Home »
» SAKATA LA ESCROW: KAFULILA: NILITISHWA SANA, SASA YAMETIMIA
SAKATA LA ESCROW: KAFULILA: NILITISHWA SANA, SASA YAMETIMIA
SIKU
moja baada ya Bunge kupitisha maazimio nane ya Kamati ya Kudumu ya Bunge
ya Hesabu za Serikali za Mitaa (PAC), kutokana na sakata la uchotaji
fedha kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow, Mbunge wa Kigoma Kusini, Bw.
David Kafulila (NCCR-Mageuzi), ameweka wazi usumbufu alioupata katika
sakata hilo.
Akizungumza na Majira
jana, Bw. Kafulila ambaye ndiye aliyeliibua sakata hilo bungeni,
alilishukuru Bunge kwa hatua waliyochukua baada ya kupokea ripoti ya
PAC, kuijadili na kufikia uamuzi wa kuchukua hatua kwa wahusika.
Alisema baada ya kuibua
ufisadi huo bungeni, aliingia katika vita kubwa na wabunge waliokuwa
wanatumiwa na mafisadi pamoja na mafisadi wenyewe.
"Kutokana na vitisho
nilivyokuwa nikivipata katika simu yangu ya mkononi na mitandao mingine,
niliishi kwa tabu Mjini Dodoma nikibadili hoteli...sikuishia hapo bali
nilikwenda polisi Dodoma mara mbili," alisema.
"Nilikuwa nakunywa kwa
uangalifu sana hasa nikiwa Dodoma ingawa hata Dar es Salaam nilichukua
tahadhari, ninachoweza kusema, ufisadi huu ni mkubwa uliohusisha mfumo
mzima serikalini," alisema Bw. Kafulila.
Aliongeza kuwa, hatua
tulizochukua kama Bunge zinaweza kuonekana kutosha kwa Bunge changa kama
hilo lakini kwa mabunge yaliyokomaa, sakata hilo lilitosha kuiingiza
nchi katika Uchaguzi Mkuu.
"Ni vyema Rais Jakaya
Kikwete asafishe watendaji wake Ikulu ili aweze kuendesha nchi kwa
misingi ya sheria na utawala bora...Benki ya Stanbic lazima warudishe
fedha kwa kushiriki utakatishaji fedha haramu.
"Huu ni utaratibu wa
kimataifa kama ilivyokuwa nchini Nigeria ambapo Stanbic imeingia kwenye
kashfa ikidaiwa kushiriki utakatishaji fedha takriban dola za Marekani
bilioni nane," alisisitiza Bw. Kafulila.
Juzi sakata hilo
lilihitimishwa katika hatua nzuri bungeni baada ya Bunge kuazimia
viongozi wote waliotajwa katika ripoti ya CAG wakihusishwa na sakata
hilo, wawajibishwe.
Mwenyekiti wa Kamati ya
PAC, Bw. Zitto Kabwe, alisema maazimio hayo yamefikiwa na Kamati ya
Maridhiano katika kikao kilichoshirikisha Kambi ya Upinzani, CCM na
Serikali.
Alisema Bunge hilo
limeazimia mamlaka ya uteuzi iwawajibishe na kutengua uteuzi wa Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Profesa Anna Tibaijuka na Waziri
wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Wengine ni Mwanasheria
Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati na Madini, Bw. Eliachim Maswi na wajumbe wa Bodi ya Shirika la
Umeme nchini (TANESCO).
Maazimio mengine ni
Rais kuunda tume ya kijaji ili kuchunguza tuhuma za utovu wa maadili
dhidi ya Jaji Aloysius Mujulizi na Jaji Profesa Euden Ruhangisa wa
Mahakama Kuu ya Tanzania.
Mengine ni mamlaka
husika za kifedha na kiuchunguzi ziitaje Benki ya Stanbic Tanzania Ltd
na benki nyingine yoyote itakayogundulika kujihusisha na utakatishaji
fedha zilizotolewa katika akaunti hiyo kuwa ni taasisi za utakatishaji
fedha haramu.
Bw. Kabwe aliyataja
maazimio mengine kuwa Serikali iandae na kuwasilisha muswada wa
marekebisho ya sheria iliyoiunda Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa nchini (TAKUKURU), kwa lengo la kuanzisha taasisi mahususi
itakayoshughulikia, kupambana na kudhibiti vitendo vya rushwa kubwa,
ufisadi na hujuma za uchumi zinazotishia uhai wa Taifa.
Pia walishauri Serikali
iangalie uwezekano wa kununua mitambo ya kufua umeme ya IPTL na
kuimilikisha kwa TANESCO ili kuokoa fedha za shirika hilo na Serikali
iwasilishe taarifa za utekelezaji wa mapitio ya mikataba ya umeme kabla
ya kumalizika mkutano wa Bunge la Bajeti.
Azimio lingine Jeshi la
Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama, viwachukulie hatua
stahiki za kisheria watu wote waliotajwa katika taarifa maalumu ya
kamati kuhusika na vitendo vyote vya kijinai kuhusiana na miamala ya
akaunti hiyo na wengine ambao watagundulika kuhusika katika vitendo
hivyo kutokana na uchunguzi unaoendelea.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment