Home » » MBATIA ,SERUKAMBA WAUNGANA KUMBANA WAZIRI KAWAMBWA

MBATIA ,SERUKAMBA WAUNGANA KUMBANA WAZIRI KAWAMBWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Mbunge wa Kuteuliwa James Mbatia
 
Elimu ya Tanzania imeelezwa kwamba iko Chumba cha Wagonjwa Wenye Uangalizi Maalum (ICU) na kwamba hata wenye dhamana ya kuisimamia hawafanyi vizuri.
Wabunge pia waliishauri serikali kuunda tume maalumu itakayosimamia mfumo mzima wa elimu nchini.

Akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kwa mwaka 2014/15 iliyosomwa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, Jumamosi iliyopita Mbunge wa Kuteuliwa James Mbatia, alisema elimu nchini ni dhaifu na haina tija kwa kizazi cha Tanzania.

Alisema uchumi wa Tanzania unazidi kuporomoka kutokana na elimu kutopewa kipaumbele.

“Tuwekeze kwenye elimu. Suala hili si la chama, namuomba Rais aunde tume ya kudumu ya elimu nchini,” alisema Mbatia wakati akichangia jana.

 Mbatia alishauri kuwa tume hiyo ikiundwa itakuwa inaangalia ubora wa elimu na kufanya utafiti wa kisayansi kuhusu elimu.

Mambo mengine ambayo alishauri kushughulikiwa na tume hiyo ni kuainisha lugha itakayotumika kufundishia.

“Elimu isiwe bidhaa za kuuzwa sokoni na iendelee kubakia kama huduma,” alisema.

Alilazimika kusema hayo baada ya baadhi ya wabunge kusema kuwa ni ghali kutokana na shule binafsi kutoza ada kubwa.

Mbatia pia alisema hakuna umakini katika utungaji wa mitihani na kutoa mfano kwa mtihani wa majaribio wa darasa la saba wa mwaka 2013 wa masomo ya Hisabati, Kiingereza na Kiswahili uliofanywa katika shule 40 nchini kukosewa.

Alisema mtihani kama wa Hisabati hata maprofesa hawawezi kuufanya na kupata majibu, hivyo, alitangaza zawadi ya Sh. milioni 10 kwa wabunge ambao ni maprofesa watakaoufanya na kutoa majibu.

SERUKAMBA
Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Serukamba, naye alisema elimu ya Tanzania iko mahututi na iko  ICU.

“Tuache siasa katika elimu. Tumekuwa wabinafsi kwa sababu elimu hii haituhusu sisi na watoto wetu. Watoto wetu sisi humu ndani tunasomesha Ulaya, South Afrika (Afrika Kusini). Walalahoi wanaumia,” alisema Serukamba na kupendekeza kuundwa kwa tume ya kuchunguza elimu.

Alisema kwamba alisema elimu ya chuo kikuu haina thamani tena. “Hebu tuwalete wahitimu wa vyuo vikuu waje halafu tuwaambie waandike barua ya Kiingereza, hakuna atakayeweza. Hivi hii elimu tunaipeleka wapi?” alihoji.

RWEIKIZA

Mbunge wa Bukoba Vijijini (CCM), Jackson Rweikiza, alisema elimu ya Tanzania lazima iwe ghali kutokana na serikali kuzibana shule binafsi kwa utitiri wa kodi.

Rweikiza ambaye ni mmoja wa wamiliki wa shule za msingi na sekondari nchini, alisema wanalazimika kutoza ada kubwa kutokana na kutokuwa na ruzuku, lakini bado kuna kodi nyingi.

“Hizi shule zinatozwa kodi nyingi sana, serikali haiziungi mkono na badala yake inazitoza kodi na michango mingi,” alisema.

Kwa mujibu wa Rweikiza michango na kodi hizo haziwaumizi wamiliki wa shule tu bali mzigo mkubwa unakuwa kwa wazazi.

Alisema pia kuwa wizara inachangia kuporomoka kwa elimu nchini kwani shule bila ukaguzi haziwezi kuwa na maendeleo yoyote.

Mbunge huyo alisema wizara inalazimika kuwa na mkakati wa ukaguzi wa mara kwa mara.

MKANGA

Akizungumza kwa uchungu, Margareth Mkanga anayewakilisha walemavu bungeni, alionyesha kusikitishwa na hotuba ya Waziri Kawambwa kwamba haikumzungumzia mtoto mlemavu.

“Hivi hawa watoto walemavu ni wa nani. Watoto wangu nawapa pole sana maana hata mwenye dhamana ya kuwasimamia hakuwazungumzia kwenye hotuba yake. Natamani kulia kabisa,” alisema.

Alisema walimu wanaofundisha walemavu wanafanya kazi katika mazingira magumu, hivyo wanastahili kulipwa posho ya mazingira hayo.Alihoji ni vipi serikali inashindwa kuwasomesha bure watoto wenye ulemavu.

Baadhi ya wabunge walihoji ni kwa nini Waziri Dk. Kawambwa anaendelea kubebwa wakati hakufanya mabadiliko yoyote ya elimu ikiwa ni pamoja na kuongeza kiwango cha wanafunzi wanaofeli.

KAMBI YA UPINZANI

Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeiponda Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuwa imekuwa ikididimiza elimu na kumtaka Waziri  Kawambwa kujipima kama anaona anatosha kuendelea kuwapo wizarani hapo.

Kambi hiyo imesema kuwa wizara hiyo imeshindwa kupandisha kiwango cha ufaulu katika ngazi ya msingi na sekondari na kuiacha kuendelea kushuka kila mwaka.

Akiwasilisha hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo, msemaji wa kambi hiyo, Susan Lyimo, alisema kiwango cha ufaulu kimekuwa kikishuka na  Wizara hiyo imeamua kukipandisha kwa ajili ya kufuta aibu ambayo imeikumba serikali tangu awamu ya nne ingie madarakani.

Alisema kuwa mwaka 2007 miaka miwili tu baada ya serikali ya awamu ya nne kushika madaraka ufaulu wa kidato cha nne ulikuwa asilimia 90.3 mwaka 2008 ufaulu ulishuka hadi asilimia 83.6 na mwaka 2009  ufaulu uliendelea kushuka hadi kufikia asilimia 72.5 huku mwaka 2010 uliporomoka tena kufikia asilimia 50.4

“Watanzania wanapaswa kuelewa kuwa mchezo unaofanywa na Serikali ya CCM wa kuchezea madaraja na alama za kufaulu utaligharimu sana taifa hili huko tuendako,” alisema Lyimo.

Alisema kuwa kitendo cha Wizara hiyo ya kupandisha madaraja na alama za ufaulu utaligharimu sana taifa kwa kutoa wahitimu ambao wanafaa hapa nchini tu na wasio na sifa katika wigo wa kimataifa.

Alisema kuwa pamoja na wabunge na wadau mbalimbali wa elimu kupigia kelele kuhusiana na upangaji mpya na alama za madaraja, lakini Wizara hiyo imendelea kutekeleza mpango huo ambao unaligharimu taifa.

Alitolea mfano matokeo ya mwaka 2013 ya kidato cha nne kuwa yamepangwa kwa kutumia alama mpya za ufaulu na kusababishwa mfumo wa elimu nchini kuporomoka na kutoa wahitimu ambao hawana ubora.

Alisema kuwa Wizara hiyo imekuwa ikitumia mfumo wa elimu ambao umepitwa na wakati kutokana na watoto wanaoanza shule ya msingi wanachelewa kuanza na kukaa shuleni kwa muda mfupi.

Lyimo alisema kiwango cha wastani duniani cha muda wa kusoma ni miaka tisa, lakini hapa nchini watoto wamekuwa wakisoma katika kipindi cha miaka saba na matokeo yake wamekuwa wakimaliza wakiwa bado na wadogo na bila kuwa na maarifa na stadi za kuwafanya wajitegemee.

Alisema kuwa licha kambi ya upinzani kutoa mapendekezo ya mara kwa mara ili kuboresha mfumo huo, lakini yamekuwa yakipuuzwa na Serikali na matokeo yake elimu hiyo imekuwa ikishuka kila siku.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa