Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
OFISI YA WAZIRI MKUU
TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA
Mkoa wa Dodoma
Anwani ya Simu REGCOM
Simu Nambari: 2324343/2324384
E-Mail No. ras@dodoma.go.tz
Fax No. +255 026 2320046
|
Ofisi ya Mkuu wa Mkoa,
S.L.P. 914,
DODOMA.
|
Ndugu
wananchi wa Mkoa wa Dodoma, tarehe 25 Oktoba, 2015 ni siku ya Uchaguzi
Mkuu hapa nchini; ambapo, Watanzania wale wenye sifa za kupiga kura na
waliojiandikisha, watapata fursa na kutumia haki yao ya kikatiba
kuchagua viongozi mbalimbali wa nchi yetu, kuanzia Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Wabunge na Madiwani.
Maandalizi
ya kufanikisha zoezi la Uchaguzi Mkuu kwa Mkoa wa Dodoma yamekamilika.
Hadi kufikia siku ya leo tayari wasimamizi wa uchaguzi wa wilaya zote
saba za Mkoa wa Dodoma wameshapokea vifaa vyote vitakavyo tumika kwenye
zoezi la uchaguzi. Hadi tunavyozungumza sasa, vifaa hivyo vinapelekwa
kwenye vituo vya kupigia kura.
Vilevile,
wasimamizi wa uchaguzi kwenye wilaya zote saba za Mkoa wa Dodoma
wameshapokea fedha za kuendeshea uchaguzi Mkuu. Aidha, Mafunzo kwa
watendaji wote watakaoshiriki katika zoezi la uchaguzi yanahitimishwa
kwenye wilaya za Dodoma.
Mkoa
wa Dodoma tumefanikiwa kuandikisha jumla ya wananchi 1,053,136 kuwa
wapiga kura sawa na asilimia 102.74 ya lengo, ambapo lengo ilikuwa
kuandikisha watu/wapiga kura 1,025,084, Hivyo, natumia fursa hii
kuwataka wale wote waliojiandikisha kupiga kura katika Mkoa wa Dodoma,
kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya Jumapili Oktoba 25.
Vituo
vya kupigia kura vitafunguliwa kuanzia saa 1:00 asubuhi na zoezi la
kuhesabu kura litaanza saa 10:00 jioni. Natumia fursa hii kusisitiza
mambo machache ya muhimu kwenye zoezi la uchaguzi Mkuu mwaka 2015 kwa
wananchi wa Mkoa wa Dodoma na wadau mbalimbali wanaoshiriki Uchaguzi
Mkuu kama ifuatavyo:
· Wananchi
wale wenye sifa za kupiga kura, wanahimizwa kwenda kupiga kura kwa
amani na utulivu kwa kuzingatia muda na kisha kurejea makwao/majumbani
baada ya kumaliza kupiga kura.
· Viongozi
wa vyama vya siasa na wagombea wa nafasi mbalimbali wawaandae wanachama
na wafuasi wao kwenda kupiga kura, bila kuvunja sheria za uchaguzi,
taratibu na kanuni zilizowekwa; wakidumisha hali ya Amani na utulivu.
· Hairuhusiwi kwa mtu yeyote siku ya uchaguzi kufanya kampeni ya aina yoyote wala kuvaa mavazi ya chama chochote cha siasa.
· Hairuhusiwi kwa mtu yoyote kutoa Rushwa kwa lengo la kumshawishi mtu kupiga kura au kumshawishi asipige kura.
· Kila
mtu aliyejiandikisha kupiga kura atunze shahada yake ya kupigia kura na
asiitoe kwa mtu mwingine wala yeye kutumia shahada ya mtu mwingine
kwani ni kosa la jinai kutumia shahada ya mtu mwingine kupigia kura.
vilevile ni kosa kutumia shahada bandia.
· Ni
vizuri kila mmoja akahakikishe jina lake kwenye kituo
alichojiandikishia ili kupata uhakika wa kuwepo kwenye orodha na kupiga
kura kabla ya siku ya kupiga kura Oktoba 25.
· Wananchi
wote wakae katika hali ya utulivu wasiwe na hofu wala woga, Jeshi la
polisi litafanya doria mbalimbali zenye lengo la kuhakikisha kunakuwa na
hali ya Utulivu na hali ya Amani ili kila mtu apate fursa ya kushiriki
zoezi la Uchaguzi.
Kabla
sijahitimisha salamu zangu, narudia kuwasisitiza Wananchi wote wa
Dodoma wale wenye sifa za kupiga kura wajitokeze kwa wingi kupiga kura
siku ya Jumapili, Serikali imejiandaa vya kutosha na kuwahakikishia
wananchi uchaguzi Mkuu kufanyika kwa amani, utulivu na kuwa uchaguzi wa
Huru na Haki.
Nawaomba
wananchi wote wajiepushe na vitendo vyovyote vinavyosababisha vurugu na
Uvunjifu wa Amani; tuendeleze sifa yetu ya Mkoa wa Dodoma kufanya
Uchaguzi tukiwa katika hali ya usalama.
Mwisho
kabisa, nawatahadharisha wale wote wenye nia mbaya au wanaojipanga
kutaka kujaribu kuvuruga zoezi la uchaguzi au kuleta vurugu ya aina
yoyote hapa Mkoani Dodoma kuwa, vyombo vya ulinzi na usalama
vimejipanga imara na vitamshughulikia mara moja mtu huyo. Wananchi
mnaombwa kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama au kwa kiongozi
yoyote wa eneo husika.
Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.
Imetolewa na:
OFISI YA MKUU WA MKOA WA DODOMA
Oktoba 23, 2015.
0 comments:
Post a Comment