Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
SERIKALI imeshauriwa kuchunguza kwa kina wafanyakazi wa Idara ya
Wanyamapori Kitengo cha Intelijensia kutokana na kile kilichoelezwa
bungeni kwamba wanashirikiana na majangili.
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugora (CCM) alitoa angalizo kwa Serikali
jana bungeni wakati akichangia mwongozo wa mapendekezo ya mpango wa
taifa wa maendeleo wa mwaka mmoja.
Alisema ili kuinua Pato la Taifa ni lazima serikali ishughulike na
ujangili unaotishia kwenye mapori pamoja na watalii wanaoingia nchini
akisema wapo baadhi ya polisi waliofukuzwa, lakini wameajiriwa ndani ya
idara hiyo jambo alilosisitiza kuwa ni hatari.
“Naomba nikujulishe Mheshimiwa Maghembe (Profesa Maghembe- Waziri wa
Maliasili na Utalii), hii mambo ya kuandika humu kwamba tunataka
kuboresha miundombinu, kununua zana za kupambana na majangili...maana
yake tukiendelea kukupa zana za kupambana na majangili, wanaendelea
kuzitungua (akimaanisha helikopta),” alisema.
Aliendelea kusema, “Na kwenye idara yako ya wanyamapori, na kwenye
hifadhi yako ya Ngorongoro ndiko kuna wafanyakazi wasio waaminifu,
kwenye Idara ya Intelijensia ambao wanaazimisha silaha za kivita,
wanawapa majangili halafu wanatungua ndege.”
Kwa mujibu wa Lugora, mmoja wa watuhumiwa wa kuangusha ndege
iliyosababisha kifo cha rubani hivi karibuni, aliajiriwa na idara hiyo
licha ya kuwa amefukuzwa kwa uhalifu. Alisisitiza kuwa bila wafanyakazi
wa idara husika kuchunguzwa na kusimamiwa, nchi itaendelea kuwa na
majangili hata kama serikali italeta zana za kisasa.
Akizungumzia mpango wa Serikali wa kutaka taasisi zake pamoja na
halmashauri kuweka fedha za makusanyo kwenye mfuko wa pamoja wa Hazina,
mbunge huyo alisema mapendekezo hayo ni mazuri.
CHANZO : HABARI LEO.
0 comments:
Post a Comment