Home » » SITTA IKIBIDI TUTAITA WATAALAMU

SITTA IKIBIDI TUTAITA WATAALAMU

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MWENYEKITI wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta amesema Sheria ya Mabadiliko ya Katiba inaruhusu kuitwa mtu yeyote katika Bunge hilo kutoa ufafanuzi kuhusu jambo lolote lenye utata, ikionekana ipo haja kufanya hivyo. Kauli hiyo ya Sitta ameitoa huku siku chache zilizopita, baadhi ya wajumbe wa kamati kuonesha uhitaji wa kutaka ufafanuzi wa kitaalamu wa maneno kadhaa ikiwemo nchi, muungano, serikali, dola, shirikisho katika siku ya kwanza ya kujadili sura ya kwanza na ya sita ya Rasimu ya Katiba mjini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Dar es Salaam mara baada ya kufanya mkutano na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Sitta alisema sura namba 83 ya sheria hiyo inatoa ruhusa hiyo.
“Ni halali kwa mujibu wa sheria kupata ufafanuzi wa jambo lolote, sikuwa Dodoma kwa siku mbili hivi, sijajua ofisini nini kimewasilishwa, lakini tukipokea ombi hilo, tutafanya jitihada na sitasita hata kidogo kumuita Warioba (Jaji Joseph-Mwenyekiti wa iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba)……. …au mtaalamu mwingine aje kutusaidia,” alisema Sitta akijibu swali kuhusu utata wa maneno hayo uliowakumba wabunge na kama amepokea ombi la kutaka wataalamu wa lugha waende kuwasaidia kuyafafanua.
Wakati Sitta anasema hayo, gazeti hili lilitafuta matumizi ya maneno hayo kwa Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) na kupata ufafanuzi na uchambuzi wa maneno hayo.
Katika kufafanua wao, Bakita limeeleza tofauti ya neno muungano na shirikisho kwa kubainisha kuwa shirikisho ni umoja wa nchi kadhaa zilizoweka mkataba wa kuwa chini ya serikali moja au kiongozi mmoja wakati muungano ni mshikamano wa pamoja wa pande mbili au zaidi.
Uchambuzi wa Bakita unafafanua zaidi kuwa, katika muktadha wa kawaida huku wakitolea mfano Tanzania, muungano ni mshikamano wa nchi mbili, zenye serikali mbili tofauti lakini mambo mengi wamekubaliana kama serikali moja.
“Katika baadhi ya mambo walioungana wanakubaliana kuyatekeleza kwa pamoja kama kitu kimoja lakini si vyote. Ikiwa watakubaliana kutekeleza kwa pamoja kila kitu, basi huo si muungano tena bali ni nchi moja kamili,” alifafanua Mtaalamu wa Kiswahili wa Bakita, Mussa Kaoneka.
Kuhusu neno nchi, Bakita ilieleza kuwa ni sehemu ya ardhi yenye mipaka ya kisiasa na kijiografia na kufafanua kwamba, kisiasa kunakuwa na utawala mmoja ikifafanua kwa kutoa mfano kama ilivyo Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinavyotawala Zanzibar na Bara.
Uchambuzi kuhusu dola unaeleza kuwa, ni utawala unaotaja na kuhusisha vyombo vitatu vikuu vya uamuzi, ambavyo ni Bunge, Mahakama na Serikali Kuu na kueleza kuwa serikali ni sehemu ya dola na ndicho chombo chenye mamlaka ya kutawala nchi.
Akifafanua zaidi kuhusu serikali, Kaoneka kwa niaba ya Bakita alisema katika serikali, kunakuwa na Amiri Jeshi Mkuu wa Serikali, nae ndio msemaji wa mwisho na wa juu kabisa wa kutoa kauli iwe katika mazingira ya hatari ama salama.
“Mfano ikitokea hali ya hatari, mwenye kauli ya mwisho kusema nini kifanyike na kuwataka Watanzania wachukue hatua gani, ni Amiri Jeshi Mkuu, huyu ndie mwenye dhamana ya kila kitu,” alifafanua Kaoneka.
Kuhusu taifa, Bakita inaeleza kuwa ni umoja wa watu wenye historia, utamaduni, siasa na uchumi unaofanana chini ya utawala unaofanana.
Kwa mujibu wa Bakita, muungano uliopo ni wa serikali mbili kwa maana ya serikali ya Muungano na ile ya Zanzibar, na kueleza kuwa kutokana na kutokana na amana halisi ya nchi, haikuwa sasa kwa Zanzibar kuweka neno nchi katika mabadiliko ya 10 ya Katiba yake hata kama ilikuwa na maana ya dola kamili.
“Kitaalamu, sisi na Zanzibar hatuna mipaka ya kisiasa, kwa mfano, CCM ndicho chama kinachoongoza serikali, hiki kinatawala hadi Zanzibar, Mwenyekiti wa Taifa wa chama hicho ni Rais wa Muungano, ukitaja Tanzania, unaingiza Zanzibar ndani yake, huu ni ufafanuzi wa kitaalamu tu hauhusiki na siasa yoyote,” alisema Kaoneka akifafanua kwa mifano halisi.
Katika siku ya kwanza ya kujadili rasimu, kamati tatu zilizotoa taarifa zilieleza mjadala ulianza kwa amani lakini ukiibua utata wa mkanganyiko kwa wajumbe katika Sura ya Kwanza ya Rasimu ya Katiba katika baadhi ya matumizi ya maneno nchi, dola, serikali, shirikisho, taifa na muungano.
Miongoni mwa kamati wajumbe walichanganywa na maneno hayo hadi kutaka wataalamu wa Kiswahili waitwe kuyafafanua ni pamoja na kamati ya Kwanza inayoongozwa na Ummy Mwalimu, ya Tano iliyo chini ya Uenyekiti wa Hamad Rashid Mohamed na ya 11 ile inayoongozwa na Anne Kilango Malecela.
Wajumbe katika kamati hizo walitaka kufahamu kitaalamu matumizi ya maneno hayo na mipaka ya matumizi yake kabla ya kuendelea na mjadala. Kilango alisema katika kamati yake alilazimika kutoa taarifa kwa Mwenyekiti wa Bunge, Samuel Sitta wapate mtaalamu aje awape ufafanuzi wa matumizi ya maneno hayo.
 Chanzo:Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa