Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
“Kwa hali ilivyo sasa bungeni, tusitegemee kupata Katiba au ikipatikana
inaweza kutokidhi matakwa ya wananchi kwa sababu tayari wanaoitengeneza
wamegawanywa. Tunamwomba Mungu aingilie kati.”
Kanisa la Makole Pentekoste Holyness la mjini hapa, linafanya
maombi maalumu ya kuliombea Bunge Maalumu la Katiba baada ya
kutoridhishwa na mwenendo wa Bunge hilo.
Maombi hayo yaliyoanza Jumatatu, yanatarajiwa
kumalizika Jumapili ijayo kwa waumini kugawanyika makundi, kila moja
linaomba kwa kufunga kwa siku moja kabla ya kujumuika pamoja kanisani,
Jumapili kuomba kwa pamoja.
“Kificho (aliyekuwa mwenyekiti wa muda wa Bunge
hilo) aliliongoza bila kanuni ingawa kulikuwa na mvutano haukuwa mkubwa
na alipochaguliwa Sitta kuwa mwenyekiti wa kudumu wananchi wengi
tulifurahi,” Mchungaji Kiongozi Asajile Mwandiga alisema na kuongeza.
“Kwa tulivyomfahamu uwezo wake wa kuongoza, kwa
mfano Bunge la Tanzania la 9, tuliamini tungepata Katiba bora lakini
imekuwa kinyume, anaegemea upande wa chama chake kwa uwazi kabisa.”
Mch. Mwandiga alisema hali hiyo iliwakatisha
tamaa, lakini kwa kuwa wanaamini katika Mungu, sasa wanaongoza Kanisa
kuomba msaada wake ili abadilishe mioyo ya wanaopindisha mambo.
Naye Mchungaji kiongozi msaidizi wa kanisa hilo,
Lucas Mwakalonge, alisema tofauti na Bunge kuamua mambo kwa mtindo wa
wengi wape, wao wanaoamini katika Mungu.
Mwakalonge alitaja sababu nyingine za maombi hayo
kuwa ni mivutano ya mara kwa mara bungeni kiasi cha vikao kuvunjika na
mgawanyiko wa Wabunge wa Bunge Maalumu.
Mchungaji huyo aliyekuwa Mkurugenzi Msaidizi wa
Idara ya Maktaba na Tafiti ya Bunge la Jamhuri ya Muungano hadi
alipostaafu mwaka 2011, alisema ili kufikia uamuzi wa kutoa Katiba bora
ni lazima kuwe na umoja miongoni mwa wanaoiunda na kuiandika.
“Kwa hali ilivyo sasa bungeni, tusitegemee kupata
Katiba au ikipatikana inaweza kutokidhi matakwa ya wananchi kwa sababu
tayari wanaoitengeneza wamegawanywa. Tunamuomba Mungu aingilie kati,”
alieleza.
Mbali na hayo, Mwakalonge alisema wanataka uwezo
wa Mungu uzuie mambo yasiyompendeza kuingizwa kwenye Katiba, akitoa
mfano wa sura ya 4 inayohusu Haki za Binadamu, kwamba kusiwe na utetezi
wa mashoga na wasagaji.
“Kuna mambo hakika hayapaswi kuingizwa kwenye
katiba yetu, tunamuomba Mungu apitishie mbali wale wote wanaotaka
kuifanya katiba hii kama mchezo wa kuigiza,” alisema
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment