MJADALA kuhusu ripoti
ya uchunguzi wa fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow iliyowasilishwa
bungeni Mjini Dodoma na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali
(PAC) na utetezi wa Serikali kuhusu sakata hilo, jana umewagawa wabunge.
Ripoti ya PAC inatokana
na uchunguzi uliofanywa na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu
za Serikali (CAG), ambapo mjadala huo ulianza jana jioni ukiongozwa na
Mwenyekiti wa Bunge ambaye ni Mbunge wa Ilala, Bw. Mussa Azzan Zungu.
Kabla ya kuanza mjadala
huo, Bw. Zungu aliwataka wabunge kuijadili ripoti hiyo kwa utulivu na
kuvumiliana lakini hali ilikuwa tofauti na maombi yake.
Wabunge waliokuwa
wakichangia mjadala huo, walitofautiana kimtazamo juu ya sakata hilo
baadhi yao wakitaka viongozi waliotajwa wawajibishwe na wengine
wakipinga.
Mbunge wa Singida
Mashariki, Bw. Tundu Lissu (CHADEMA), alisema wanaotajwa katika ripoti
hiyo lazima waachie ngazi kuanzia Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda,
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema pamoja na viongozi
wengine.
Alijenga hoja kuwa
fedha za Akaunti ya Escrow hazikuwa binafsi kwani haiwezekani fedha
binafsi zipate maelekezo ya kutolewa kwenye akaunti kwa ushauri wa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwenda Ikulu.
Alisema barua ya
kutolewa fedha hizo kwenye akaunti hiyo iliandikwa na Ikulu kwa niaba ya
Rais wakati fedha binafsi haziwezi kutolewa maelezo na Mawaziri,
Makatibu Wakuu, Mwanasheria wa Serikali wala Ikulu.
Aliongeza kuwa, kwa
msingi huo fedha hizo zilikuwa za umma hivyo waliohusika kuanzia Waziri
Mkuu, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mawaziri na wabunge, wawajibishwe na
kuwajibika.
Bw. Lissu alienda mbali
zaidi akimtaka Waziri wa Fedha, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mkuu wa
Kitengo cha Usalama wa Taifa kuwajibika kwani haiwezekani miamala ya
fedha ifanyike bila wao kujua kinachoendelea.
"Wale wanaodai fedha
hizo si za umma ni wale waliohongwa," alisema Bw. Lissu na kuongeza
kuwa, wote waliotajwa kupokea mgawo wa fedha hizo wakiwemo watumishi wa
Serikali wamelitia aibu Taifa.
Mbunge wa Muleba
Kaskazini, Bw. Charles Mwijage (CCM), alisema jambo sakala hilo ni zito
lakini kwa kuwa Kamati ya PAC imelifikisha mbele ya Bunge, linapaswa
kufanyiwakazi na maamuzi magumu yatolewe na wabunge wote.
Alisema tangu
kuanzishwa IPTL mwaka 1994, haoni sababu ya mtu kama Naibu Waziri wa
Nishati na Madini, Bw. Stephen Massele, kuambiwa awajibike kwa sababu ya
kumsema Balozi wa Uingereza na kusisitiza Bunge linapaswa kuondoa
kibuyu ambacho kimekuwa mzigo.
Aliongeza kuwa, katika
ripoti ya CAG haoni sehemu ambayo Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda,
anaguswa na kutakiwa kuwajibika na mapendekezo ya PAC kutaka mitambo ya
IPTL itaifishwe, alionya wabunge kuwa makini kwani kufanya hivyo ni
kubeba mzigo wa deni linalodaiwa na Benki ya Standard Chartered ya Hong
Kong.
Alisema deni hilo linatosha kununua mtambo mpya ukafungwa Kinyerezi na kazalisha umeme mwingi zaidi ya ule wa IPTL.
Chanzo;Majira
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment