Home » » WABUNGE SABA WATIKISA BUNGE

WABUNGE SABA WATIKISA BUNGE

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 Wabunge saba wamelitikisa Bunge tangu mkutano wa Bunge la Bajeti ulipoanza kutokana na michango yao binafsi.
Mwandishi wetu ambaye amekuwa bungeni tangu Mkutano wa Bajeti ulipoanza ametoa tathmini yake kuhusu michango ya wabunge iliyosisimua katika mjadala na kuibuka na orodha ya wabunge hao saba. Hata hivyo, katika tathmini hiyo, majina ya wabunge ambao walichangia kwa niaba ya kamati au kutokana na nafasi zao za uwaziri au uwaziri kivuli hajayaingizwa katika orodha hiyo.
Tathmini hiyo imefanyika huku leo mjadala wa Bajeti ya Serikali ya 2014/15 ukihitimishwa tayari kwa kupigiwa kura na wabunge kesho, baada ya kukamilisha mfululizo wa mijadala ya bajeti za wizara zote za Serikali tangu Bunge hilo lilipoanza Mei 6, mwaka huu. Hoja zilizoibuliwa na wabunge hao kwa nyakati tofauti ziliitikisa Serikali na kusababisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kiti cha Spika au aliyekuwa akikaimu nafasi ya Waziri Mkuu bungeni, Profesa Mark Mwandosya ambaye ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Kazi Maalumu) kusimama kutoa ufafanuzi.
Waliotikisa
Wabunge waliotikisa Serikali katika michango yao ni Ally Keissy (Nkasi Kaskazini - CCM), David Kafulila (Kigoma Kusini - NCCR-Mageuzi), Kangi Lugola (Mwibara - CCM), Dk Faustine Ndugulile (Kigamboni - CCM), Tundu Lissu (Singida Mashariki - Chadema), Abbas Mtemvu (Temeke –CCM) na Cecilia Paresso (Mbunge wa Viti Maalumu-Chadema) .
Kafulila
Siku mbili baada ya Bunge kuanza Mei 8 mwaka huu, wakati wa Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Kafulila aliibuka na sakata la kuchotwa kwa Dola za Marekani 122 milioni (Sh200 bilioni) akidai ni ufisadi uliofanywa na vigogo sita wa Serikali.
Aliwataja kwa majina vigogo hao na kusisitiza kuwa wamehusika na ufisadi wa fedha hizo zilizokuwa zimewekwa katika akaunti ya Baraza la Usuluhishi la Migogoro ya Kibiashara (Escrow), katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT). Akaunti hiyo ilifunguliwa kutokana na mgogoro wa kibiashara kati ya IPTL na Tanesco na Tanesco ilipeleka shauri hilo mahakamani kulalamikia gharama kubwa za uwekezaji wanazotozwa na IPTL, hivyo kuamuliwa fedha hizo ziwekwe humo hadi shauri litakapoamuliwa, lakini baadaye zilichotwa katika mazingira ya kutatanisha.
Lugola
Lugola aliibuka Mei 10, mwaka huu katika mjadala wa Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika na kusema kuwa Serikali ya CCM ambayo yeye ni mbunge wake, inaendeshwa kisanii huku akishangaa waziri mwenye dhamana ya kilimo, Christopher Chizza kuendelea kuwa waziri wakati hotuba yake imejaa blaablaa.
Pia alimgeukia Naibu Waziri, Godfrey Zambi na kumwambia amejisahau kwamba naye alikuwa akikaa kiti cha nyuma bungeni akipaza sauti, baada ya kupata madaraka amewageuka wenzake na kushirikiana na waziri.
Akizungumza kwa sauti ya ukali ambayo mara nyingi haitarajiwi kwa wabunge wa CCM, Lugola alihoji inakuwaje wakulima wanapelekewa pembejeo feki, dawa feki na skimu za umwagiliaji zinachakachuliwa na bado Chizza anaendelea kubaki kama waziri?
Keissy
Mei 27, mwaka huu ilikuwa zamu ya Keissy, mbunge machachari wa Nkasi Kaskazini pale alipozua sokomoko wakati akichangia hotuba ya Wizara ya Mambo ya Nje. Kauli yake kuwa Zanzibar haichangii katika Muungano hivyo haina haki ya kuhoji mambo ya upande wa pili wa Muungano na kwamba hata umeme hailipi nusura imponze.
Alisema Zanzibar ina asilimia 2.8 ya watu wote wa Tanzania na kwamba kwa idadi hiyo, wananchi wa jimbo moja wanaweza kukusanyika eneo moja kwa kuitwa na mlio wa filimbi tu, kauli iliyosababisha wabunge kutoka Zanzibar kutaka kumpiga ‘kavukavu’.
Abass Mtemvu
Juni 5, Mtemvu naye aliibua mpya baada ya kumlipua Mbunge wa Urambo Magharibi (CCM), Profesa Juma Kapuya kuwa anafahamu uuzaji wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) ambalo alidai limeuzwa kwa Sh280 milioni.
Mtemvu alisema kulifanyika ujanjaujanja kati ya Kampuni ya Simon Group na Meya wa Jiji Dar es Salaam, Didas Masaburi kukopa benki na taasisi nyingine kwa ajili ya kununua shirika hilo, kauli ambayo ilipingwa na Kapuya huku suala la Uda likiendelea kukamata mjadala hadi Mwendeshaji wa Uda kuitwa bungeni.
Faustin Ndungulile
Mei 29 mwaka huu, Dk Ndugulile alimweka katika wakati mgumu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka wakati wa mjadala wa bajeti ya wizara hiyo na kuwa Serikali haijashirikisha wadau katika mradi wa Kigamboni utakaogharimu Sh11.7 trilioni.
Sakata hilo liliingiliwa na Waziri Mkuu ambaye alisema kuwa tatizo la mradi huo ni elimu kutotolewa kwa umma na kuomba wabunge waiachie Serikali suala hilo.
Tundu Lissu
Juni 2, Lissu aliwalipua Waziri wa Maji, Profesa Jumanne Maghembe na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira), Dk Binilith Mahenge kwamba wanatumia vibaya nafasi zao kwa kuweka fedha nyingi za miradi ya maji katika maeneo wanakotoka, huku sehemu zenye matatizo ya huduma hiyo zikitengewa fedha kiduchu.
Lissu alisema Profesa Maghembe ambaye ni Mbunge wa Mwanga, Kilimanjaro, wizara yake imetenga Sh1.4 bilioni kwa ajili ya miradi ya maji, ambazo ni zaidi ya mara saba ya Sh190 milioni zilizotengwa kwa ajili hiyo katika Wilaya ya Ikungi, Singida. 
Mawaziri hao waliokolewa na Profesa Mwandosya akisema kuwa miradi hiyo katika wilaya za Same, Mwanga na Korogwe ilianza wakati yeye akiwa Waziri wa Maji, hivyo hawakujipendelea.
Cecilia Paresso
Mbunge huyu aliichachafya Serikali na kuungwa mkono na wabunge 13 wanawake wakati akichangia Bajeti ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii wakitaka iongezewe fedha ili kukabiliana na vifo vya kinamama na watoto.
Paresso alisema wizara hiyo imetengewa Sh622 bilioni, ikiwa ni pungufu ya Sh131 bilioni ya bajeti ya wizara hiyo mwaka 2013/14 ilipotengewa Sh753 bilioni.
Hoja hiyo iliwanyanyua Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, Waziri wa Afya, Dk Seif Rashid na Naibu Mawaziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba na Adam Malima kutoa ufafanuzi. Wote hao walishindwa kumshawishi Paresso na wenzake, hadi Serikali ilipoahidi kuongeza fedha za wizara hiyo, ikiwa ni pamoja na kutoa Sh87 bilioni kwa ajili ya kulipa deni la Bohari Kuu ya Dawa (MSD).
Chanzo:Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa