Home » » MUHONGO AISHUKIA TANESCO.

MUHONGO AISHUKIA TANESCO.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo ameliagiza Shirika la Umeme (Tanesco) kuzalisha umeme wa kutosha na iwapo halina mwelekeo huo ni vyema kuwepo na Tanesco mpya.

Aidha, amesema kupungua kwa bei ya umeme ni jambo la lazima, si hiari na kwamba umeme unatakiwa uwe wa uhakika na sio wa kubahatisha. Alikuwa akizungumza na wazalishaji wadogo wa umeme wa maeneo mbalimbali nchini kwenye mkutano uliofanyika Mtera ambapo kuna bwawa la kuzalishia umeme.

Profesa Muhongo alisema umeme unaozalishwa kwa sasa nchini hauvuki megawati 1,500 hivyo juhudi lazima zifanyike kuongeza uzalishaji wa umeme kwa kutumia vyanzo vingine kama vya nguvu ya jua, mabaki ya miwa, mkonge, kuzalisha umeme kwa kutumia taka za aina mbalimbali na mimea na taka zinazojaa chini ya miti na hata unaotokana na joto la miamba.

“Umeme tunaouhitaji unatakiwa utufikishe kwenye Power Per Capital…. kama tunalipenda taifa letu miaka 10 ijayo tujitahidi tuwe na megawati 10,000 hadi 13,000 bila hivyo tutakuwa tunajichanganyachanganya,” alisema.
“Kama Tenesco hawana mwelekeo wa kuzalisha umeme mwingi lazima tuwe na Tanesco mpya bila hivyo hatuwezi kutoka kwenye umaskini. Tunataka uchumi ukue kutoka asilimia saba hadi asilimia 10,” aliongeza.

Pia alisema wazalisha umeme wana haki ya kumuuzia umeme wanaozalisha mtu yeyote pasipo kupitia Tanesco. Kwa sasa Tanzania chanzo cha kwanza cha umeme ni gesi inayotoa asilimia 50, asilimia 35 ni umeme unaozalishwa kwa maji huku umeme wa mafuta ukiwa asilimia 15.
CHANZO: GAZETI LA HABARI LEO.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Dodoma Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa