Home » » MASWALI MAGUMU KWA WAZIRI MKUYA HAYA HAPA

MASWALI MAGUMU KWA WAZIRI MKUYA HAYA HAPA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Waziri wa Fedha,Saada Mkuya Salum
 
Baada ya siku saba za mjadala mkali wa wabunge kuhusu Bajeti ya Serikali mwaka 2014/15, kesho Waziri wa  Fedha Saada Mkuya Salum, atakabiliwa na kibarua kizito kujibu hoja za kasoro mbalimbali zilizoibuliwa na wabunge.
Ratiba iliyotolewa na Ofisi ya Bunge, mwishoni mwa wiki, inaonyesha mjadala wa bajeti hiyo utahitimishwa kesho.

Spika Anne Makinda tayari amewataka wabunge wote kuhudhuria bungeni kupitisha vifungu hadi kifungu vya bajeti hiyo na baadaye bajeti nzima wakati bunge litakapokaa kama kamati, kesho jioni.

Katika bajeti hiyo iliwasilishwa bungeni Juni 12, mwaka huu, na Waziri Mkuya wabunge waliikosoa wakiielezea kuwa haiwezi kutekelezeka kwa kuwa inategemea zaidi fedha za wahisani, ambao kwa uzoefu wa miaka iliyopita, utekelezaji wa ahadi zao umekuwa ukisuasua.

Bajeti ya kuu ya mwaka huu ni Sh. trilioni 19.8 ambazo kati ya hizo kuna mikopo na misaada ya kibajeti Sh. bilioni 922,168, mikopo na misaada ya miradi ya maendeleo Sh. trilioni 2.0, mikopo ya ndani Sh. trilioni 2.9 na mikopo yenye masharti ya kibiashara Sh. trilioni 1.3.Mapato ya ndani ni Sh. Trilioni 12.1.

Wabunge pia walikosoa uamuzi wa serikali wa kupunguza kodi ya mapato kwa wafanyakazi (PAYE) kutoka asilimia 13 hadi 12 tu, wakisema kuwa haitawasaidia wafanyakazi kwa kuwa ni kidogo mno. Wanapendekeza ipunguzwe kufikia digitali moja.

Pia mawaziri hao watatakiwa kutoa maelezo namna ambavyo serikali imejipanga kudhibiti matumizi yake ambayo yamelalamikiwa kuwa ni makubwa mno.

Aidha wabunge waliopata nafasi ya kuchangia waliitaka serikali kuchukua hatua dhidi ya matumizi mabovu kama vile safari na misafara mikubwa ya viongozi ambao haina tija kwa taifa na kulipa mishahara kwa watumishi hewa.

Waziri Mkuya pia atatakiwa kueleza sababu za kuongezeka kwa bajeti kwa ajili ya safari za nje za Rais kutoka Sh. bilioni 15 nadi 50, ambayo ni kubwa kulinganisha na fedha zinazopelekwa katika miradi ya maendeleo ya baadhi ya wizara.

Baadhi ya wabunge walilalamikia bajeti ya safari za Rais kwamba inalingana na na fedha zinazopelekwa katika miradi ya Wizara ya Kilimo na inazidi bajeti ya miradi ya maendeleo ya Wizara ya Afya ambazo ni Sh. bilioni 46.

Kuongezeka kwa deni la Taifa kufikia Sh. trilioni 30.5 kuliibua mjadala mkali kutoka na wabunge wengi kuhoji sababu zinazochangia pamoja na kutoa angalizo kwamba hali hiyo isipodhibitiwa kuna hatari kwa serikali kufilisika.

Pia, wabunge wengi walizungumzia suala la ajira, wakiilalamikia serikali kwamba imeshindwa kutengeneza ajira mpya za ajira kwa vijana huku vyuo vya elimu ya juu vikizalisha wahitimu 40,000 mwaka.

Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani, Freeman Mbowe, alisema kuwa kuna haja ya kuliweka suala la ajira kama ajenda katika Serikali Kuu, Bunge na Halmashauri.

Aidha, Wabunge wengi pamoja na makundi mengine ya jamii waliilaumu serikali kwa kukosa ubunifu wa kuibua vyanzo vipya vya mapato na badala yake kuendelea kutoza kodi katika soda, bia, mvinyo, vinywaji vikali, sigara baada ya mwaka 2014/15 kozitoza bidhaa hizo kodi ya asilimia 10.

Waziri Mkuya atalazimika vilevile kueleza mikakati ya serikali ya kuhakikisha inakabiliana na naksi katika bajeti ya Sh. trilioni tatu. Wabunge wengi waliochangia walionyesha wasiwasi wao kama bajeti ya 2014/15 itaweza kutekelezeka kutokana na naksi hiyo.

Uamuzi wa serikali kushusha umri wa magari chakavu kutoka miaka 10 hadi minane ambayo itakuwa ikikatwa kodi ya asilimia 25 ulilalamikiwa na wabunge kadhaa wakisema magari chakavu yanahitajika kwa wananchi wengi ili kuwaletea maendeleo katika shughuli zao, kwamba ni Watanzania wachache wenye uwezo wa kununua magari mapya.

Waziri Mkuya na manaibu wake, Adamu Malima na Mwigulu Mchemba, watalazimika kujibu  hoja hizo kwa majibu ambayo yatawaridhisha wabunge.

Haata hivyo, kutokana hoja nzito ziilizotolewa na wabunge na Kamati ya Bajeti, upo uwezekano mkubwa kwa serikali kufanya marekebisho katika baadhi ya mapendekezo iliyoyawasilisha.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa