Home » » SUALA LA DK. MENGI LATINGA BUNGENI.

SUALA LA DK. MENGI LATINGA BUNGENI.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi.

Suala la Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, kutishiwa maisha na kutakiwa kwenda kuripoti polisi limezua mjadala bungeni, baada ya Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, kuitaka serikali kutoa ufafanuzi baada ya kutoa mfano wa mbunge mmoja kutishiwa maisha na Mwanasheria mkuu wa serikali, lakini alipokwenda kuripoti hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.
 
Mbilinyi alitoa kauli hiyo wakati Bunge lilipokaa kama kamati kupitisha bajeti ya wizara hiyo, kuwa bunge lililopita Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, alitishiwa maisha na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, na pamoja na kutoa ripoti polisi hakuna hatua zilizochukuliwa.
 
Akichangia katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, mbilinyi alisema: “Nataka ufafanuzi tunamsaidiaje huyu mwenyekiti ambaye maisha yake yanatishiwa,” alisema.
 
Baada ya kauli hiyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda alimtaka Mbunge kutochanganya mambo ya kisera na mshahara wa waziri na kumtaka kuegemea kwenye hoja iliyo mbele.
 
Aidha, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), Jenister Mhagama, alisimama na kutoa ufafanuzi kuwa Mbunge ametumia lugha ya dhihaka dhidi ya rais na kulitumia katika kushawishi bunge kuamini katika jambo lililotokea.
 
Mhagama alisema si kweli kuwa rais ametishia maisha ya Mengi na kumtaka Spika Makinda, ambaye kwa wakati huo alikaa kama mwenyekiti kumtaka Mbilinyi afute kauli yake.
 
Hata hivyo, Mwenyekiti alisema suala hilo ni la jinai hivyo, halikubaliki kujadiliwa bungeni na kutaka bunge liendelee kupitisha vifungu vya bajeti ya wizara hiyo.
 
Awali akisoma maoni ya Kambi Rasmi ya Upinzani, Mbilinyi alisema kambi hiyo inalaani taarifa za kutishiwa maisha kwa mmiliki wa Kituo cha Televisheni cha ITV, Dk.  Mengi, kwa madai kuwa kituo chake kimekua kikitoa habari za kiuchochezi zinazosababisha kuyumba kwa serikali ikiwamo habari za kashfa ya ufisadi wa mabilioni ya akaunti ya Tegeta Escrow.
 
Alisema sheria mpya ya habari  inalenga kuminya haki ya Watanzania kupata takwimu sahihi ambazo zinaweza kutolewa kwa usahih na wadu wengine ambao wanashiriki katika mchakato wa uchaguzi mkuu.
 
Alisema muendelezo wa malalamiko dhidi ya sheria hizo kandamizi pamoja na Muswada wa Habari ambao unaelezwa kuwa katika mkakati wa kuletwa ndani ya bunge hilo, umepingwa vikali pia na wadau wengi nchini kikiwamo Chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini (MOAT).
 
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa