Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Rais Jakaya Kikwete
Rais Jakaya Kikwete kesho ataambatana na ujumbe mzito wa marais
wastaafu wa pande zote za Muungano, wake wa waasisi wa taifa na mawaziri
wakuu wastaafu atakapokwenda kuzindua Bunge Maalumu la Katiba.
Hatua ya Rais kuambatana na ujumbe huo imepongezwa
na viongozi wa vyama vikuu vya upinzani nchini, Mwenyekiti wa CUF,
Profesa Ibrahim Lipumba na mwenzake wa Chadema, Freeman Mbowe.
Mbali na viongozi hao, Rais Kikwete pia
ataambatana na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein na Makamu wa Rais,
Dk Mohamed Gharib Bilal na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Seif
Sharif Hamad.
Wanaotarajiwa kuwamo katika msafara huo ni Rais wa
pili wa Tanzania, Ali Hassan Mwinyi, Rais wa tatu, Benjamin Mkapa na
marais wastaafu wa Zanzibar, Dk Salmin Amour na Amani Abeid Karume, Mama
Maria Nyerere na Mama Fatma Karume.
Miongoni mwa mawaziri wakuu wastaafu wanaotarajiwa
kuwamo ni pamoja na Jaji Joseph Warioba, ambaye juzi aliwasilisha
bungeni hapo Rasimu ya Katiba kwa kutoa hotuba iliyoliteka Bunge kwa
jinsi alivyofafanua mambo mengi yenye utata kuhusu muundo wa Muungano.
Mawaziri wakuu wengine ni Cleopa Msuya, John
Malecela, Dk Salim Ahmed Salim, Frederick Sumaye pamoja na Edward
Lowassa na Mizengo Pinda ambao ni wajumbe wa bunge hilo.
Wengine walioalikwa ni mabalozi wa nchi
mbalimbali, wawakilishi wa mashirika ya kimataifa, viongozi wa dini,
vyama vya wafanyakazi, vyama vya siasa, wafugaji, wakulima, wavuvi na
wawakilishi wa sekta binafsi.
Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Yahaya Khamis
Hamad aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa Rais Kikwete atahutubia
Bunge hilo kwa mujibu wa Kanuni ya 75 (1).
Rais Kikwete atapokewa katika Viwanja vya Bunge na
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta na baadaye kukagua
gwaride maalumu kabla ya kuhutubia Bunge kuanzia saa 10:00 jioni.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa jana, baada ya
Rais kuhutubia saa 11:35 jioni, aliyekuwa mwenyekiti wa muda wa bunge
hilo, Pandu Ameir Kificho atatoa neno la shukurani kabla ya Rais kupiga
picha za kumbukumbu na wajumbe wa Bunge hilo.
Suala la hotuba ya Rais Kikwete limekuwa sehemu ya
mjadala katika Bunge hilo kutokana na baadhi ya wajumbe kuhoji sababu
za Jaji Warioba kuwasilisha Rasimu kabla ya Rais kuzindua Bunge kwa
mujibu wa kanuni.
Mjadala huo uliwafanya baadhi ya wajumbe kumzuia
Jaji Warioba Jumatatu iliyopita kuwasilisha rasimu hiyo kama ilivyokuwa
imepangwa hadi kilipofanyika kikao cha maridhiano siku hiyohiyo usiku na
kufikia mwafaka kwamba Mwenyekiti huyo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
awasilishe Rasimu juzi na Rais ahutubie kesho.
Lipumba, Mbowe na Mtatiro
Akizungumzia ujumbe huo, Profesa Lipumba alisema hiyo inaonyesha jinsi mkuu huyo wa nchi alivyolipa uzito bunge hilo.
Profesa Lipumba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja
wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ulioundwa na baadhi ya wajumbe wa bunge
hilo alisema ni jambo jema kwa Rais kulizindua Bunge hilo kwa kuwa ndiye
mwasisi wa mchakato wa Katiba Mpya... “Ujio wake utasherehesha Bunge
hili na nasaha zake zitatusaidia.”
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzani bungeni alisema tendo la kuandika Katiba ni kubwa na linalohusu
wananchi wote hivyo ni dhahiri kuwa marais wastaafu na wake wa waasisi
wa Muungano wana fursa ya kipekee kuhudhuria uzinduzi huo.
“Nina hakika wapo viongozi wengine walioalikwa.
Kwa msingi huu, sina tatizo na ushiriki au ualikwa wao kwani bado wana
heshima katika jamii kama viongozi wastaafu,” alisema na kuongeza:
“Ni matumaini yangu kuwa hotuba ya Rais itasaidia
kupunguza hofu na hisia hasa kwa makundi yanayohasimiana katika Bunge
hili na siyo kuongeza hofu na ufa.”
Alisema wapo viongozi wa Bunge ambao wamekuwa
wakiwaona baadhi ya viongozi kama ni wafanya fujo... “Bunge la Katiba ni
tofauti na Bunge la kawaida na linahitaji kuvumiliana na kustahimiliana
sana wanachokitazama kama fujo kwa wengine ni staili muhimu ya kudai
kusikilizwa. Walichokiona kama fujo kimesaidia wabunge wote na hata
Watanzania kusikia kwa kina taarifa ya mheshimiwa Warioba. Fujo zile
ndizo zilizozaa saa nne alizopewa mheshimiwa Warioba na timu yake na
kuleta utulivu mkubwa katika nchi.”
Alisema kilichoonekana kama rabsha na fujo kwa
Rais wakati alipozindua Bunge la 10 ndicho kilichozaa mchakato huu wa
Katiba. Katika Bunge hilo, wapinzani walisusia hotuba ya Rais Kikwete
ambayo pamoja na mambo mengine, alitangaza kuanza kwa mchakato wa Katiba
Mpya.
Mjumbe wa Bunge hilo, Julius Mtatiro alisema
anatarajia Rais atasisitiza umuhimu wa maridhiano, maelewano,
kuheshimiana baina ya wajumbe na kuwataka watilie maanani masilahi ya
taifa badala ya kundi mojamoja au vyama.
Chanzo;mwananchi
Chanzo;mwananchi
0 comments:
Post a Comment