Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
SERIKALI imebadilisha kipengele cha mwongozo wa Mpango wa Kuandaa
Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17 unaotaka mapato yote
yakusanywe na Wizara ya Fedha na Mipango.
Badala yake imesema baadhi ya taasisi za serikali zikiwamo mamlaka za
serikali za mitaa zitaendelea kutumia utaratibu wa zamani wa kukusanya
na kupanga bajeti kulingana na makusanyo yao.
Akizungumzia utaratibu huo,Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Rais Tawala
za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawene alisema
Mamlaka za Serikali za Mitaa zimepewa madaraka hivyo ni lazima zikae na
fedha zinazokusanya.
“Serikali za Mitaa zinaendesha huduma za jamii kama afya na elimu, ni
lazima ziwe na fedha. Fedha hizo ndizo tunazipeleka kwenye huduma,”
alisema Simbachawene.
Alisema hata utoaji wa elimu bure unategemea fedha hizo na haupaswi kufanyiwa siasa.
“Elimu ya bure isifanyiwe siasa, tunawapa walimu kubuni michango.
Lakini sasa tunatoa Sh540 kwa mwanafunzi kwa mwezi, kwa kuwa mwaka
haujaisha na wanafunzi wa sekondari Sh3600 kwa mwezi,” alisema
Simbachawene.
Alisema tofauti na Serikali za Mitaa, yapo mashirika ambayo hukusanya
fedha nyingi lakini hayana huduma wanazolazimika kutoa kwa wananchi
hivyo yanatakiwa kubanwa kuliko kuondoa fedha Serikali za Mitaa.
Awali akisoma hotuba ya mwongozo huo wa bajeti bungeni jana, Waziri
wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango alisema mapato yote yatakusanywa
na Wizara ya Fedha na Mipango.
“Hivyo basi, maofisa masuuli wa wizara za Serikali, wakala, taasisi,
Sekretarieti za mikoa na mamlaka za Serikali za Mitaa watatakiwa
kuwasilisha mapato yote yakayokusanywa kwenye mfuko mkuu wa Serikali na
yatagawiwa kulingana na bajeti za mafungu zitakazoidhinishwa,” alisema
Dk. Mpango.
Vilevile Waziri Mpango alisema utaratibu wa ‘retention’ uliokuwa
ukitumika awali umefutwa na badala yake mapato yote yatakusanywa na
kuwasilishwa kwenye mfuko mkuu wa Serikali na kila fungu litapewa fedha
kulingana na bajeti yake.
Hoja hiyo ililalamikiwa na baadhi ya wabunge akiwamo Mbunge wa Kigoma
Kaskazini (CCM), Peter Serukamba aliyeitaka Serikali kufikiria vyanzo
zaidi vya mapato kwa halmashauri.
Wabunge wengine waliopinga kipengele hicho ni Riziki Ngwali (CUF)
kutoka Mafia, na Mbunge wa Babati Mjini Pauline Gekul akisema utaratibu
huo ulishafanywa na Mwalimu Nyerere miaka ya 1980 na ulishindwa.
Katika hatua nyingine, suala hilo limefika kwenye vikao vya ndani vya
CCM huku wabunge wa chama hicho wakitaka hoja hiyo iondolewe.
CHANZO : MTANZANIA.
0 comments:
Post a Comment