Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
MWENYEKITI wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji mstaafu Damian Lubuva
amewataka wanasiasa walioshindwa katika uchaguzi mkuu uliopita wajipange
kwa ajili ya uchaguzi ujao wa mwaka 2020 na si kuzungumza maneno ambayo
hayana tija kwa taifa.
Alitoa kauli hiyo jana mjini hapa wakati akifungua mkutano wa
tathimini wa asasi za kiraia kuhusu elimu ya mpiga kura wakati wa
uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
“Uchaguzi umekwisha wanasiasa msiwapotoshe wananchi, walioshinda
wameshinda na walioshindwa wameshindwa sasa tujipange kwa ajili ya
uchaguzi mkuu wa mwaka 2020… wanaotoa hukumu kwenye uchaguzi ni wananchi
wenyewe sio Tume wananchi kwa utashi wao huchagua wanayemtaka,”
alisema.
Alisema katika uchaguzi mkuu uliopita Tume ya Uchaguzi haikuwa na
chama wala haikupendelea chama chochote bali ilifanya kazi kwa kufuata
kanuni na taratibu za nchi na kuongeza kuwa hakuna hata mgombea mmoja
aliyekwenda tume kuonesha ushahidi kuwa aliibiwa kura.
Jaji Lubuva alisema kumekuwa na maneno kuwa tume inatakiwa ifukuzwe kutokana na kuonekana kukipendelea chama fulani.
Akitoa mfano alisema mwaka 2010 watu milioni 20 walijitokeza
kujiandikisha lakini waliopiga kura ni milioni nane na pia mwaka 2015
jumla ya watu waliojiandikisha walikuwa milioni 22.5 lakini waliopiga
kura ni milioni 15.5.
Jaji Lubuva alisema katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 kura
zilizoharibika zilikuwa 227,889 sawa na asilimia 2.65 wakati katika
uchaguzi mkuu mwaka 2015 kura zilizoharibika zilikuwa ni 402,248 sawa na
asilimia 2.5, hali ambayo inaonesha watu wakielimishwa kura
zinazoharibika zinapungua.
Mwenyekiti huyo wa tume alisema mwaka 2015 jumla ya asasi za kiraia
zilizoomba kutoa elimu ya mpiga kura zilikuwa 551 lakini asasi
zilizoruhusiwa kufanya hivyo zilikuwa 447.
CHANZO: GAZETI LA HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment