Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Uhusiano na
Uratibu), Steven Wasira amesema hana sababu ya kuona haya kutangaza
kuutaka urais kwa kuwa urais si ukwe ila anasubiri wakati mwafaka.
Wasira alitoa kauli hiyo hivi karibuni alipokuwa akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili mjini Dodoma.
“Watakaposema ruksa, nitasema na wala kugombea
urais si suala la kuonea haya. Ni kutoa huduma kwa Watanzania. Unalionea
haya la nini? Kwani kugombea urais ni ukwe?” alihoji Wasira na
kuendelea;
“Urais ni mama mkwe wako, hapana. Wakati ukifika
nitasema tu. Na mradi kuna wananchi wanasemasema na wananitia moyo,
ukifika wakati nitasema.”
Hata hivyo, waziri huyo ameonya kuwa endapo urais
utachezewa kwa kuingia mtu ambaye si mwadilifu, biashara atakayoifanya
Ikulu itakuwa ni kuuza haki za watu.
Alisema hawezi kufahamu nani atashinda katika
kinyang’anyiro cha urais katika uchaguzi mkuu wa mwakani, lakini lazima
rais awe mtu mwenye sifa za kushika nafasi hiyo.
“Mimi siwezi kufahamu ni nani ataongoza Tanzania,
lakini ninaweza kusema sifa.” Alisema Wassira na kutaja sifa hizo kuwa
ni pamoja na kuwa Mtanzania kwa sababu haiwezekani kuagiza mtu kutoka
nje ya nchi kuja kuwania nafasi hiyo.
Aliongeza; “Rais pia anatakiwa kuwa mzalendo
anayeipenda nchi yake na adhihirishe mapenzi yake, awe na uwezo wa
kuongoza na pia ame-prove (amedhihirisha) uwezo wake huo wa kuongoza.”
Sifa nyingine ya urais, aliitaja kuwa ni mgombea
kuwa mtu aliyewahi kuongoza taasisi nyingine na kuwaridhisha Watanzania
kuwa aliongoza vizuri.
“Lakini pia rais lazima awe mwadilifu maana
unalinda haki za watu. Baba wa Taifa aliwahi kusema Ikulu kuna biashara
gani, lakini kuna biashara ya nguvu tu. Unaweza kuuza haki za hao watu,”
alisema na kuongeza;
“Maana chakuuza pale hakuna. Mimi nafanya pale.
Mimi naona watu wanamwagilia maua tu lakini kuna power (nguvu), kama
wewe unapenda hela zaidi kuliko watu waliokuweka pale basi wewe utakuwa
kazi yako ni kuuza haki zao.”
Alisema sifa hizo ni za msingi na wala si ngumu na kama mtu hana, hana tu.
Alipoulizwa katika sifa hizo anazozielewa yeye anajipimaje,
alijibu, “Mimi siwezi kujipima. Nitajipimaje? Mimi nitapimwa na watu
wengine”.
“Lakini kama wananitaja habari ya urais,
wananisema na mimi nawashukuru wanaonisema. Kumbe na mimi ninaweza
kupimwa na Watanzania,” alisema.
Waziri huyo ambaye pia ni mbunge wa Bunda alisema
kwa sababu Watanzania wanasema na yeye ni miongoni mwa watu wenye nia ya
kuwania urais, labda wanapima kwa sifa hizo.
Alisema chama chake kina utaratibu wa kufuata endapo mwanachama anataka kuwania nafasi ya uongozi.
Umri wa urais
Wasira mwenye umri wa miaka 69, alisema ujana au uzee siyo sifa za uongozi.
“Sifa zipo, akiwa anazo kijana anaongoza, akiwa
nazo mzee anaongoza. Huwezi kusema ujana ni sifa. Mbona ni wengi.
Tungekuwa hatuna tatizo la kupata rais maana wako wengi, asilimia 60 ni
vijana, sasa tungepata shida gani kama ni ujana tu,” alisema.
Alisema uzee ni idadi ya miaka tu na wala si sifa
ya uongozi kwa sababu hata hao wanaojiita vijana leo, kesho watakuwa
wazee na wanaweza kuwa wazee bila ya kuwa na sifa za uongozi.
Rushwa katika uchaguzi
Wassira alisema rushwa ndani ya siasa ina madhara
makubwa kwa sababu watapatikana watu waliochaguliwa ambao kimsingi
hawana cha kuwafanyia wananchi zaidi ya kurudisha mali zao.
“Lakini unawachagua ili waende kupambana na
rushwa, halafu wanachaguliwa kwa rushwa, sasa hii ni problem (ni
tatizo), rushwa si kitu kizuri sana cha kujivunia,” alisema Wasira na
kuongeza;
“Lakini unaisemaje rushwa, siipendi. Na
ninachoweza kusema mimi sipendi hayo mambo. Mimi ningependa mtu
anayechaguliwa achaguliwe na Watanzania hawa kwa imani.”
Alisema angependa Watanzania wachague rais na viongozi wengine
kwa imani baada ya kuwapima sifa zao za uongozi na siyo kwa rushwa.
“Unaweza kuchaguliwa ubunge kwa rushwa lakini uchague mpaka rais kwa rushwa Mungu wangu mbona nchi itakuwa imekufa!”
Chanzo:Mwananhi
Chanzo:Mwananhi
0 comments:
Post a Comment