Home » » 'MANENO MANENO' YAMKERA WAZIRI

'MANENO MANENO' YAMKERA WAZIRI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

WAZIRI wa Maji Profesa Jumanne Maghembe amekerwa na kauli ya kuwa Bahi hawautaki mradi wa maji wa bwawa la Farkwa na kutaka maoni ya watu wachache yasiwe sababu za kukwamisha mradi huo.
Profesa Maghembe alitoa kauli hiyo hivi karibuni wakati wa kikao cha wadau cha kukusanya maoni kwa ajili ya tathmini ya athari kwa mazingira na jamii ya mradi wa bwawa la Farkwa na mfumo wake wa kupeleka maji Manispaa ya Dodoma.
Hatua hiyo ilifuatiwa na kauli ya Mtaalamu Mshauri wa Kampuni ya Tres Consult, Bashiru Hassan inayotekeleza mradi wa usanifu wa mradi wa ujenzi wa bwawa la Farwa kusema kuwa Bahi hawautaki mradi huo hata kama kuna hatua za kudhibiti na kupunguza madhara. Kutokana na kauli hiyo Waziri Maghembe aliingilia kati na kuhoji uhalali wa kauli hiyo.
“Lazima unapoongea upime maneno yako, ongea kwa takwimu sio mtu moja hataki usiongee kwa ujumla,” alisema.
Alisema wakati wa kutoa taarifa kama hiyo lazima taarifa ziwe sahihi.
“Lazima takwimu ziwe sahihi unaweza kusema kati ya watu tulioongea nao asilimia fulani wanakubali na wengine hawakubali na wengine hawana maoni’ alisema. Waziri Maghembe alisema mradi huo ni mkubwa na utanufaisha wakazi wa Wilaza nne za Mkoa wa Dodoma ikiwemo Dodoma Manispaa, Chamwino, Bahi na Chemba.
‘’Hakuna chanzo kingine kikubwa cha maji kikubwa kama cha Farkwa, lazima Dodoma waukumbatie mradi huu ni mradi wa Maji ya Mji Mkuu wa Tanzania “ alisema.
Alisema wote ambao hawautaki mradi huo hawautakii mema Mkoa wa Dodoma. “Ukiona wanachochea watu ujue kuna kitu wanachokitafuta,” alisema.
Akisoma taarifa ya maoni ya jumla ya mradi, mtaalamu mshauri huyo alisema kwa ujumla wadau walio wengi wanauona mradi kuo kuwa ni mzuri na utaweza kumaliza tatizo la maji Manispaa ya Dodoma ambapo bomba litapita.
Pia mradi unaweza kukuza shughuli mpya za kiuchumi na kijamii na kuimarisha maendeleo katika eneo hilo na angalizo kubwa ni juu ya ulipaji wa fidia kwa muda.
Kwa upande wake Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia alisema mradi huo ukikamilika utakuwa mkombozi mkubwa. Hata hivyo alibainisha kuwa, kuna watu wanatumiwa ili kuharibu mradi huo.
“Bahi hawana maji lakini baadhi ya watu wanapiga vita mradi huo kutokana na sababu zao binafsi, lakini wananchi walio wengi wanaunga mkono mradi huu kwani wanajua faida yake itakuwa nini,” alisema Nkamia.
Pia aliomba kwenye bajeti ya mwakani fedha zitengwe ili mradi huo uanze. Hata hivyo Diwani wa Kata ya Bahi Ramadhani Mtawa alisema wananchi hawajashirikishwa vya kutosha juu ya mradi wa ujenzi wa bwawa la Farkwa. Alisema katika skimu sita za umwagiliaji katika wilaya hiyo wananchi hawakushirikishwa.
“Hili ni jambo jema lakini kuna skimu sita za umwagiliaji ambazo viongozi na wakulima hawajashirikishwa vya kutosha,” alisema.
Alisema uhai wa maisha ya wananchi wa Bahi unategemea kilimo cha umwagiliaji lakini kuna umuhimu wa watu wa Bahi kupatiwa elimu juu ya faida za bwawa la Farkwa ambalo pia litasambaza maji kwa matumizi ya wananchi wa Bahi.
Pia Mwenyekiti wa Halmashauri ya Bahi, Hussein Kamau alisema mradi huo ukikamilika utanufaisha wananchi kwa kiasi kikubwa kwani maji yatakuwa yakienda kwa utaratibu na utanufaisha zaidi kwenye kilimo cha umwagiliaji.
Chanzo;Habari Leo

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa