Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, imejipanga kuibuka
na mikakati mipya ndani ya Bunge linalotarajiwa kuanza mjini Dodoma
Januari 27, mwaka huu.
Aidha, kambi hiyo imepanga kutangaza Baraza lake la mawaziri kivuli Januari 26, mwaka huu.
Chanzo kutoka ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema),
kimeliambia Nipashe kuwa siku hiyo atafahamika Mnadhimu wa kambi hiyo
pamoja na mawaziri kivuli wa kambi hiyo.
Kambi hiyo inaundwa na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa),
inayojumuisha vyama vya Chadema ambacho ni chama kikuu cha upinzani
Tanzania Bara, Chama cha Wananchi (CUF)ambacho ni chama kikuu cha
upinzani Zanzibar, NLD na NCCR-Mageuzi.
Chanzo hicho kimeeleza kuwa mikakati ya Kambi Rasmi ya Upinzani kwa
Bunge lijalo, itawekwa hadharani siku hiyo ikiwa ni pamoja na namna
walivyojipanga katika kuweka hoja mbalimbali.
Aidha, imebainika kuwa Ukawa inajipanga kuja na muundo mpya kwa
kuwanoa zaidi wabunge wao ili kuuonyesha umma namna walivyojiweka tayari
kuendesha serikali.
“Moja ya mambo ambayo lazima tuonyeshe tofauti, ni jinsi
tulivyokuwa tumejipanga kuongoza serikali ya awamu ya tano. Hivyo
wabunge wetu wataonekana tofauti hasa katika uchangiaji na uwasilishaji
wa hoja mbalimbali,” kilieleza chanzo hicho.
Kilisema hoja kubwa ambayo itatawala katika Bunge hilo ni hotuba ya Rais ambayo kambi hiyo imebaini kuwapo kwa mapungufu mengi.
“Mjadala wetu katika Bunge hili, utajikita katika hotuba ya Rais
aliyoitoa wakati wa ufunguzi wa Bunge Novemba, mwaka jana. Yapo mambo
mengi yenye upungufu yanayohitaji serikali kutoa ufafanuzi,” alisema.
Aidha, chanzo hicho kimeeleza kuwa pamoja na muundo mpya wa
utendaji kazi wa wabunge hao, suala la migomo ya kutoka nje pale
wanapoona Bunge linaendeshwa ndivyo sivyo, litajitokeza kama ilivyokuwa
katika mikutano ya Bunge iliyopita.
Kambi hiyo kwa sasa itaundwa na wabunge 113 wa upinzani, tofauti na Bunge la 10 waolikuwa 91.
Katika Bunge lililopita, Mnadhimu Mkuu wa Bunge alikuwa ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Bunge la 10 lilitawaliwa na mvutano baina ya wabunge wa upinzani na wa CCM.
Mara kadhaa, wabunge wa upinzani walitoka nje wakati Bunge likiendelea kuonyesha kutokukubaliana na baadhi ya hoja.
Mathalani, walitoka wakati wa uwasilishwaji wa na kujadiliwa kwa
miswada ya sheria za mafuta na gesi, mapato yatokanayo na mafuta na
gesi.
Zomea zomea pia ilitawala katika bunge hilo, kiasi cha kiti cha
Spika kushindwa kuendesha baadhi ya vikao na kulazimika kuahirisha kwa
muda.
CHANZO:
NIPASH.
0 comments:
Post a Comment