Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mjumbe wa Bunge la Katiba, John Mnyika amesema
hajaondoa hoja yake ya kutaka kuwekwa wazi mkataba halisi wa Muungano wa
Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar.
Akizungumza na gazeti hili, Mnyika alisema hoja
hiyo haijafa licha ya mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta kusema
imepelekwa katika kamati na sasa ni zaidi ya wiki mbili haijatolewa
maelezo.
Mnyika, ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Ubungo kwa tiketi ya Chadema, alisema anakusudia kuirudisha hoja hiyo bungeni.
“Natarajia tukianza majadiliano katika sura hizi
mbili, sura ya kwanza na ya sita, niombe tena hati halisi kwani ndio
msingi wa majadiliano hasa kuhusiana na mambo ya Muungano,” alisema .
Alisema kuirejesha hoja hiyo itakuwa ni
utekelezaji wa kanuni za Bunge la Katiba, kwani bado haijapatiwa majibu
lakini ni hoja yenye msingi mkubwa hasa katika majadiliano ya Bunge
hilo.
Mnyika aliwasilisha hoja ya kuomba kupatiwa hati
halisi ya Muungano wakati bunge hilo lilipoanza, lakini hata hivyo, hadi
sasa haijapatiwa ufumbuzi. Hadi sasa wajumbe wa Bunge hilo wamepewa
nyaraka zenye maudhui ya hati hiyo.
“Ni ukweli tumepewa Sheria ya Tangayika kuridhia
Muungano Sheria Namba 22 ya mwaka 1964, lakini sheria hii ina maudhui tu
ya Muungano siyo hati ambayo mimi naihitaji,” alisema Mnyika.
Tangu kuanza vikao vya kamati za Bunge hilo, hoja ya kutakiwa Hati ya Muungano ilijitokeza katika kamati zote 12.
Jambo hilo liliulazimisha uongozi wa Bunge
kumwita Dodoma aliyekuwa katibu wa Bunge la Tanganyika, Pius Msekwa
kutoa ufafanuzi kuhusu hati na sheria ya kuridhia Muungano.
Hata hivyo, ufafanuzi wa Msekwa unaonyesha haukuwakuna wajumbe wengi wa Bunge hilo.
chanzo:mwananchi
chanzo:mwananchi
0 comments:
Post a Comment