Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
WABUNGE wa kambi ya upinzani jana walitoka bungeni, huku ulinzi mkali
ukiwa umeimarishwa katika viunga vya Bunge, MTANZANIA linaripoti.
Hatua hiyo ilitokea baada ya kipindi cha maswali na majibu pamoja na
maswali kwa Waziri Mkuu alichokiongoza Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia
Ackson.
Wabunge hao wa kambi ya upinzani inayoundwa na wabunge wengi kutoka
vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), walitoka nje ya
ukumbi wa Bunge baada ya kutaka mwongozo wa mambo mbalimbali jambo
lililokataliwa na Naibu Spika Dk. Tulia.
Hatua hiyo ilikuja mara baada ya Dk. Tulia kutoa taarifa kuhusu ajali
ya kivuko cha Mto Kilombero kilichozama juzi, ambapo Serikali ilitoa
kauli juu ya tukio hilo.
Wakati Naibu Spika akitoa maelezo hayo, baadhi ya wabunge wa upinzani walisimama na kuomba mwongozo.
Hata hivyo Dk. Tulia alimpa nafasi Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko kuomba mwongozo wake.
Matiko alitumia kanuni ya 68(7) na 63(1) akidai Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa alisema uongo bungeni alipokuwa akifafanua kuhusu utoaji wa
elimu bure.
“Kwanini Waziri Mkuu anatoa maelezo ambayo hana uhakika nayo? Kwa
mfano kule jimboni kwangu kule Tarime, wanafunzi wa bweni wanatakiwa
wapeleke chakula magunia ya mahindi na mwisho wa siku michango inafikia
Sh 500,000, iko wapi dhana ya elimu bure?” alihoji Matiko.
Akijibu mwongozo huo, Dk. Tulia alisema tayari ufafanuzi ulishatolewa ya kuwapo kwa changamoto ya utoaji wa elimu bure.
Hata hivyo, kauli hiyo iliibua mzozo zaidi baada ya wabunge wa upinzani kuinuka na kudai miongozo zaidi.
Mbali na Matiko wengine walioomba mwongozo huo ni Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali
Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya na Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara wote wa Chadema.
Wabunge hao waliendelea kusimama na kupiga kelele wakiomba mwongozo
na baadae kiti kilipoelekeza shughuli nyingine, wabunge wote wa upinzani
walisimama na kuondoka wakiongozwa na Kiongozi wa upinzani bungeni,
Freeman Mbowe na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT-Wazalendo).
ULINZI MKALI BUNGENI
MTANZANIA lilishuhudia askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU)
zaidi ya 15 wakirandaranda katika viwanja vya Bunge, na wengine wakiwa
wamesimama na kutanda katika milango yote ya kuingia bungeni.
Kuimarishwa kwa ulinzi huo kumetokana na hali ya juzi, ambapo Bunge
lilichafuka wakati wa jioni pale polisi walipoamriwa kuingia ukumbini
kuwatoa wabunge wa upinzani waliokuwa wakipinga kauli ya Serikali ya
kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya vikao vya Bunge kupitia Shirika la
Utangazaji la Taifa (TBC).
BULAYA
Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya, alishangazwa na uwepo wa wingi
wa polisi bungeni na kusema ni aibu katika karne ya sasa Bunge
kuendeshwa kwa mtutu wa bunduki.
“Tumetoka kuonyesha hatukubaliani na uamuzi wa Serikali wa kuzuia
matangazao ya Bunge yasiende ‘live’ (moja kwa moja). Wamejipanga kwa
wingi wao kukandamiza haki ya wananchi ya kupata habari.
“Sisi tunajua, huu ni mkakati mpana utakaovikumba hadi vyombo
vingine, TBC ni mwanzo tu, lakini hili ni tatizo, hapa si tu wananyima
haki za wananchi, lakini wanakandamiza uhuru wa vyombo vya habari,”
alisema.
LIJUALIKALI
Kwa upande wake, Mbunge wa Kilombero, Peter Lijualikali,
alisikitishwa na hatua ya Naibu Spika kumnyima nafasi wakati akiomba
mwongozo wa kiti.
“Mara baada ya Waziri Mhagama kutoa taarifa ya ajali ya kuzama kwa
Kivuko cha Kilombero, nilisimama kuomba mwongozo ili nitoe taarifa
nilizokuwa nazo kuhusiana na tatizo hilo.
“Nilipokuwa nikiomba nafasi nilidhani hawanijui, nikasema mimi ndiye
Mbunge wa Kilombero kwa ‘attention’ zaidi, lakini bado sikusikilizwa.
“Nilitaka kutoa taarifa kwamba waziri amedanganya, yeye anasema watu
30 wameokolewa, lakini taarifa nilizonazo mimi nimepigiwa simu na
wananchi jimboni kwamba kuna watu wamefariki dunia,” alisema.
KUBENEA
Naye Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea, alisema: “Kutoka kwetu ni
mwendelezo wa hoja ya jana ya kupinga kauli ya Serikali juu ya matangazo
ya TBC.
“Lakini hoja yangu ilikuwa kutaka kujua kama ni sahihi katika nchi
kama Tanzania inayoheshimu haki za raia kuwanyima wananchi haki ya
kupata habari.
“Lakini pia katika vurugu za jana, wapo wabunge wanawake waliporwa
hereni na mikufu yao, lakini pia kuna waandishi wa habari walizuiliwa
kutimiza majukumu yao, sasa yote haya ni sahihi?” alihoji.
CHANZO ; MTANZANIA.
0 comments:
Post a Comment