KAULI ya Spika wa Bunge, Anne Makinda ya kuwataka wabunge kuacha kujihusisha na vitendo vya rushwa vinavyoweza kuwaingiza matatani, huku akionya watakaokutwa na hatia wataibeba misalaba yao, imepongezwa na wanasheria wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) na kutaka hatua zaidi za kiuchunguzi kuwabaini wahusika.
Makinda, alitoa onyo hilo Jumamosi usiku kabla ya kuahirishwa kwa Mkutano wa 16 na 17 wa Bunge mjini Dodoma ambapo aliwataka wabunge kuachana na watu wanaofanya ushawishi kwa kutumia fedha ili kupenyeza hoja zao.
Pongezi za LHRC zilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho ya Sera LHRC, Harold Sungusia wakati akitoa tathmini ya mwenendo wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na jinsi lilivyoshughulikia sakala la uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Tegeta Escrow katika Benki Kuu ya Tanzania (BoT).
“Kuna tuhuma za wabunge kutokuwa wasafi na kwamba baadhi yao wamekuwa wakituhumiwa kupewa rushwa ili kushinikiza maamuzi yasiyo na tija kwa taifa,†alisema Harold na kuongeza kuwa wanapongeza kauli ya Makinda kwa kuweka wazi suala hilo kwani si la kuachwa lipite, bali uchunguzi wa kina ufanyike kuwabaini wabunge wenye tabia za aina hiyo.
Alisena LHRC inazitaka mamlaka zenye dhamana ya kuchunguza mambo ya rushwa kulifuatilia jambo hilo na wale wote watakaobainika wachukuliwe hatua inayostahili kwa mujibu wa sheria.
Kadhalika alisema LHRC inalishauri Bunge kuichukulia uzito wa pekee kauli hiyo kuhusu baadhi ya wawakilishi hao wa wananchi waliopokea fedha ili kushawishiwa kupindisha ukweli na kisha Bunge liwachukulie hatua za kinidhamu ikibidi kuwafukuza ubunge.
Kuhusu uchotwaji wa fedha katika akaunti ya Escrow alisema hilo ni jambo kubwa kuliko yote na kwamba ni kipimo cha maadili ya uongozi ambapo kwa Katiba ya sasa inatoa mianya mingi ya kutozingatiwa kwa miiko ya uongozi hasa baada ya kufutwa kwa azimio la Arusha.
Kuhusu majaji kutajwa katika sakata hilo, Ofisa Programu Dawati la Serikali, Hussein Sengu alisema suala hilo linaweza kuleta athari kwa wananchi kwa kukosa imani na vyombo hivyo na wengine kutumia Mahakama kama kichaka cha kuficha maovu.
Spika wa Bunge, akizungumza mjini Dodoma, alikemea suala la rushwa miongoni mwa wabunge akisema vitendo hivyo vinawaaibisha na vitawandolea uadilifu wao katika kuisimamia Serikali.
“Kuna hili la lobbying (kushawishi) linalofanywa na wafanyabiashara. Acheni kupokea rushwa, mtaaibika. Kama ninyi sio wasafi, mtawezaje kuwasimamia wengine,†alisema Makinda.
“Hakika mtajikuta mko ndani, na sisi hatutakuja kuwasaidia. Kama chombo hicho cha kuwasimamia wananchi kitaoza, nani atawasimamia wananchi? “Wananchi wanatutegemea sisi kwa hiyo acheni vitendo hivyo, vitawaaibisha na mtatiwa ndani na mimi sitakuja kuwatoa. Kataeni vitendo hivyo,†alisisitiza Spika Makinda.
Kauli yake imekuja baada ya kuwapo kwa madai ya matumizi makubwa ya rushwa katika sakata la akaunti ya Tegeta Escrow ya BoT, ambayo ilikuwa mali ya Kampuni ya kufua umeme ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL).
Wakati wa majadiliano ya sakata hilo linalohusisha uchotaji wa Sh bilioni 306 zilizokuwa katika akaunti hiyo, baadhi ya wabunge waliwatuhumu wenzao kwa kuhongwa ili kufanikisha njama za ama kuwatetea watuhumiwa au kuwakandamiza watu wasiohusika.
Miongoni mwa waliohusishwa na sakata hilo ni viongozi wa umma, watendaji wa serikali, wafanyabiashara, majaji, ambao inaaminika kwa namna moja au nyingine walihusika kufanikisha uchotaji huo wa fedha na wengine kunufaika na fedha hizo.
Alipochangia mjadala huo, Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM), alisema sakata hilo linasukumwa na makundi manne (ingawa baadaye aliongeza moja).
Lusinde aliyataja kuwa ni wanasiasa wenye ndoto za kuwania urais mwakani, walionufaika na fedha hizo, waliokosa fedha hizo, mawakili waliokuwa wakipata fedha nyingi kutokana na malipo ya kesi mbalimbali za IPTL na benki zilizotaka kununua hisa za kampuni hiyo ya Tegeta Salasala, Dar es Salaam.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Chanzo:Habari Leo
0 comments:
Post a Comment