Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ibara ya 26 kifungu kidogo cha
pili kwa sasa inatajwa kuwa kikwazo kikubwa kilichowekwa kwa kundi lenye
wafuasi wengi kuamua kila kitu bungeni.
Sheria hii inasema: Ili Katiba inayopendekezwa
iweze kupitishwa katika Bunge, itahitaji kuungwa mkono kwa wingi wa
theluthi mbili ya idadi ya wajumbe wote wa Bunge kutoka Tanzania Bara na
Tanzania Zanzibar.
Sheria hii inaungwa mkono na Kanuni za Bunge hilo,
ibara ya 64(1) ambayo inasema mambo yanayojadiliwa na kamati
yataamuliwa kwa kuungwa mkono na theluthi mbili ya wajumbe wote wa
Kamati kutoka Tanzania Bara na theluthi mbili ya wajumbe wote wa kamati
kutoka Tanzania Zanzibar.
Kanuni hiyo, inaendelea kufafanua kuwa, isipokuwa
uamuzi hata kama haukufikia theluthi mbili, suala hilo litapelekwa
kwenye Bunge Maalumu.
Kwa sasa sheria na kanuni hii, inaonekana ndiyo
itarejesha m mwafaka na maridhiano kwa kila kundi kama kweli kuna nia ya
dhati ya kupatikana Katiba Mpya.
Mjumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, Kajubi
Mkanjanga anasema sheria hii, kwa sasa ndiyo ambayo inazuia kutungwa
katiba ya chama kimoja au kikundi cha watu wachache.
Anasema Msingi wa Sheria hii ni kuweka utaratibu
utakaowezesha kujenga mwafaka wa kitaifa katika masuala yenye masilahi
kwa taifa.
“Sheria hii inarejesha mazungumzo ya pande
zinazokinzana, inarejeha kuondoa dharau baina ya makundi na kulazimisha
maridhiano katika kupata Katiba Mpya” anasema Mkajanga
Sheria ilivyowakaanga wajumbe
Ukali wa sheria hii, ulianza kubainika katika
zoezi la kura katika kamati zilipokuwa zinapitisha ibara mbali mbali.
Katika sura ya kwanza na sura ya sita. Katika zoezi hilo, kamati 10 kati
ya 12 za Bunge Maalumu la Katiba, zilishindwa kupata theluthi mbili
katika kufanya mabadiliko ya ibara katika sura hizo ya kwanza na sita
hasa zile ambazo zilikuwa zinafumua Rasimu ya Katiba. Wajumbe wa
Zanzibar ndiyo ambao kwa kiasi kikubwa, walikwamisha upatikanaji
theluthi mbili.
Sura ya kwanza ya Rasimu, ilikuwa inazungumzia
Jina, Mipaka, Alama, Lugha na Tunu za Taifa na Sura ya Sita,
inazungumzia Muundo wa Jamhuri ya Muungano
Kamati mbili ambazo zimeweza kupata theluthi mbili
katika kufikia uamuzi ya kutengua baadhi ya vifungu hasa juu ya Muundo
wa Muungano ni kamati zilizokuwa zinaongozwa na Hamad Rashid na Kamati
ya Kidawa Hamis na kamati ya Dk Fransis Michael.
Ngeleja atamba kupata theluthi mbili
William Ngeleja ni Makamu Mwenyekiti wa kamati
namba tisa, anasema kupata theluthi mbili, katika kufikia uamuzi ya
Serikali mbili kunawezeka.
Mjumbe huyo, anasema kama kwenye kamati yake
wameweza kupata theluthi mbili za Zanzibar na Bara, haoni ni kwa nini
ikosekane bungeni.
“Kama sisi katika sura ya kwanza na sita, tumepata
theluthi mbili, ina maana inawezekana kabisa bungeni kuzipata na hivyo
kuendelea na mfumo wa serikali mbili ambao unaungwa mkono na Watanzania
wengi” anasema Ngeleja. Bunge la Jamhuri lina wajumbe 628, wajumbe
kutoka Zanzibar ni 212 sawa na asilimia 33.8% na wajumbe kutoka bara ni
416 sawa na asiliami 66.2% ya wabunge wote.
Mwenyekiti wa kamati namba tano, Hamad Rashid, pia
alieleza kamati yake, kuweza kupata theluthi mbili za Bara na Zanzibar
katika kufikia uamuzi.
Anasema kwa maana hiyo, kamati yake itabadili
vifungu kwenye rasimu ambayo vinaeleza muundo wa Serikali tatu katika
sura ya kwanza na ya sita.
Ibara zilizopata ugumu kupata theluthi mbili
Katika sura ya kwanza ibara ya kwanza kifungu cha
kwanza. kilichokosa theluthi mbili kinasomeka kuwa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania ni nchi na Shirikisho lenye mamlaka kamili ambalo linatokana
na Muungano wa nchi mbili Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa
Zanzibar. Akizungumza na gazeti hili, Mwenyekiti wa kamati namba sita,
Stephen Wasira anasema katika kamati yake, ibara hiyo, imeshindwa kupata
theluthi mbili, ili kuweza kufanyiwa marekebisho. “Kwa upande wa bara
tulipata theluthi mbili lakini Zanzibar imekosekana na tumeacha kama
ilivyo kwani matokeo haya ya kamati siyo mwisho”anasema Wasira.
Alisema hata katika sura ya 6 ibara ya 60(1)
ambayo inasema Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itakuwa ni ya muundo wa
Shirikisho lenye Serikali tatu, ambazo ni serikali ya Jamhuri ya
Muungano, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na Serikali ya Tanganyika
theluthi mbili ya Zanzibar ili kutengua kifungu hicho imeshindwa
kupatikana.
“Lakini huu siyo mwisho kama nilivyosema awali.
Tukirudi bungeni tutapiga kura kwa wajumbe wote na ndiyo itakuwa na
uamuzi wa mwisho kama Muundo wa Muungano utakuwa na serikali tatu ama
mbili ambao utapelekwa kwa wananchi” anasema Wasira
Vifungu hivi pia kwa mujibu wa wenyeviti wa kamati
nyingine, isipokuwa kamati moja tu ya Tano, ambayo inaongozwa na Hamad
Rashid, havikupata kura theluthi mbili na hivyo kubaki kama vilivyo
kwenye rasimu. ,
Ukawa: Sheria ya theluthi mbili imewaokoa
Wanasheria wawili, kutoka wajumbe wa kundi la Katiba ya
Wananchi, Tundu Lissu na Ismail Jusa, wanasema sheria hiyo, sasa ndiyo
mwamuzi wa wa mwisho. Ndiyo, ambayo inaonesha siyo rahisi CCM kuliburuza
Bunge hilo kama ambavyo walitegemea.
Jussa anasema sura ya kwanza na ya sita ndiyo
kiini ya rasimu hivyo, kama vikikosa theluthi mbili ya kutenguliwa kwa
kiasi kikubwa rasimu itabaki kama ilivyo.
“Tumeanza na sura ambazo ni uti wa mgongo wa
Katiba kwa sababu huwezi kuandika katiba kama hujajua mfumo wa nchi
unakwendaje,”anasema.
Alisema kwa taarifa alizo nazo katika kamati zote,
CCM wamekuwa na mapendekezo yao kwa kila ibara ambayo wanataka
yaingizwe katika Rasimu ya Katiba lakini sasa wanakwama.
Alisema pasipokuwa na Katiba iliyopendekezwa na wananchi kutaleta mpasuko mkubwa ndani ya nchi.
Jussa alisema kwa sasa ili kuhakikisha kuwa na
msimamo mmoja, wajumbe wa upinzani na makundi yanayounga mkono Muundo wa
Serikali tatu, kutoka Zanzibar watakuwa wakipiga kura ya wazi.
Lissu akizungumzia matokeo ya awali, anasema kwa
sasa CCM ndiyo inaweza kuanza mkakati wa kuvuruga Bunge kwani tayari
wamejua hawana theluthi mbili ya Zanzibar ili kubadili rasimu kama
wanavyotaka.
Je, Sheria hii inaweza kuzuia Bunge kupitisha serikali mbili katika vikao vinavyoendelea? Tusubiri.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment