Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Profesa Abdul Shariff (kulia) akipiga
kura ya siri wakati Bunge hilo jana lilipokuwa likipitisha utaratibu wa
kupiga kura za aina mbili (siri na wazi)
Wajumbe wa Kamati ya Maridhiano jana walinusuru Bunge Maalumu la
Katiba kuvunjika, baada ya kukubaliana kutumika kwa utaratibu wa
upigaji kura wa wazi na siri kama ilivyopendekezwa na Kamati ya Kanuni
na Haki za Bunge.
Wajumbe hao walitangaza uamuzi huo bungeni
kutokana na makubaliano yaliyofikiwa katika kamati ndogo ya maridhiano
iliyofanyika jana asubuhi baada ya kushindwa kuafikiana katika kikao cha
awali kilichofanyika juzi kuanzia saa 3:00 usiku hadi usiku wa manane
ili kunusuru kukwama kwa Bunge hilo.
Kabla ya uamuzi huo, Mwenyekiti wa Bunge hilo,
Samuel Sitta alisema juzi usiku walikutana hadi usiku wa manane baada ya
hapo, walikabidhi kamati ndogo yenye mchanganyiko wa wajumbe kutoka
Kamati ya Kanuni na Kamati ya Maridhiano.
“Baada ya kukamilisha kazi, wajumbe wa kamati
ndogo watatoa taarifa hapa ambao ni John Mnyika, Profesa Ibrahimu
Lipumba, Vual Ali Vual na Askofu Donald Mtetemela,”alisema Sitta.
Akitoa taarifa ya maridhiano hayo, kwa niaba
Freeman Mbowe, Mjumbe John Mnyika alisema, alianza kwa kunukuu kitabu
kilichoandikwa na Mwalimu Nyerere, mwaka 1962 chenye ujumbe mahususi kwa
Chama cha TANU akisema ujumbe huo kwa sasa ni sahihi kwa watu wengi na
taasisi ikiwamo CCM.
Mnyika pia alisema Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa) hawana nia yoyote ya kuvuruga mchakato wa katiba kama ambavyo
imeelezwa katika siku za karibuni na viongozi, kwani wazo la kutaka
Katiba Mpya imekuwa ni kilio chao cha muda mrefu.
Naye Profesa Lipumba alisema suala ambalo tumekuwa
tukisimamia kwa muda mrefu suala ambalo lina utata, kati ambao
wanapenda kura za uwazi na wale wa siri.
Alisema: “Tuliletewa mchanganyiko wa uwazi na
siri, lakini maana yake ni kura ya uwazi, wenzetu wamekuwa na msimamo
mkali hata hili la kufanya uamuzi ilikuwa tufanye kwa siri, lakini hata
hivyo hawakukubali.”
“Tulifanya uamuzi ili tusonge mbele, basi
tulipendekeza upigaji kura wa kuamua tupige kura kwa mfumo wa siri,
lakini pia wenzetu walikataa,”alisema Profesa Lipumba.
Alisema kwa kuzingatia kutokwama kwa zoezi la kuanza kujadili rasimu, wameamua kukubali kutokubaliana.
“Ili kusonga mbele tunahitaji kusonga mbele tuanze
kujadili Katiba, natoa wito kwa wenzangu wa chama tawala kwa kuwa mpo
wengi mnadhamana kubwa, ni vyema mkawa na utaratibu wa kuwasikiliza
wachache,” alisema.
Mjumbe Vuai Ali Vuai alisema, wamefikia maridhiano
hayo, ili kuwezesha kuendelea na mchakato wa katiba mpya kwani kila
upande uliendelea kutetea msimamo wake hata katika kikao cha maridhiano.
“Yapo mambo yalijitokeza kwenye kamati ambayo ni mengi,
tulidhani hapa tunakuja kueleza yale ambayo tunakubaliana kulikuwa na
hoja nyingi kuwa CCM hatutaki kuendeleza mchakato, lakini nilisema CCM
tutakuwa wa mwisho kusitisha mchakato wa Katiba,” alisema.
Alisema kwa mustakabali wa taifa waliamua kupitisha uamuzi wa kukubali kura za siri na wazi kwa pamoja.
Naye Askofu Mtelemela aliomba wajumbe kukubali
maridhiano ambayo, wamefikia ili kuweza kusonga mbele katika kuanza
kujadili mchakato wa Katiba.
Askofu Mtetemela alisema baada ya majadiliano,
wamekubaliana kurudi kwenye azimio la Kamati ili kuruhusu kuendelea na
kazi ya kujadili rasimu ya Katiba.
“Jambo zuri ambalo limejitokeza sote tuna nia
njema kwa ajili ya Bunge hili maalumu kuhakikisha mchakato wa kupatikana
Katiba Mpya haukwami,” alisema.
Alisema kwa siku 40 sasa wamekuwa wakijadili suala moja tu la kanuni, kazi ambayo inasubiriwa ya kujadili rasimu ya Katiba.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge
Baada ya taarifa hiyo ya Kamati ya Maridhiano,
Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na Haki za Bunge, Pandu Ameir Kificho,
pamoja na wajumbe wa kamati hiyo, Profesa Costa Mahalu na William Ole
Nasha, walitoa ufafanuzi wa kisheria kuhusiana na kanuni hizo.
Hata hivyo, kwa pamoja walieleza kuwa uamuzi wa
utekelezaji ya kanuni ya 37 na 38 yaliyokuwa ya yameachwa kama kiporo,
yakikamilika kutawezesha kuendelea na mchakato ya Katiba.
Baada ya kamati kuridhia makubaliano hayo, zoezi
la upigaji kura kuhusu uamuzi wa awali kama kura zipigwe kwa mfumo
uliopendekezwa wa kura za siri na wazi ulianza.
Matokeo ya kura
Akitangaza matokeo haya, Makamu Mwenyekiti wa
Bunge hilo, Samia Suluhu alisema idadi ya wajumbe waliokuwa katika
ukumbi ilikuwa 511, waliopiga kura walikuwa 509.
Alisema waliopiga kura ya wazi walikuwa 438 kati yao 351 walipiga kura ya ndiyo na 87 walipiga kura ya hapana.
Suluhu alisema waliopiga kura ya siri walikuwa
wajumbe 71, kati yao 25 walipiga kura ya ndiyo huku wajumbe 46 wakipiga
kura ya hapana.
Alisema jumla ya wajumbe waliopiga kura ya ndiyo
ni 376 na waliopiga kura ya hapana walikuwa wajumbe 133. Katika matokeo
hayo wajumbe wawili hawakupiga kura ingawa waliokuwamo bungeni.
Kutokana na matokeo hayo Bunge hilo sasa litatumia
utaratibu wa kupiga kura ya wazi na siri kwenye uamuzi wake katika
kupitisha vifungu vya rasimu.
Mjumbe awananga wenzake
Mjumbe wa Bunge la Katiba, Paul Gekul
amewashambulia wabunge wa Katiba wanaotoka kundi la CCM kuwa ni wanafiki
wanaojipendekeza kwa sauti, lakini matendo yao hayaendani nao.
Gekul alisema kitendo cha wabunge hao kulazimisha
kupiga kura za wazi ili wasikike na wapiga kura wao ni sawa na unafiki
kwa kuwa katika majimbo yao hakuna maendeleo.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, ni hivi juzi tulitoka
katika Jimbo la Uchaguzi la Kalenga (Iringa) kati ya kata 17 ni kata
tatu ndizo zenye umeme, leo hii wanaposema wanataka kura ya wazi siyo
haki,” alisema Gekul.
Alipinga kauli za wabunge kuwa wapinzani ndiyo
wanaotaka kupinga na kuvuruga mchakato wa Katiba kwa kusema wao ndiyo
waliokuwa wa kwanza kuomba Katiba Mpya hivyo hawatakuwa tayari kuvuruga
utaratibu huo.
Katika mchango wake mbunge huyo ambao ulionekana
kujikita zaidi kwenye vijembe badala ya hoja ya kura za siri au wazi,
alisema hakuna chochote ambacho viongozi wa CCM wamefanya kwa kipindi
cha miaka 50.
Chanzo;Mwananchi
Chanzo;Mwananchi
0 comments:
Post a Comment