Home » » WAPINZANI:RATIBA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA HAIELEWEKI

WAPINZANI:RATIBA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA HAIELEWEKI

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mkuu wa Organaizesheni wa NCCR-Mageuzi, Faustine Sungura

Uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Desemba 14, mwaka huu, unaonekana kuviumiza vichwa baadhi ya vyama vya upinzani nchini kwa madai kwamba, ratiba kamili haieleweki.

Akizungumza na NIPASHE, Mkuu wa Organaizesheni wa NCCR-Mageuzi, Faustine Sungura, alisema hadi sasa wanaendelea kufuatilia iwapo uchaguzi huo unaweza kufanyika mwaka huu kama ilivyotangazwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, au la.

Hata hivyo, alisema bado hawajaelewa ratiba kamili ya kufanyika kwa uchaguzi huo kutokana na kuwapo kwa taarifa mbili tofauti, ikiwamo aliyodai kutolewa na Rais mwanzoni mwa mwezi uliopita kwenye kikao cha pamoja kilichofanyika mjini Dodoma na ile ya Waziri Mkuu, Desemba 14 mwaka huu.

“Rais katika kikao cha pamoja mjini Dodoma tulipokuwa tunamwomba kuahirisha Bunge Maalumu la Katiba, alisema uchaguzi huo unaweza kufanyika kati ya Februari au Machi, mwakani,” alisema.

Kutokana na hilo, alisema bado maandalizi ya kutosha kuhusu uchaguzi huo hayajafanyika ikiwa ni pamoja na kanuni, taratibu na tangazo kwenye gazeti la serikali.

Mkurugenzi wa Organaizesheni, Mafunzo na Usimamizi wa Kanda wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Benson Kigaila , alisema wanaendelea kujipanga, lakini bado hawajapewa taarifa zozote kuhusu masuala mbalimbali, yakiwamo ya kanuni.

Alisema utaratibu wa kuandikisha wapigakura ulipaswa kutangazwa, lakini hadi sasa haujatekelezwa na kwamba, mbali na baadhi ya mambo kuonekana kutokamilika, wanaendelea na maandalizi.

Kuhusu orodha ya wagombea, alisema kwa sasa wanaendelea na mkakati wa kuwaandaa wagombea na baadaye wataweka bayana orodha hiyo.
Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Joran Bashange, alisema walishajiandaa kushiriki mbali na taarifa za ratiba ya kufanyika kwa uchaguzi huo kuwa tofauti.

Alisema katika kikao cha TCD, Rais alisema uchaguzi huo utasogezwa hadi mwakani, lakini hadi sasa bado hawajaelewa tarehe kamili kati ya ile ya Waziri Mkuu na mapendekezo ya Rais.

“Katika kikao cha TCD na Rais, alisema uchaguzi usogezwe hadi Februari, mwakani. Ilibidi siku 90 kabla kutolewe tangazo. Walitangaza kwamba, baada ya idadi ya wapigakura kujulikana, ndipo uchaguzi ufanyike. Lakini sasa tunashangaa kutangazwa kwa siku ya uchaguzi. Lakini sisi tumeshajiandaa,” alisema Bashange.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Jumanne Sagini, alisema kanuni zimeshakamilika, ikiwa ni pamoja na uwekaji wa mipaka ya vijiji na vitongoji.

Alisema maeneo mengine walishindwa kuweka mipaka kwa ajili ya uchaguzi huo kutokana na kutokuwa katika mpango maalumu wa ardhi.

“Kuna maeneo mengine waliomba kuingizwa kwenye tarafa na vijiji, lakini ilishindikana kutokana na tatizo hilo la mipango maalumu ya ardhi katika maeneo hayo kutokuwa sawa,” alisema. 

Kuhusu ratiba, alisema msimamo tayari ulishatangazwa na Waziri Mkuu, kwamba siku rasmi ya uchaguzi ni Desemba 14, mwaka huu. 

Alisema uchaguzi huo hauna ‘makeke’ makubwa kama Uchaguzi Mkuu, kwani wasimamizi wanatoka miongoni mwa wale wanaochaguliwa na wananchi wenyewe. 

Hata hivyo, alisema hadi sasa utaratibu kuhusu maandalizi ya uchaguzi huo, ikiwa ni pamoja na mawakala na wasimamizi, unaendelea vizuri.
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa