Home » » KAMATI KUU CCM:BUNGE HALITASITISHWA

KAMATI KUU CCM:BUNGE HALITASITISHWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye
 
Matumaini ya kufikiwa maridhiano kwanza kabla ya Bunge Maalum la Katiba kuendelea, yamefutika baada ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kubariki bunge hilo kuendelea na vikao vyake vya ngwe ya pili hadi Oktoba 31, mwaka huu.
Chama hicho tawala kimeshikilia msimamo wake huku  makundi mbalimbali ya jamii yakipaza sauti kutaka bunge hilo liahirishwe ili kupata mwafaka kwanza baina ya makundi yanayohasimiana ili Katiba itakayopatikana itokane na ridhaa ya wananchi wote.

Makundi yanayoendelea kuvutana ni CCM na wajumbe wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umaoundwa na Chadema, CUF na NCCR-Mageuzi.

Uamuzi wa CCM ya kubariki Bunge Maalum la Katiba kuendelea yalitangazwa jana mjini Dodoma na Katibu wa Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, baada ya kumalizika kwa kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika juzi chini ya Uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete.

“Kuhusu mwenendo wa Bunge Maalum la Katiba, Chama Cha Mapinduzi kinautakia kila la kheri mchakato unaoendelea na kwa ujumla, Kamati Kuu imeridhishwa na namna wajumbe wanavyoshughulikia tofauti za kimtazamo na kimawazo katika vikao vyao na hatimaye uhitimishaji wa majadiliano kwa kura,”  Nape aliwaambia waandishi wa habari.

Alisema kufuatia maamuzi hayo, Kamati Kuu Maalum imemwagiza Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kukutana na Ukawa pamoja na wadau wengine ili kufanikisha maridhiano ya pande mbili zinazohasimiana ambazo zimeweka rehani matumaini ya kupatikana Katiba yenye maridhiano.

“Kamati Kuu Maalum inaunga mkono juhudi za TCD za kuendeleza mashauriano kati ya vyama na ndani ya vyama kwa minajili ya kupunguza mivutano, kujenga uaminifu, ustahimilivu na umoja kati yao,” alisema.

Alisema kikao hicho kilipokea taarifa na kufanya tathmini juu ya maendeleo ya mchakato wa katiba nchini, ndani na nje ya Bunge Maalum.

Aidha, alisema kamati hiyo ilijadili taarifa ya mazungumzo na mashauriano kati ya vyama vya CUF, Chadema, NCCR-Mageuzi na CCM yaliyofanywa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, pamoja na kujadili taarifa ya kikao cha Baraza la Vyama vya Siasa na ile ya Kituo cha Demokrasia Tanzania (TCD).

YASIKITISHWA NA UKAWA
Nape alisema Kamati Kuu Maalum imesikitishwa na kuvunjika kwa mazungumzo kati ya CCM, CUF, Chadema na NCCR-Mageuzi yaliyokuwa chini ya Jaji Mutungi kwa sababu alikuwa na lengo la kujenga na kuimarisha maridhiano na mshikamano ili kupata mwafaka.

UTORO WA WAJUMBE
Kuhusu utoro wa wajumbe zaidi ya 80 wa Bunge Maalum la Katiba ambao unawahusisha Mawaziri na baadhi ya wabunge wanaotokana na CCM, Nape alisema kamati hiyo inawahimiza kurudi kuendelea na vikao hivyo kwa kutanguliza maslahi mapana ya taifa ili kuipatia nchi katiba inayotarajiwa na Watanzania wote.

“Rais Kikwete amefanya maamuzi magumu kwa kuchukua hatua kwenye ziara yake ya kikazi inayoanza leo (jana) mkoani Morogoro.Amewaondoa baadhi ya mawaziri kwenye msafara wake na kuwataka warejee Dodoma kuendelea na vikao vya kamati pamoja na wajumbe wengine,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa