Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Waziri Mkuu Kassim Mjaliwa.
Viongozi wa dini nchini wametakiwa kuendelea
kuiombea serikali ya awamu ya tano ili iendeleze kazi ya kutumbua majipu
ambayo inagusa baadhi ya watu wenye nguvu serikalini.
Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri Mkuu Kassimu Mjaliwa,
alipokuwa mgeni rasmi kwenye sherehe za kumsimika Askofu Mkuu wa Kanisa
la Evangelist Assemblis Of God Tanzania (EAGT) Dk. Brown Mwakipesile.
Majaliwa alisema ni muhimu kuiombea serikali ya awamu ya tano
inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli ambayo imekuwa ikisimamia
uwajibikaji kwa kuwa utumbuaji majipu unahitaji maombi zaidi kutokana na
kuwa na vikwazo vingi.
“Watu hawapendi kuguswa maslahi yao, mtuombee kazi ya kutumbua
majipu ni ngumu. Serikali itafanya kazi kwa kufuata sheria na taratibu
na haitamwonea mtu,” alisema.
Alisema kama kuna mtumishi ambaye anaona haendani na kasi ya
utendaji kazi awamu ya tano, apishe kwa kuwa kuna wasomi wengi
wanaohitaji ajira.
Pia alisema ili kuendelea kutoa huduma nzuri lazima mapato ya
serikali yanayokusanywa yasimamiwe na kukusanywa kwa ufasaha. Alisema
anajua kuna kundi litakasirika kutokana na utendaji kazi wao.
“Wanaosema hii ni nguvu ya soda wanajidanganya, kwani tumedhamiria
na jitihada zetu ni kuhakikisha fedha zote zinazokusanywa zinarudi kwa
ajili ya kusaidia wananchi,” alisema.
Aidha alisema kuwa serikali inaanza kupitia maeneo yote muhimu
yatakayofanya Watanzania kupata huduma kwa ukamilifu na moja ya maeneo
yatakayoangaliwa katika bajeti ijayo ni kupunguzwa kwa vifaa vya gharama
ya ujenzi.
Alisema kuna baadhi ya taasisi za dini zinazotumia vibaya nafasi za
kuingiza bidhaa bila ushuru na kuwanyima fursa wale wenye malengo
mazuri wanaotaka kuifanya kazi ya Mungu kwa uwazi na ukweli.
Waziri Mkuu pia alisema atakuwa na kikao na viongozi wa dini zote
ili kujadili mambo yanayotakiwa kufanywa kati yao na serikali ili kuwa
kitu kimoja.
Kuhusu mpango wa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari,
alisema serikali ilitenga Sh. bilioni 131.6 kuhudumia shule hizo kuanzia
Januari hadi Juni, mwaka huu.
Alisema wameanza na changamoto nyingi lakini wataendelea kuboresha
kutokana na serikali kuwa na mpango mzuri kwenye jambo hilo. Pia
alisema ubora wa elimu utaendelea kuimartishwa.
Naye Askofu Mkuu Mwakipesile alisema kanisa hilo lina malengo ya aina mbili ambayo ni ya kiroho na kimwili.
Alisema kwa sasa Kanisa hilo lina jumla ya makanisa 5,000 Tanzania nzima huku wakiwa na zaidi ya majimbo 90 na Kanda tisa.
Dk. Mwakipesile aliahidi kuwa kanisa hilo litaendelea kuombea nchi ili iwe na utulivu, amani na mshikamano.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa EAGT, Leonard Mwizarubi, alisema
kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu inaleta hamasa kubwa kwa kanisa kwa kuwa
wanaaminmi uchumi utaimarika.
Askofu Dk. Mwakipesile anakuwa Askofu Mkuu wa pili wa kanisa hilo
baada wa Askofu Mkuu wa Kwanza, Dk. Moses Kulola, kufariki dunia Agosti
29, 2013.
CHANZO:GAZETI LA
NIPASHE
0 comments:
Post a Comment