Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Bunge Maalumu la Katiba leo linaanza wiki ngumu pale
litakapohitimisha mjadala wa muundo wa Muungano na kupiga kura kupitisha
au kukataa.
Hiyo inatokana na ukweli kwamba muundo huo wa muungano ndiyo unaotabiriwa kubeba ajenda zote katika mjadala huo wa Katiba.
Kwa mara ya kwanza wiki hii Watanzania
watashuhudia hatua ya upigaji kura ambayo awali iliibua mvutano mkubwa
wakati wa kupitishwa kanuni ili kuamua mfumo gani utumike kati ya kura
ya siri na wazi.
Katika hili, mjumbe atakuwa na uhuru wa kupiga
kura ya wazi au ya siri wakati wa kupitisha sura namba moja na namba
sita. Ili zipite, ni lazima zipate theluthi mbili ya kura kwa kila
upande wa Muungano.
Hata hivyo, leo Bunge hilo litaanza kwa kumpa
nafasi Mjumbe wa Bunge hilo, Tundu Lissu kuendelea kutoa ufafanuzi wa
hoja za walio wachache kwenye Kamati Namba Nne.
Ufafanuzi huo wa Lissu uliahirishwa juzi baada ya
matangazo ya moja kwa moja ya Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC)
kukatika ghafla.
Baada ya Lissu kumaliza, kamati zilizobaki ambazo
ni Namba Sita inayoongozwa na Steven Wassira, Kamati Namba Saba
inayoongozwa na Brigedia Jenerali mstaafu Hassan Ngwilizi zitawasilisha
taarifa zao.
Inatarajiwa kuwa katika kipindi cha mchana, Kamati
Namba 10 inayoongozwa na Anna Abdallah itawasilisha taarifa yake na
kufuatiwa na ufafanuzi wa wajumbe walio wachache wa kamati hizo.
Kulingana na hali ya mambo ilivyo, kuna uwezekano
mkubwa kwamba wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba, wataanza kuchangia
taarifa za kamati zote 12 katika kipindi cha jioni au kesho asubuhi.
Kwa mujibu wa Kanuni ya 33 (7), baada ya taarifa ya kamati hizo kuwasilishwa, zitajadiliwa katika kipindi kisichozidi siku tatu.
Kama mambo yatakwenda kama ilivyo, inatarajiwa
kuwa upigaji wa kura kupitisha sura hizo mbili huenda ukafanyika Ijumaa
na hivyo kutegua kitendawili cha muda mrefu kuhusu aina ya muundo wa
Muungano katika Katiba Mpya.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment