Home » » Kura bado kitendawili Bunge la Katiba

Kura bado kitendawili Bunge la Katiba

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Mchungaji Christopher Mtikila akimlalamikia Mwenyekiti wa muda wa Bunge hilo kwa kutompa nafasi ya kuchangia bungeni mjini Dodoma jana.

Kuonyesha kutokukubaliana na uamuzi huo, Mchungaji Mtikila alisimama bila kuruhusiwa na Mwenyekiti wa Muda wa Bunge hilo, Pandu Ameir Kificho na kuhoji sababu za kutopewa nafasi ya kuzungumza katika Bunge hilo.
“Kwa nini unanizuia kuzungumza, unataka nikuheshimu wakati heshima yangu unaivunja? Nataka kujua haki yangu, nataka unijibu, nataka kujua kwanini hutaki nizungumze hapa ndani,” alihoji.
Mtikila aliongeza kusema: “Unachagua watu wa kuzungumza unachofurahia wewe ndicho kina haki ya kuzungumzwa hapa ndani. Nataka kuzungumza ni haki yangu siyo kwa kupenda wewe ni haki yangu. Unawapa watu ambao mnakubaliana na kupitisha kanuni mbovu na wengine unatunyima kusema, siyo haki katika kutengeneza Katiba,” alisema.
Kwa upande wake, Felix Mkosamali aliwasha kipaza sauti na kusema hata yeye anashangaa hapewi nafasi ya kuzungumza anapoomba kufanya hivyo. Alimtuhumu Mwenyekiti kwa kuwapa fursa hiyo wajumbe ambao inaonekana walikubaliana naye kuunga mkono azimio.
Hata hivyo, Kificho aliwaomba radhi wajumbe ambao hawakupata nafasi ya kuzungumza, akisema orodha ilikuwa ndefu na kwamba isigewezekana kwa wote walioomba kupata fursa.
Wakati Mchungaji Mtikila na Mkosamali wakizungumza, baadhi ya wajumbe waliendeleza utamaduni wa kuzomea licha ya kwamba Kificho alishakemea hivi karibuni.
Akizungumza na waandishi wa habari nje ya Ukumbi wa Bunge, Mkosamali alisema siyo sahihi Bunge hilo kupitisha kanuni ambazo hazina kifungu kinachoeleza namna ya kufanya uamuzi.
Mkosamali alisema kifungu cha 22(1) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba kinamtaka mwenyekiti wa muda kusimamia uandaaji na upitishwaji wa kanuni zote za Bunge Maalumu na siyo nusunusu.
Mbatia: Ilikuwa lazima tukubaliane
Mjumbe mwingine wa Bunge la Katiba, James Mbatia alisema ilikuwa ni lazima wakubaliane na kupitisha Kanuni za Bunge hilo ambazo katika mjadala wake, ziliwagawa wajumbe katika makundi mawili yanayopingana.
Alipoulizwa sababu za kukubali kupita kwa kanuni hizo wakati hazijakamilika, alisema: “Kila jambo linaundwa kwa maridhiano na hata mwafaka wa Zanzibar ulipatikana baada ya pande mbili zilizokuwa zikivutana kukubaliana.
Kwa upande wake, Profesa Ibrahim Lipumba alielezea matumaini yake kuhusu kufikiwa mapema kwa maafikiano katika vifungu vya 37 na 38.
“Ninawapongeza Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni na wewe (Kificho) kwa kutuletea kanuni zinazokidhi haja,” alisema.
Habari hii imeandaliwa na Kizitto Noya, Fidelis Butahe, Habel Chidawali, Daniel Mjema na Sharon Sauwa.
Chanzo;Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa