Home » » Kuchaguana kwa jinsia sio sahihi

Kuchaguana kwa jinsia sio sahihi

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Majuma matatu yamepita tangu kuanza kwa Bunge Maalumu la Katiba, wajumbe wa Bunge hilo la kihistoria wamekuwa wakifanya kazi moja tu, kutunga kanuni bora za uendeshaji.
Kamati ya Kanuni, ikiongozwa na Profesa Costa Ricky Mahalu imejitahidi kufanya kazi nzuri, hasa ya kuwarudisha wajumbe katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Sina tatizo sana na sehemu kubwa ya kanuni hizo, tatizo langu ni kundi la wajumbe wanawake kudai haki zaidi kwenye kanuni hizo hata ambazo sasa zinakwenda kinyume na sheria na Katiba ya nchi.
Nilifuatilia kwa karibu sana michango ya baadhi ya dada zangu na wengine ambao nadiriki kusema wana umri sawa na mama yangu, lakini haki walizozidai zilivuka mipaka.
Wakati wakichangia Rasimu ya Kanuni, baadhi ya wajumbe wa jinsi hiyo walikwenda mbali na kutaka Mwenyekiti wa Bunge akiwa mwanaume, makamu wake awe mwanamke.
Hawakuishia hapo, kwani walitaka hata kama mwenyekiti wa Kamati ya Bunge anakuwa mwanaume, basi makamu wake awe mwanamke.
Hoja kubwa waliyoijenga hapa ni kwamba wanataka usawa wa jinsia, hata kama kwa kudai haki hiyo inakwenda kinyume na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba au Katiba ya Nchi ya mwaka 1977.
Ni vizuri nikatumia fursa hii kuwarudisha wajumbe waliokuwa wakipaza sauti, huku wakitoka mapovu wakidai usawa huo, juu kuwapo kwa kifungu cha 23 (A) cha sheria ya mabadiliko ya katiba sura ya 83.
Sehemu ya pili ya kifungu hicho inasomeka hivi: ‘Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, watachaguliwa kutoka miongoni mwa wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba.”
Kifungu hicho hicho kinaeleza zaidi kuwa “endapo mwenyekiti anatoka upande mmoja wa Jamhuri ya Muungano, basi makamu wake atakuwa mtu anayetoka upande mwingine wa Jamhuri ya Muungano”.
Sifa ya mtu anayestahili kushika wadhifa huo imeainishwa katika kifungu kidogo cha tatu cha sheria hiyo kuwa atapaswa kuwa amehitimu shahada kutoka chuo kikuu kinachotambulika.
Sheria hiyo pia inataka mwenyekiti huyo au makamu wake, awe amethibitika kuwa na uzoefu na ujuzi wa kuongoza mihadhara au mabaraza. Hakuna jinsia hapo.
Kwa mtazamo wangu naona haikuwa sahihi kwa wajumbe kutaka viongozi kuchaguliwa kwa jinsia.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa