Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Katibu wa Bunge Maalumu la Katiba, Yahaya Khamis Hamad amesema
wajumbe ambao ni wanachama wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
hawajachukua posho wasiyostahili.
Wajumbe hao wamekuwa wakituhumiwa katika mitandao
ya kijamii na majadiliano bungeni kuwa wameondoka na posho za Bunge hilo
ambazo wamelipwa hadi Aprili 30 mwaka huu.
Wajumbe wa Ukawa waliondoka bungeni Aprili 17
mwaka huu baada ya kulalamikia vitendo vya ubaguzi, matusi na wajumbe
kutojadili Rasimu ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya Mabadiliko ya
Katiba iliyokuwa ikiongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Hamad alisema wajumbe hao walilipwa posho za hadi
Aprili 18 mwaka huu. “Tulikuwa tulipe posho za hadi Aprili, lakini baada
ya baadhi kuondoka tulibadili utaratibu,” alisema Hamad.
Alisema wanafanya tathmini kujua ni nani wapo ili
kuwalipa. “Hata kama mbunge ameondoka akirudi atatuambia, tumlipe fedha
yake, lakini sasa tunalipa waliopo bungeni,” alisema na kuongeza:
“Hatuna list (orodha) maalumu ya Ukawa na hakuna
mtu aliyetuambia kuwa ameondoka kwa sababu ya Ukawa kwa hiyo
watakavyorudi watatuambia.”
Kauli ya Katibu huyo imekuja wakati Mwenyekiti wa
Bunge hilo, Samuel Sitta, akitangaza kwamba wajumbe wa kundi la Ukawa
hawawezi kulipwa posho kutokana na kususia vikao vya Bunge hilo.
Sitta alitangaza msimamo huo bungeni juzi, akisema hakuna sababu za kuwalipa watu ambao hawajafanya kazi ya Bunge.
Sitta alisema haitakuwa na maana ya wajumbe kulipwa posho, wakati hawajafanya kazi ambayo iliwapeleka Dodoma.
Awali, Naibu Waziri wa Fedha, Adam Malima alitoa
taarifa kwamba wamekuwa wakishauriana na Ofisi ya Katibu wa Bunge
Maalumu ili kusitisha malipo ya Ukawa.
Malima alisema malipo hufanyika kwa wale
wanaokwenda bungeni kwa ajili ya kufanya kazi za Bunge hilo na siyo watu
ambao wako nje ya Bunge.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment