Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Matarajio ya Bunge Maalumu la Katiba kukamilisha kanuni kwa
maridhiano yaliyeyuka tena jana huku mambo ndani ya ukumbi yakionekana
kuwa vululuvululu kwa baadhi ya wajumbe kuzungumza nje ya utaratibu na
wengine kurushiana vijembe.
Baadhi ya wajumbe waliamua kutoleana lugha chafu
na kuweka kando hoja za msingi zinazowafanya watofautiane na
kuchelewesha kazi ya kuandika Katiba Mpya.
Hali ilichafuka mchana wakati wajumbe walipokutana
kupitisha kanuni baada ya mmoja wao, Felix Mkosamali kuomba mwongozo
kwa Mwenyekiti wa muda, Pandu Ameir Kificho. Hata hivyo, Kificho
alimtaka kukaa chini kwa muda kwa maelezo kuwa wajumbe waliofika katika
kikao hicho walikuwa wachache, hivyo mwongozo wake kama ulikuwa
unahitaji majibu ingekuwa vigumu kutolewa.
Baada ya muda alisimama, James Mbatia na kuomba
mwongozo, akihoji sababu za kutaka kuanza kikao cha kupitisha kanuni
hizo wakati wajumbe hawajapewa vitabu vya rasimu ya kanuni zenyewe.
“Mwenyekiti ulitangaza asubuhi kuwa tutagawiwa
kanuni kabla ya saa tisa lakini hadi sasa tunataka kusomewa kanuni
wakati hatujagawiwa kanuni hizo,” alihoji Mbatia.
Kificho alitoa ufafanuzi kuwa kanuni hizo zilikuwa
bado zinadurufiwa na kuwataka wajumbe wawe na nidhamu kwani
anapotangaza wanapiga kelele.
Ghafla alisimama Mkosamali tena na kuwasha kipaza
sauti na kuhoji kitendo cha mwenyekiti huyo kumpa Mbatia nafasi ya kutoa
mwongozo wakati yeye amenyimwa... “Mwenyekiti hivi unaongozaje kikao,
inakuwaje mimi nikuombe mwongozo uninyime na mwenzangu umpe? Mwenyekiti
nakuheshimu sana, lakini sijui unatumia kanuni ipi kutoa nafasi kwa
mjumbe wakati mimi ulinizuia nisiseme,” alihoji Mkosamali.
Baada ya kauli hiyo Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu, Hawa Ghasia aliwasha kipaza sauti na kwa sauti ya juu
alisema “Mtoto mdogo hana adabu.” Kauli hiyo iliibua hasira za Mjumbe
mwingine, Moses Machali ambaye naye aliwasha kipaza sauti na kumjibu:
“Kubwa jinga halina adabu,” kauli iliyoibua miguno ndani ya Bunge.
Hata hivyo, licha ya Mwenyekiti kutoa onyo kwa
kauli hizo kwamba hazifai, Mkosamali alisimama katika sehemu yake na
kusema kuwa hakuna mtoto mdogo na kwamba tangu lini mtoto aliishinda
CCM.
Chanzo cha tatizo
Chanzo cha mvurugano huo ambao wiki iliyopita
kidogo usababishe ngumi kurushwa bungeni, ni mfumo wa upigaji kura
katika kupitisha ibara za rasimu, ambao jana uliendelea kuwagawa wajumbe
na kufanya ukumbi huo kuonekana kama eneo la mzaha.
Kauli za ‘ndiyoooo’, ‘hapanaaaa’ na vitendo vya
kugonga meza viliongezeka katika kipindi cha asubuhi baada ya Mwenyekiti
wa Kamati ya Kuandaa Kanuni, Profesa Costa Mahalu kuwaleza wajumbe kuwa
kamati yake haijafikia mwafaka wa ama iwe kura za siri au wazi na
kwamba suala hilo limerejeshwa kwa wajumbe wenyewe.
Profesa Mahalu alisema uamuzi unaachwa mikononi mwa Kamati ya
Kudumu ya Bunge itakayoundwa baadaye. Alisema ili Bunge lisonge mbele
baada ya kukwama kwa takribani wiki nzima, vifungu namba 37 na 38
vilivyozua utata vimerekebishwa.
“Tulizungumzia kanuni ya 37 na 38 zinazoelezea
utaratibu kufanya uamuzi. Kanuni hizo sasa zitaeleza tu kwamba utaratibu
wa uamuzi utakuwa ni wa kura, bila kusema ni ya siri ama ya wazi,”
alisema na kuongeza: “Lakini tumeona ni vizuri tukaweka fasili nyingine
katika kifungu cha 38 ambayo itaeleza waziwazi kwamba ni aina gani ya
kura itakayotumika na kwamba hiyo itategemea itakavyoamuliwa na Bunge
hili.
Wajumbe wapinga
Mjumbe Profesa Ibrahim Lipumba ambaye pia ni
Mwenyekiti wa CUF, alisema walichokubaliana katika Kamati ya Mashauriano
ni kinyume na kilichoelezwa na Kamati ya Profesa Mahalu.
Alisema walikubaliana kuwa kifungu cha 37 na 38
visomeke kuwa mambo nyeti yaliyomo katika rasimu ya Katiba, yapigiwe
kura ya siri na ya kawaida yapigiwe kura ya wazi.
“Tulichokubaliana ni tofauti kabisa na hiki
ambacho kamati imekiwasilisha. Hatuwezi kufanya uamuzi wakati
hatujafikia mwafaka,” alisema Profesa Lipumba.
“Huku ni kukwepa uwajibikaji na haiwezekani
tupitishe kanuni wakati baadhi ya vifungu havijakamilika. Kamati
imepinga makubaliano yetu,” alisema.
Mjumbe David Kafulila alisema: “Kwa namna
tunavyokwenda, hakuna kinachoendelea, bado pande mbili zinavutana na
kusababisha masuala yakwame. Tukikutana jioni (jana) na bado hali ni hii
ya kupata taarifa nusunusu ambazo hazina mwafaka kuhusu jambo hili,
tukubaliane kwamba semina hii isimame kwa muda, watu warudi majumbani
kwao ili wafanye makubaliano huko nje.”
Mwenyekiti Kificho alimjibu akisema Rais Kikwete
ndiye aliyeitisha Bunge hilo na kwamba hata uamuzi wa kulivunja
utafanywa na yeye.
Mjumbe Ezekiah Oluoch alisema iwapo Kamati ya
Maridhiano iliyoanza kuketi Ijumaa imeshindwa kukubaliana, kilichopo
sasa ni sekretarieti kuandaa karatasi za kura.
“Kwamba sisi tulikuchagua kwa kutumia kura ya
siri, sasa tupige kura ya siri ambayo itaamua kura ambayo tunaitaka.
Ikiwa tunakuja hapa jioni ukatuletea rasimu ya kanuni ambayo haina
vifungu hivi 37 na 38 vya namna ya kufanya maamuzi, sidhani kama
umetutendea haki kupitisha vitu nusu,” alisema.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera,
Uratibu na Bunge), William Lukuvi alijikuta katika wakati mgumu baada ya
kuzomewa na baadhi ya wajumbe kwa madai ya kuwapotosha.
“Mimi nilivyoelewa wamesema tumepitisha vifungu 85 katika zile
kanuni, vimebaki vifungu viwili 37 na 38 kwa uwiano wowote huwezi kusema
kanuni imeshindwa,” alisema Lukuvi na kuongeza:
“Tumeshaamua vifungu 85 na ili Kamati ya Kanuni
ipate mamlaka ya kufanya marekebisho yoyote ya kanuni, lazima rasimu hii
ipite kwanza.”
Mchango wa Lukuvi ulionekana kuzidisha utata zaidi
kwa wajumbe na hivyo Mwenyekiti Kificho kuwataka wajumbe wa Kamati ya
Kanuni kufafanua zaidi.
Akitoa ufafanuzi kwa niaba ya wenzake, George
Simbachawene ambaye pia ni Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi alidai wajumbe hawakuwa wamemsikiliza vizuri Profesa Mahalu,
kauli iliyozidisha mkanganyiko.
“Si kweli kwamba kanuni hizi zinapitishwa kasoro
hivyo vifungu vya 37 na 38, bali vinapitishwa vyote isipokuwa kanuni
hizo zitaishia tu kusema uamuzi utafanywa kwa kura basi.
“Hiyo siri mnayoitaka siyo hoja hapa… hoja hapa ni
kupiga kura badala ya neno kura ya siri au ya wazi, tumesema utaratibu
utakuwa ni wa kupiga kura,” alisisitiza.
Alisema kamati yake imefikia hapo ili kuondoa dhana ya kwamba wanalipwa posho bure.
“Utaratibu wa kura gani itapigwa hauwezi
kutupotezea muda hapa na kweli tuna uchungu na fedha za Watanzania,
tunakula pesa bila kufanya kazi,” alisema Simbachawene.
Nje ya Bunge
Mwanasiasa mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru
alisema kinachofanyika ndani ya Bunge hilo sasa ‘ni uhuni’ ambao
umemfanya awe kimya wakati wote na kushindwa kuzungumza.
Sipendi uhuni huo, ndiyo maana wakati wote
nimekuwa kimya, lakini ukifika wakati wa kuijadili rasimu yenyewe
nitazungumza kwa masilahi ya wananchi,” alisema Kingunge.
Mjumbe Freeman Mbowe pamoja na kusema mvutano huo
unatokana na kugawanyika kwa wajumbe wa Kamati ya Maridhiano, alipinga
utaratibu uliopendekezwa kupitisha kanuni hizo nusunusu akisema ni mbovu
kwa sababu vifungu wanavyotaka kuacha ndiyo nguzo ya mchakato wote wa
Katiba.
“Huwezi kuweka sheria ya mchezo bila kuwa na sheria ya kufunga
goli. Hapa tulipofikia lazima tupitishe sheria ya kupiga kura ndipo
mambo mengine yafuate, kinyume chake hatufanyi kitu,” alisema Mbowe
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema.
Alisema ni afadhali taratibu nyingine zikasimama
ili kusubiri kupitishwa kwa utaratibu wa kupiga kura badala ya kuendelea
na mchakato huo ambao hatima yake iko shakani.
Alisema kura ya wazi ni hatari kwa kuwa itawagawa wananchi na wawakilishi wao bungeni.
Mjumbe mwingine, Yusuf Manyanga alisema: “Hapa
bungeni tunayumbishwa na vyama vya siasa vyenye wabunge. Vimekuwa
vikiweka masilahi ya vyama vyao mbele kuliko ya Watanzania.”
Mjumbe mwingine Joseph Selasini alisema
kilichoamuliwa na kamati hiyo siyo kulikabili tatizo, bali ni kuongeza
ukubwa wa tatizo... “Hata jioni wajumbe watapingana tu na kamati, maana
haiwezekani ukapitisha kanuni wakati vifungu havijakamilika.”
Selasini alisema tatizo ni CCM kujiona kuwa ina
mamlaka katika kila jambo na kusisitiza kuwa Tanzania siyo nchi ya chama
hicho pekee.
Mjumbe Henry Shekifu alisema katika uandaaji wa
kanuni, ikitokea kifungu kimoja kikaleta mvutano, lazima upitishaji wa
kanuni hizo uendelee ili kuokoa muda, kauli ambayo iliungwa mkono na
Mjumbe mwingine Martha Mlata.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment