Imeandikwa na Sifa Lubasi, Dodoma
RAIS John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya
sherehe ya Siku ya Wafanyakazi Duniani maarufu Mei Mosi ambayo kitaifa
yatafanyika mkoani Dodoma.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA),
Nicholas Mgaya alisema Tucta waliwasilisha maombi rasmi ya kumuomba Rais
Magufuli kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo na tayari wamepata
taarifa rasmi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kuwa Rais amekubali kuwa mgeni
rasmi.
Mgaya alisema hayo jana mjini hapa wakati wa mkutano baina ya Mkuu wa
Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana na timu ya maandalizi ya sherehe za
Mei Mosi Kitaifa, ambao mkutano huo ulikuwa na lengo la kujadili na
kuendelea kuweka mipango na maandalizi ya kufanikisha sherehe za mwaka
huu kwa mafanikio makubwa.
Alisema ili kufanikisha sherehe za Mei Mosi, Tucta Makao makuu
watachangia nusu ya gharama zote za sherehe nzima na nusu inayobaki
itachangiwa na wadau mbalimbali wakiwemo waajiri ambapo kwa mujibu wa
Kamati ya Maandalizi Bajeti nzima ya sherehe ya mwaka huu ni Sh milioni
29.6.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa Rugimbana aliishukuru Tucta na Serikali
kwa ujumla kwa kuupa Mkoa wa Dodoma ambao ni Makao Makuu ya Nchi
heshima ya kipekee ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya sherehe ya Sikukuu
ya Mei Mosi Kitaifa mwaka huu.
Naye Katibu wa Tucta Mkoa wa Dodoma, Ramadhani Mwendwa alisema tayari
wameunda kamati ya maandalizi ya sherehe na jukumu kubwa lililoko mbele
ni kutafuta fedha na michango kutoka kwa wadau, wengi wao wakiwa ni
waajiri serikalini.
CHANZO: HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment