Home » » MCHUNGAJI KORTINI KWA WIZI MIL. 9.6/-

MCHUNGAJI KORTINI KWA WIZI MIL. 9.6/-

MCHUNGAJI wa Kanisa la Anglikana, Kata ya Gulwe, Wilaya ya Mpwapwa, mkoani Dodoma, Michael Mahimbo, amefikishwa mahakamani kwa kosa la wizi wa sh. milioni 9.6.

Mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya hiyo, Paskal Mayumba, Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Michael Joseph, aliiambia Mahakama hiyo kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo kati ya Novemba 2013 na Juni 2014, kwenye Kijiji cha Berege, wilayani humo.

Alisema mshtakiwa aliiba fedha hizo ambazo ni mali ya Ruben Mlewa, ambazo alimpa ili kununulia trekta lakini alizitumia kwa matumizi mengine.

Mshtakiwa alikana shtaka hilo na yuko nje baada ya kutimiza masharti ya dhamana ambayo ni kuwa na wadhamini wawili ambao walisaini bondi ya sh. milioni tano kila mmoja. Kesi hiyo imepangwa kuitwa tena Januari 19 mwaka huu.

Wakati huo huo, watu wawili wote wakazi wa Kijiji cha Idilo, Kata Kisokwe, wilayani humo, wamefikishwa mbele ya Hakimu Mayumba wakikabiliwa na shtaka la mauaji ya mkazi wa Kijiji hicho, Henry Magalale.

Washtakiwa hao ni Musa Masila (36) na Yohane Matayo (22), ambao wote walitakiwa kutojibu lolote kutokana na Mahakama hiyo kutokuwa na uwezo wa kusikiliza shtaka hilo.

Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Joseph alisema washtakiwa walifanya mauaji hayo Desemba 17,2014, kinyume cha kifungu namba 196 na 197 cha kanuni ya adhabu namba 16 ambayo imefanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Kesi hiyo itasikilizwa tena kwa mara ya kwanza Januari 19 mwaka huu.

Chanzo:Majira

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa