Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Rais Jakaya Kikwete.
Amesema serikali haitavumilia wale watakaokaidi agizo hilo halali
na kusababisha vurugu, badala yake watachukuliwa hatua za kisheria.
Kadhalika, alisema wasidanganyike na kuilazimisha serikali kufanya
kile isichokitaka na kwamba kazi ya kulinda kura za wagombea wa nafasi
mbalimbali itafanywa na mawakala waliteuliwa na wagombea hao.
Rais Kikwete alitoa agizo hilo jana mkoani Dodoma katika kilele cha
mbio za Mwenge na maadhisho ya kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa,
Mwalimu, Julius Nyerere.
“Naagiza Watanzania wenzangu, msidanganyike kwamba mkishapiga kura
katika vituo vyenu msiondoke mfanye kazi ya kulinda kura, hilo siyo
jukumu lenu, kila mgombea ana wakala wake anayefanyakazi ya kuangalia na
kulinda kura… serikali haitavumilia kuona amani na usalama vinavurugwa,
sheria itachukua mkondo wake, narudia tena ukishapiga kura usikae
kwenye kituo, rudi nyumbani kasubiri matokeo,” alisema.
Aliongeza: “Kama mgombea umeweka wakala wako mzembe, hakuna wa
kukufanyia kazi ya ulinzi na msiwadanganye wananchi kwamba wanawake
wakishapiga kula warudi nyumbani na wengine wabaki kulinda kura,
wanawachuuza msidanganyike.”
Akifafanua zaidi, alisema kila wakala katika vituo vya kupigia kura
ana kitabu cha watu wanaostahili kupiga kura katika kituo husika kwa
hiyo hakuna ubabaishaji kila kitu kinaeleweka.
Alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi imeshatoa maelekezo ya kisheria
kwamba baada ya kupiga kura watu waondoke, ni vizuri maelekezo hayo
yakazingatiwa.
Akizungumzia usalama siku ya kupiga kura, alisema serikali
imejiandaa na kwamba katika kipindi chote cha uchaguzi hali itakuwa
salama na watakaovunja sheria watakuwa wamefanya makosa ya jinai na
sheria itachukua mkondo wake.
Akizungumzia kumbukumbu ya miaka 16 ya kifo cha Mwalimu Nyerere,
Rais Kikwete alisema hotuba zake mbalimbali zisipuuzwe na usia wake kwa
kuwa alisisitiza watu wasiwachague viongozi wasiokuwa na sifa, wapenda
rushwa na wale wasiokuwa na nia njema na amani ya Tanzania.
RUSHWA
Alisema Mwalimu Nyerere, aliwausia Watanzania wawachague viongozi wanaokemea rushwa.
Alisema kuwa rushwa bado ni tatizo na kwamba wagombea katika
uchaguzi wa mwaka huu wasiwe na kigugumizi mbele ya wananchi kuzungumzia
namna watakavyoshughulikia rushwa.
“Wapo viongozi wanaowaomba ridhaa muwachague, wanakemea rushwa na
wengine wanamung’unya kuhusu suala hilo kwa kuwa wana lengo la kwenda
kutatua matatizo yao na siyo yenu, sisi Watanzania tumieni demokrasia
tupate viongozi wazalendo,” alisema Rais Kikwete.
Aliwahakikishia wananchi kuwa serikali ijayo itapambana na rushwa kwa kasi kubwa.
Alisema zimebaki siku 10 za Watanzania kuwachagua viongozi kuanzia
ngazi ya urais, ubunge na udiwani, hivyo kila mmoja anatakiwa kutumia
demokrasia kwenda kupiga kura kumchagua kiongozi anayemtaka.
AFYA
Alisema serikali yake imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kukabiliana
maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto
na kwamba wazazi na walezi wajipange kuzungumza na vijana ili kupunguza
kasi ya maambukizi kwa vijana nchini.
“Wazazi na walezi zungumzeni na vijana kuhusu kuepuka na kujitenga
na masuala ya maambukizi ya VVU ili kupunguza wimbi la nguvu kazi ya leo
na kesho kuingia kwenye wimbi hilo,” alisema.
Akizungumzia kuhusu malaria, alisema serikali ilisambaza vyandarua
vyenye dawa nchi nzima na dawa mseto kwa ajili ya kukabiliana na maradhi
hayo na kwamba maambukizi yameshuka hadi kufikia asilimia 51 na vifo
vimepungua kufikia asilimia 70.
Kwa upande wa Zanzibar, alisema wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa na wamefikia asilimia 0.2 ya maambukizi.
Rais Kikwete alisema serikali imejenga kiwanda cha kuua viluilui
vya malaria wanapozaliwa, wasiweze kukua na kusababisha maambukizi.
DAWA ZA KULEVYA
Kuhusu dawa za kulevya, alisema serikali yake imefanikiwa kwa kiasi
kikubwa kuwabana wauzaji na wasambazaji kwa kuwa zinaathiri sana vijana
na kudhoofisha nguvu kazi ya leo na kesho.
Alisema walioathirika na dawa hizo wanaweza kutibiwa na kupona na
kwamba serikali inaendelea kutoa huduma katika vituo vyake nchini kwa
ajili ya tiba kwa warioathirika.
RC DODOMA
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Chiku Gallawa, alisema kabla ya kilele cha
maadhimisho hayo, vijana walifanya maonyesho ya ujasiriamali, pamoja na
makongamano mbalimbali kuhusu afya zao na kuinuana kiuchumi.
WAZIRI MUKANGARA
Akimkaribisha Rais Kikwete, Waziri wa Habari, Vijana Utamaduni na
Michezo, Dk. Fenella Mukangara, alisema Mwenge ulitembelea wilaya zote
na kuzindua miradi 1, 342 yenye thamani ya zaidi ya Sh. bilioni 463.5.
Alisema kwa mwaka 2016, sherehe za uzinduzi wa mbio za Mwenge zitazinduliwa mkoani Morogoro na kuhitimishwa Mkoa wa Simiyu.
Sherehe hizo zilipambwa na watoto zaidi ya 1,000 wa halaiki kutoka
shule za msingi na sekondari ambao walichora maumbo mbalimbali na
vikundi mbalimbali vya utamaduni.
Aidha wilaya na taasisi mbalimbali zilitunukiwa vyeti vya kutambua michango yao mbalimbali katika shughuli za maendeleo.
CHANZO:
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment