Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Lawrence Mchome
ameipongeza Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kukubali kuingiza katika
Katiba Mpya ibara inayotaka kuanzishwa kwa Mahakama ya Juu nchini.
Kama itapitishwa, mahakama hiyo itakuwa ndiyo ngazi ya mwisho ya rufaa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Pamoja na mambo mengine, mahakama hiyo itasikiliza
na kuamua mashauri yanayohusu matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano.
Pia itasikiliza na kuamua mashauri
yatakayowasilishwa na wananchi, Serikali au Serikali za washirika kuhusu
tafsiri au utekelezaji wa Katiba Mpya kama itapitishwa na wajumbe wa
Bunge Maalumu la Katiba.
“Kenya na Uganda wanayo mahakama kama hiyo kwa
hiyo sisi (Tanzania) tulikuwa tukienda Mahakama ya Rufaa ya Afrika
Mashariki, tulionekana wanyonge kwa sababu tumeishia hatua mbili za
rufaa,” alisema Jaji Mchome.
Jaji Mchome, ambaye ni rais wa zamani wa Chama cha
Mahakimu na Majaji Afrika Mashariki (EAMJA), alisema kuwapo kwa
mahakama hiyo kutasaidia kuweka utawala sawa wa sheria katika nchi za
Afrika Mashariki.
“Wenzetu Kenya na Uganda wana hatua tatu za rufaa
kabla ya kufika Mahakama ya Rufaa ya Afrika Mashariki, lakini sisi tuna
mbili tu; Mahakama Kuu ya Tanzania na Mahakama ya Rufaa,” alisema Jaji
Mchome.
Jaji Mchome alisema kama ibara hiyo itapitishwa na
wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, itaifanya Tanzania kuwa na hatua za
sheria zinazolingana na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
(EAC).
“Hata mitalaa ya vyuo vya sheria katika nchi zetu
za Afrika Mashariki, zinatakiwa zifanane sambamba na nchi hizo kuwa na
hatua za rufaa zinazofanana kati ya Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda na
Burundi,” alisema.
“Tukishafanya hivyo, tutakuwa tumepatanisha haki
na uendeshaji wake na kufanya hatua zote za sheria zilingane na hivyo
haki itakayokuwa inatolewa kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika
Mashariki italingana,” alisisitiza.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment