CHAMA cha Alliance for
Change and Transparency (ACT-Tanzania), kimewaomba wabunge wote
kuunganisha nguvu zao katika Bunge lijalo ili kupiga kura ya kutokuwa na
imani na Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, kama Rais Jakaya
Kikwete atashindwa
kutekeleza maazimio ya Bunge likiwemo la kumwajibisha na kutengua uteuzi
wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
Katibu Mkuu wa chama hicho, Bw. Samson Mwigamba, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema upo umuhimu wa
wabunge wote kuunganisha nguvuzao bila kujali itikadi za vyama ili
kumshinikiza Rais Kikwete atekeleze maazimio waliyoyatoa kwa kupiga kura
ya kumkataa Bw. Pinda ili iwe fundisho kwa viongozi wengine.
“Bunge ni sauti ya
wananchi na ndio maana linatoa maelekezo, linatunga sheria na kuisimamia
Serikali, hivyo ni chombo muhimu na ndio mhimili mkubwa zaidi kuliko
mihimili yote likiwa na uwezo wa kumwondoa Rais sasa iweje maazimio yake
yasitekelezwe,” alisema Bw. Mwigamba.
Alisema maazimio ya
Bunge yametokana na ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za
Serikali (CAG) na kuwahoji viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (TAKUKURU), lakini Rais ameshindwa kuchukua hatua badala yake
jambo hilo linafanyiwa uchunguzi.
“Bunge likipiga kura ya
kumwondoa Bw. Pinda, litajiwekea heshima kubwa ya kutambulika kama
mhimili mkubwa zaidi kuliko mihimili mingine,” alisema.
Aliongeza kuwa, kama
vyombo vinavyowachunguza viongozi ambao bado wanaendelea na kazi
vitathibitisha kuwa hawana makosa, Rais Kikwete yupo tayari kuukubali
uchunguzi huo na kuupuuza ule wa Kamati ya Bunge.
“Hakuna mtu asiyejua
kuwa Mawaziri walioondolewa baada ya kusitishwa kwa Operesheni Tokomeza
akiwemo Bw. Shamsi Vuai Nahodha, Dkt. Emmanuel Nchimbi, Balozi Hamisi
Kagasheki ambao wote hawakushika silaha wala kuua; lakini Rais alitengua
uteuzi wao mara moja kutokana na Wizara zao kuhusishwa na matukio hayo.
“Inashangaza kuona Rais
anapata kigugumizi kuhusu suala la Escrow na kushindwa kutekeleza
maazimio ya Bunge kama lilivyoshauri... Rais hana chombo kingine cha
uchunguzi zaidi ya TAKUKURU na CAG,” alisema.
Alisema maazimio yote
ya Bunge, yamelenga kulisaidia Taifa si vinginevyo sasa iweje Rais
alichukua maamuzi ya haraka katika Operesheni Tokomeza, lakini
anashindwa kuwawajibisha Mawaziri walioguswa na sakata la Escrow?
Chanzo:Majira
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment