Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WAUMINI wa Kiislamu mkoani hapa wamemtaka Mufti wa Tanzania, Sheikh
Abubakari Zubeir, kutomrudisha madarakani aliyekuwa Sheikh wa Mkoa wa
Dodoma, Mustapha Rajabu kwa madai kuwa anachangia kurudisha nyuma
maendeleo ya uislamu.
Sheikh Mustafa alisimamishwa na Baraza Kuu la Waislamu Tanzania
(BAKWATA) kupisha uchunguzi ambako alidaiwa kutumia vibaya fedha, mali
na ofisi za Baraza hilo.
Walikuwa wakizungumza mjini hapa jana kwenye kikao kilichofanyika
kwenye Msikiti wa barabara ya tisa ambacho kiliongozwa na Mjumbe wa
Baraza la Ulamaa Taifa, Sheikh Hamid Masoud Jongo, na Katibu Mkuu wa
BAKWATA, Selemani Lolila.
Walisema uongozi uliokuwa chini ya Sheikh Mustafa ulikuwa na matumizi
mabaya ya fedha na mali hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya waumini wa
dini ya kiislamu.
Mmoja wa waumini hao, Ramadhan Mzazi, alisema Mufti wa Tanzania
anatakiwa kutomrudisha huku akieleza madai dhidi ya sheikh huyo kwamba
akiwa madarakani alijimilikisha baadhi ya mali za BAKWATA jambo ambalo
lilichangia kurudisha nyuma maendeleo.
“Sisi hapa Dodoma tuna shule mbili za Hijra na Jamhuri, shule hizi
zimekuwa nyuma katika maendeleo sababu kubwa ni Sheikh huyo kuzitumia
vibaya fedha zinazopatikana na walimu kila siku wanalalamika hawajapewa
fedha sababu ikiwa ni yeye.
“Kwa manufaa ya Uislamu na maendeleo yetu Waislamu namuomba Mufti
Sheikh Abubakari Zuberi, asimrejeshe madarakani kwani na sisi Waislamu
tunataka maendeleo tumechoka kila siku sisi kuwa wa mwisho,” alidai
Mzazi mbele ya viongozi hao wa BAKWATA.
Naye Awadh Mohammed alilitaka Baraza la Ulamaa kumpelekea taarifa
kuwa Mkoa wa Dodoma hawamtaki Sheikh huyo kwa madai amekuwa na kiburi
cha madaraka.
Akijibu hoja hizo, Mjumbe huyo wa Baraza la Ulamaa, Sheikh Jongo,
alisema ameyapokea malalamiko ya waumini wa kiislamu hivyo atampelekea
Mufti Zuberi kwa ajili ya kufanya uamuzi kwa mujibu wa utaratibu.
“Mshenga hauawi, haya mliyoyasema nitampelekea Mufti, jibu lolote
atakalokuja nalo mlikubali na msije mkanilaumu mimi manake mimi napeleka
kile mlinielezea,’’ alisema Sheikh Jongo.
Wajumbe wa Bakwata kwa sasa wako katika ziara ya kutatua migogoro na
matatizo katika mikoa mbalimbali. Mbali na Dodoma pia watazunguka
katika mikoa ya Mwanza, Iringa, Njombe, Ruvuma na Morogoro.
CHANZO: MTANZANIA.
0 comments:
Post a Comment