, kama ambavyo uliona Mwenyekiti alivunja Kanuni ya
47(a) ambayo ilimtaka afanye mawasiliano na Jaji Warioba ili kumpangia
muda ambao unafaa kusoma rasimu.
Lakini Mwenyekiti alimpangia saa moja tu na baada
ya malalamiko yetu, aliongeza saa mbili. Tulipinga na hata kusababisha
kusitishwa Bunge siku ambayo Jaji Warioba alipangiwa kuwasilisha rasimu
ya pili.
Swali: Kwa nini mlizuia Jaji Warioba kusoma rasimu na baadaye mkaja kukukubali?
Jibu: Naomba hapa nieleze Ukawa ilikuwa haimzuii
Jaji Warioba kusoma Rasimu, ila ilitaka apewe muda wa kutosha kwani
tulijua muda wa saa mbili yasingetosha na ukweli baadaye ulijionesha
alitumia zaidi ya saa tatu.
Lakini kabla ya uamuzi huo, tuliomba kuonana na
Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba Samuel Sitta ambaye alitupuuza na
hata tulipoandika barua pia alipuuza na tulikuwa hatuna njia nyingine ya
kumpatia fursa nzuri Jaji Warioba zaidi ya sote kusimama bungeni.
Pia tulikuwa na hoja ya kupinga kuvunjwa kanuni ya
71(1)(g) na (h) ambayo ilitaka Baada ya Rais Jakaya Kikwete kuzindua
bunge ndipo Jaji Warioba awasilishe rasimu.
Swali: Je maombi yenu baada ya kusitishwa bunge yalifanikiwa.
Jibu: Tulifikia maridhiano ambayo yamekuwa na
manufaa makubwa kwa Watanzania,kwani Jaji Warioba alipewa muda wa
kutosha kuwasilisha rasimu na Katiba ya Rais kuendelea kama awali hapa
ilikuwa ni “Give and take” na hapo ndio utaona umuhimu wa kuwa na chombo
kama Ukawa.
Swali: Baada ya Jaji Warioba kuwasilisha rasimu je imekidhi matakwa yenu?
Jibu: Jaji Warioba na tume yake wamefanya kazi kubwa sana na hakika wamewasilisha bungeni maoni ya wananchi na sisi tumeridhika.
Swali: Katika siku za Karibuni zimepitishwa kanuni
za bunge kuhusiana na masuala ya nidhamu bungeni na Mwenyekiti wa
bunge, ameonya kuchukuliwa hatua kali kwa watakaoleta vurugu ni nini
maoni yako?
Jibu: Ni kweli tumepitisha kanuni na hatuna shida
na hili, lakini tuna matatizo na kauli za vitisho ambazo zinatolewa.
Kwanza hapa lazima ieleweke sote sisi ni watu wazima hivyo, mambo ya
kutishana si vizuri.
Swali: Kwa hiyo mtaendelea kusimamisha bunge kwa kusimama na kuomba miongozo kama kanuni zikikiukwa?
Jibu: Kama nilivyosema awali tutahakikisha
tunasimamia kanuni na taratibu hivyo hatutakubali kuburuzwa kwani sisi
tunawakilisha wananchi na kutetea maoni yao yaliyopo kwenye rasimu pia
kanuni na taratibu ambazo tumejipangia.
Huu ndio Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa)
lakini je utafikia malengo yake ya kutetea kile wanachokieleza maoni ya
wananchi yaliyopo kwenye rasimu ya Jaji Warioba, tusubiri vikao vya
bunge vinavyoendelea.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment