Home » » BUNGENI KWACHAFUKA

BUNGENI KWACHAFUKA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkurugenzi wa Kamati ya Ufundi ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), John Mnyika, akifafanua jambo kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.Kulia ni Mjumbe wa Kamati hiyo, Joran Bashange. 


Licha ya Bunge Maalum la Katiba (BMK) kuunda Kamati ya Mashauriano ili kusaka theluthi mbili ya kura za upande wa Zanzibar, Bunge hilo jana lilichafuka baada ya Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Othman Masoud Othuman, baada ya kupiga kura ya wazi akikataa sura na ibara kadhaa za Rasimu inayopendekezwa.

Hali hiyo ilisababisha vurugu na hasira kutoka kwa baadhi ya wajumbe wa bunge hilo, na kupelekea mwanasheria huyo atolewe nje ya Bunge chini ya ulinzi mkali wa Polisi ili kumnusuru na kipigo.

Wajumbe wengi, hususan kutoka Zanzibar, walisikika wakimzomea na kuimba nyimbo za kumkataa, huku wengine kumweleza kuwa ni kamanda ambaye alikuwa ametoroka lakini wakashangaa kumwona yupo.

Licha ya Mwenyekiti wa BMK, Samuel Sitta kuwatuliza wajumbe kwamba kura ni uamuzi (dhamira) binafsi ya mjumbe na kwamba amefanya hivyo kwa mujibu wa demokrasia, wajumbe hao walisikika wakisema amekuja hapo si kama mtu binafsi isipokuwa kama mwenasheria mkuu.

“Hatumtaki, aliletwa atusaidie kila pahali, lakini huyu ni kamanda aliyetoroka vita sisi tunamwona hatufai tena,” walisikika wakisema wajumbe wa Zanzibar.

Sakata la tukio hilo lilianza bila kutarajiwa baadaye ya Othman ambaye alijitoa kwenye Kamati ya Uandishi wa Rasimu hiyo Septemba 5, mwaka huu, na kutoonekana bungeni hadi alipoibuka jana siku ya tatu ya wajumbe kuipigia kura Rasimu Inayopendekezwa, aliporuhusiwa kupiga kura.

Othman alipiga kura yake baada ya wajumbe watano Abdulkarim Shah, Januari Makamba, Steven Ngonyani, Dk. Seif Suleiman Rashid na Mariam Kasembe ambao hawakuwa wamepiga kura zao siku zilizotangulia.

Wajumbe hao walipiga kura za ndio kuanzia sura ya kwanza hadi ya 10, na ibara zake zote kuanzia namba moja hadi 157.Baada ya Sitta kusoma matangazo mbalimbali na kujibu taarifa au kutoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali za wajumbe, ndipo Othman aliapotinga ndani ya bunge hilo.

Baadaye alilieleza bunge kwamba Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, (AG), Othman Masoud Othman, naye yupo ndani na kwa kuwa hakuwa amepiga kura yake, basi anaruhusiwa kupiga kura kwa wakati huo.

Aliposimama kupiga kura, AG huyo alisema; “Nitapiga kura ya wazi.” (wajumbe wakapiga makofi).Aliendelea huku wabunge wakiwa kimya kwa shauku: “Napiga kura ya hapana katika  Ibara namba 2, 9, 86 na Sura ya saba ibara ya 70 hadi 75, pia ibara ya 128 na 129 na sura ya 11, ibara ya 158, 159, 160 na 161, pia sura ya sita ibara ya 243 hadi 251 na katika nyongeza ya kwanza chini ya ibara ya 70,  ibara zilizobaki napiga kura ya ndiyo.”

(Katika ibara alizopigia kura ya hapana, Ibara namba 2 inazungumzia eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakati Ibara namba 9, inazungumzia Ukuu na Utii wa Katiba, na Ibara ya 86 inazungumzia Utaratibu wa Uchaguzi wa Rais).

Aidha Sura ya Saba inahusu Muundo wa Jamhuri ya Muungano na Ibara za 128 inahusu Madaraka ya kutunga Sheria na Ibara ya 129 inahusu Utaratibu wa kubadilisha Katiba).

Pia Sura ya 11 inahusu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Baraza la Mapinduzi la Zanzibar na Baraza la Wawakilishi la Zanzibar na ibara zake za 158, 159, 160 na 161.

Sura ya 16 ambayo pia aliipigia kura ya hapana, inahusu Masharti ya Fedha za Jamhuri ya Muungano, na ibara zake 243 hadi 251 na nyongeza ya kwanza ya Ibara namba 70 inayozumzuia, Muundo wa Muungano.

Baada ya kumaliza kupiga kura hiyo, Sheikh Kasim Yahya, alioomba taarifa kwa Mwenyekiti kuhusu kuhusu mwanasheria huyo.Katika taarifa yake alisema mwanasheria huyo kwa muda wote huo hakuwapo pamoja nao katika vikao vya bunge linaloendelea.

“Tulimtegemea awemo kutoa ushauri wake lakini hakufanya hivyo, yeye alitoweka na amekuja sasa…hivi mwanasheria kama huyu ana maslahi kweli na Zanzibar,” alihoji huku akipigiwa makofi ya kibunge na wajumbe wenzake wengi wao kutoka Zanzibar hali ambayo ilionyesha kuchafuka kwa hali ya hewa.

Mwenyekiti wa BMK alilazimika kutoa ufafanuzi wa taarifa hivyo kuwa: “Kura hatupigi kwa vyeo, kila mtu ana dhamira yake.”

Hata hivyo, wajumbe hao walisikika wakisema Othman hakuja bungeni humo kama mtu binafsi isipokuwa amekuja kwa cheo chake kama Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar.

Baada ya kuahirishwa bunge hilo, AG Othman alionekana kusalimiana na wajumbe mbalimbali ndani ya ukumbi wa bunge huku wajumbe wakiwa wanatoka nje.

Hata hivyo, Othman alipotaka kutoka nje kwa kutumia mlango wa kawaida unaotumiwa na wajumbe wenzake, kundi la askari wa bunge hilo walimfuata na kumwelekeza kutumia mlango unatumiwa na viongozi akiwemo Spika na Waziri Mkuu.

Askari hao wakiwa wameongozana naye alipumzika kwa muda katika chumba maalum ndani ya bunge hilo na baada ya muda mrefu kupita walitoka naye nje na akapanda gari la Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Mwanasheria huyo hakupewa nafasi ya kuzungumza na vyombo vya habari na muda wote alikuwa amezungukwa na askari.

BUNGE LAKANUSHA KUKAMATWA
Katika hatua nyingine, BMK limetoa taarifa kukanusha taarifa zinazosambazwa na baadhi ya watu katika mitandao ya kijamii ya kuwa Othman Masoud Othman amekamatwa baada ya kupiga kura ya hapana Bungeni jana. 

“Tunapenda kuutarifu umma wa Watanzania kuwa, taarifa hizo sio sahihi na ni porojo zenye kutaka kuleta hisia potofu kwa wananchi kuhusu kiongozi huyo,” ilieleza taarifa ya Idara ya Habari.

WAJUMBE KUTOONDOKA DODOMA
Mwenyekiti wa BMK, aliwaomba wajumbe kutoondoka Dodoma kwa wakati huu hadi hapo watakaposomewa matokeo kwa maelezo kwamba baadhi ya kura zimekataa rasimu.
“Ni lazima tuyapokee matokeo, tukishayapokea matokeo ya kura za kila ibara, inawezekana baadhi ya ibara zimekataliwa au hata inawezekana kwa upande huu au ule, theluthi mbili haikufikiwa, sasa kuna hatua za kikanuni za kuchukua.

 “Sasa ukidhani kwamba baada ya kupiga kura unaweza kuondoka tu, basi itakuwa kweli kazi kubwa,” alisema.

Aliwaeleza wajumbe hao kuwa pamoja na kupokea matokeo ya kura, bunge hilo linahitaji sasa kupitisha hoja ya Kamati ya Uandishi kwa pamoja na kupitisha Katiba inayopendekezwa kwa pamoja ikiwa na akidi.

Alisema iwapo watashindwa kufikia theluthi mbili kwenye ibara ambazo zimekataliwa, basi kanuni zinawaruhusu kufikisha suala hilo kwenye Kamati ya Mashauriano na kisha kurejea tena kwenye kura ili kufikia mwafaka.

Alisema kutokana na sababu hizo kubwa muhimu anawataka wajumbe hao kuendelea kubaki mjini hapa.

UKAWA WADAIWA KUPIGA KURA
Katika hatua nyingine;  Mwenyekiti  huyo aliliambia Bunge kuwa wajumbe wawili ambao hakuwataja majina kutoka Umoja wa Katiba ya Wananchi wamepiga kura.
Alidai kuwa mjumbe mmoja kati ya hao ameamua kupiga kura yake na kwamba haogopi kufukuzwa uanachama.
“Mmoja wao yupo tayari kufukuzwa katika chama chake, amepiga kura.

“Maji yanafuata mkondo, jambo ambalo Mungu ameamua haliwezi kuzuiwa na mtu litafanyika tu…huyu mjumbe baada ya kuisoma rasimu iliyopo na kuona manufaa yake ameamua kuipigia kura,” alidai.

Kwa upande mwingine, alidai kuwapo kwa mjumbe mmoja ambaye kazi yake kubwa ilikuwa ni kuwashawishi wajumbe hususan kutoka Zanzibar, waipigie rasimu hiyo kura ya hapana.

Alidai jina la mjumbe huyo limemtoka kidogo, alisema juzi alimshikilia kwa muda mjumbe mmoja aliyemtaja kwa jina moja tu la Mwanaidi ili asiweze kupiga kura yake.
“Mjumbe mmoja alikuwa ameshikilia huyo (Mwanaidi) kama mfungwa wake, alikuwa anahakikisha sana kupunguza kura za Zanzibar,” alidai.

AMSHAMBULIA MNYIKA
Vilevile Sitta amelitumia bunge hilo kumshambulia Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, John  Mnyika, kuwa hajakomaa kisiasa na anatumia kauli za ovyo ovyo.


Alisema kuwa Mnyika akihutubia kwenye mkutano mkoani Mwanza hivi karibuni, alimshambulia yeye (Mwenyekiti) na Andrew Chenge kuwa ni maharamia.

“Mimi na Chenge tumeitwa maharamia, sasa wanadhani siasa ni siasa za chuo chuo…mimi namsamehe kwa sababu bado ni mtoto mdogo, mimi ni kama baba yake,” alisema.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa