Na Greyson Mwase, Dodoma
Meneja
wa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco)
mkoa wa Dodoma, Zakayo Temu amesema kuwa Serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 43.89 kwa ajili ya kujenga miundombinu
ya umeme katika mkoa wa Dodoma kupitia
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Awamu ya Pili.
Temu
aliyasema hayo mbele ya Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Nishati na Madini
iliyopo mkoani Dodoma kwa ajili ya kukagua miradi ya umeme
ili kujionea utekelezwaji wake pamoja na kuzungumza na wawakilishi wa
wananchi. Mbali na mkoa wa Dodoma, kamati hiyo
inatarajia kufanya ziara ya kukagua miradi ya umeme katika mikoa ya Singida, Arusha na Kilimanjaro pamoja na kuzungumza na wadau wa madini katika mkoa wa
Manyara.
Akitoa taarifa ya utekelezaji wa miradi ya umeme
katika mkoa wa Dodoma chini ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) Awamu ya Pili, Temu alisema kuwa mradi kabambe wa kusambaza umeme vijijini
awamu ya pili unahusisha
wilaya zote za mkoa wa Dodoma, wilaya za
Chamwino, Kongwa zikiwa mojawapo.
Akielezea
kazi ya usambazaji wa umeme katika wilaya
ya Chamwino Temu alisema kazi ya
kupeleka umeme itahusisha ujenzi wa njia
ya umeme msongo wa kilovolti 33 urefu wa kilomita 171.5 na njia ya msongo wa kilovoti 0.4 urefu wa kilomita 95.
Alisema ujenzi utahusisha pia ufungaji wa transfoma
22 za ukubwa mbalimbali pamoja na
kuunganisha wateja wapatao 1,195 kwa gharama inayokadiriwa kuwa shilingi za
kitanzania bilioni 8.67.
Aliongeza
kuwa katika wilaya ya Chamwino hadi sasa ujenzi wa miundombinu ya umeme
umefikia asilimia 52 na wateja 105 kati ya 1,195 wamekwisha unganishwa
na huduma ya umeme na kusisitiza kuwa
mradi huu unatarajiwa kukamilika
mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.
Alitaja
maeneo yatakayofaidika na umeme huu kuwa ni pamoja na vijiji
vya Fufu, Masanze, Mloda,
Handari, Chololo, Kikombo, Igandu, Msanga, Chinangali, Mwegamile, Mpera, Chamwino Ikulu, Solowu, Zajilwa, Segala, Izava, Itiso, Magungu, Osteti,
Dabalo, Nzali, Majeleko, Mlimwa, Igamba, Membe na Ikowa.
Alitaja vijiji
vingine ni pamoja na Msamalo, Makoja, Mnase, Mgunga, Mlebe, Ndebwe,
Handali, Chanhumba, Matumbulu, Igogi, Chaludema, Sazima, Nkowe, Chinyika, Chinyanguku, Nghaheleze,
Ikombolinga, Idifu, Miganga, Muungano, Ilolo, Chalinze B, Azimio B na Shule ya Msingi Chinangali II
Wakati
huo huo akielezea hatua iliyofikiwa ya
ujenzi wa miundombinu ya umeme katika
wilaya ya Kongwa, Temu alieleza
kuwa kazi ya kupeleka umeme katika wilaya hiyo inahusisha ujenzi wa njia
ya umeme msongo wa kilovolti 33 urefu wa
kilomita 197 na njia ya umeme msongo wa
kilovoti 0.4 urefu wa kilomita 66.
Alisema pia ujenzi huo unahusisha ufungaji wa transfoma 51 za ukubwa
mbalimbali pamoja na kuunganisha wateja
wapatao 1,195 kwa gharama inayokadiriwa
kuwa shilingi za kitanzania bilioni 9.24
Alisema
hadi kufika sasa ujenzi wa miundombinu
ya umeme umefikia kwa asilimia 68 na wateja 30 kati ya 1,640 wamekwisha unganishiwa umeme na
kusisitiza kuwa mradi huo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni mwaka
huu.
Alitaja
vijiji vitakavyonufaika na mradi huo
kuwa ni pamoja na Manguto, Matongoro, Nororia, Mlanje, Manyata, Ngomai,
Njoge, Chiwe, Moleti, Pingakame, Mlanje, Sejeli, Mkutani, Banyibanyi,
Mageseni, Makawa, Mkoka na Magereza Vijiji
vingine ni pamoja na Nilini, Ndurugumi,
Laikala, Mlali Ng’umbi, Mranana, Chingwilingwili, Ndalibo, Zoissa na
Chitego.
Akielezea
changamoto katika utekelezwaji wa mradi wa REA
Awamu ya Pili Temu alieleza kuwa ni pamoja na wananchi
wengi kuhitaji huduma ya umeme katika
awamu hiyo japokuwa hawapo kwenye mpango
huo kwa sasa na njia ya umeme
kutembea kwa umbali mrefu sana kupita kiwango cha kawaida na hivyo kuwa
na viashiria vya kupata umeme mdogo kwa
muda mfupi. Aidha,
alisisitiza kuwa katika utekelezaji wa mradi, baadhi ya wananchi wamekuwa
wakijitokeza kudai fidia.
Alisema ili kutatua changamoto hizo kama shirika la Tanesco litaendelea kubaini
maeneo ambayo yanahitaji umeme ili yawekwe kwenye bajeti ya Tanesco inayoandaliwa kila mwaka na
kwenye maeneo ya vijijini
shirika litaendelea kuweka miradi ya
REA kwa kadri itakavyokuwa inahitajika lengo likiwa ni kuhakikisha kila
mwananchi anafurahia huduma ya umeme.
“Pia
tutaendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya umuhimu wa miradi ya umeme hususan
vijijini kwa maendeo ya taifa ili kuondokana na dhana ya kudai fidia ambayo ni kubwa kuliko
bajeti iliyotengwa”, alisisitiza Temu.
Chanzo Jiachie Blog
Chanzo Jiachie Blog
0 comments:
Post a Comment