Home » » 'MUSWADA WA HABARI UTASAIDIA TAALUMA YA UANDISHI'.

'MUSWADA WA HABARI UTASAIDIA TAALUMA YA UANDISHI'.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk Fenella Mukangara

Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, imesema Muswada wa Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari ukipitishwa na Bunge kuwa sheria, utaweka misingi imara ya kuifanya taaluma ya uandishi wa habari na utangazaji kutambulika.
Aidha, Muswada huo ukipitishwa kuwa sheria utaboresa mazingira ya utendaji kazi wa watumishi katika vyombo vya habari nchini.
Akisoma hotuba ya wizara yake wakati akiwasilisha bungeni Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Fedha kwa mwaka wa fedha 2015/16, Waziri wa wizara hiyo, Dk. Fenella Mukangara, alisema katika Bunge la Bajeti la mwaka 2014/2015, aliahidi kwa kushirikiana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, wizara itawasilisha Muswada huo na kwamba ulisomwa kwa mara ya kwanza katika mkutano wa 19 wa Bunge.
 
Muswada huo pamoja na mambo mengine una kipengele kinachovilazimisha vituo binafsi vya utangazaji  kujiunga na chombo cha habari cha umma kwa ajili ya taarifa ya habari ya kila siku saa mbili usiku.
 
Sheria zingine ni kuweka kiwango cha elimu cha kuanzia shahada ya kwanza kwa mwandishi wa habari, mwandishi kushitakiwa moja kwa moja badala ya kuanzia kwenye chombo chake cha habari na kuzuia mtu kumiliki zaidi ya chombo kimoja ya habari.
 
Kuhusu changamoto za kuongezeka kwa mifumo na njia za mawasiliano kwa umma kama mitandano ya kijamii kwenye intaneti kunakoathiri maudhui ya taarifa zinazotolewa, alisema wizara kwa kushirikiana na Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), imevitembelea vituo mbalimbali vya utangazaji kwa madhumuni ya kutoa elimu kwa wamiliki na watumishi wa vyombo hivyo.
 
Alisema, Kamati hiyo imeendesha warsha za kuwakutanisha wadau wa maudhui wa kujitegmea, wamiliki wa vituo vya utangazaji na wamiliki wa miundombinu ya dijiti ili kuwapa fursa ya kutoa mchango wao katika kuboresha vipindi mbalimbali vinavyorushwa kupitia mfumo wa utangazaji wa dijiti..
 
Kamati ya Maendeleo ya Jamii ilisema imebaini kuwa utoaji wa fedha kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Vijana unashuka wakati idadi ya vijana inazidi kuongezeka.
 
Akiwasilisha hotuba ya Kamati hiyo, Makamu mwenyekiti, Albert Ntabaliba, alisema hali hii inaleta tishio kubwa kwani vijana ni kundi kubwa katika jamii na ndiyo nguvu kazi ya taifa la sasa na la kesho.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa